Logo
Chapisha ukurasa huu

بسم الله الرحمن الرحيم

 Ufisadi wa Kutafuta Ushawishi katika Demokrasia

Nchi nyingi za kidemokrasia zinaruhusu kutafuta ushawishi wa kitaasisi ambapo watu binafsi matajiri na mashirika yanafadhili kifedha wagombea wa uchaguzi kwa tegemeo lisiloelezwa na kutarajia upendeleo. Upendeleo huu wanaopatiwa kwa namna ya kisheria ambao unalinda au kuongeza maslahi ya mashirika na mara nyingi huwa dhidi ya maslahi hasa ya watu wa eneo au wananchi ambapo hutakiwa kuwawakilisha. Utafutaji ushawishi umekuwa halali Amerika, inayodhaniwa kuwa ni kidemokrasia kubwa ulimwenguni, tokea Marekebisho ya Mwanzo ya Katiba yake mwaka 1791 [1].

Muundo wa Demokrasia unaruhusu aina hii ya ufadhili wa fedha na ushawishi wa kisiasa kwa Mashirika na tabaka la matajiri kwa kuwa ni sehemu ya watu wenye haki ya kushawishi wawakilishi wa bunge katika kupitisha sheria zinazowanufaisha ummah [2]. Kwa mfano katika ufadhili kutoka kwa Mashirika ya Amerika imeripotiwa yametumia zaidi ya dolari bilioni 2.6 kwa mwaka kama ni matumizi ya ushawishi [3].

Hali kama hii haina tofauti inapolinganishwa na ile ya demokrasia kubwa zaidi duniani, India. Aina mpya ya ufadhili wa vyama vya kisiasa inayoitwa “Electoral Bonds Scheme” ilianzishwa na serikali ya NDA mwaka 2017 wakidai kuzuia miamala ya kifedha ya siri na hivyo kuondoa mapato haramu [4]. Kupitia hila hii, ufadhili wa kifedha kwa vyama vya kisiasa kutoka kwa mashirika na wafanya biashara matajiri umehalalishwa, na hivyo kuwapatia ushawishi wa kisiasa usiostahili. Mchakato huu huitwa utafutaji ushawishi. Chama tawala cha sasa hivi BJP kimepata mgao mkubwa wa Rs 1451 crore (takriban asilimia 75) katika mwaka 2019 kupitia mpango huu [5].

Nidhamu ya Demokrasia ni Uwakilishi wenye Dosari

Makampuni ya ushirika na wafanyabiashara mashuhuri muda wote hushindana kwa ajili ya ushawishi wa kisiasa kupitia ushawishi wao kwa wabunge waliochaguliwa ambao ni wawakilishi wa wananchi. Ufadhili wao unawanufaisha katika mchakato wa kisiasa katika kuwakilisha maslahi yao binafsi kuliko maslahi ya ummah. Kampeni za uchaguzi za vyama vya kisiasa zinazofanyika kila baada ya muda hujumuisha kiasi kikubwa cha fedha zinazotumika kwenye aina zote za kampeni za matangazo na kujitangaza. Ufadhili huu kutoka kwenye mashirika yanayotafuta ushawishi husaidia vyama vya kisiasa kuingia madarakani. Marejesho ya uwekezaji huu kwa mashirika yenye kutafuta ushawishi ni sheria zilizopitishwa bungeni kukidhi maslahi yao kwa gharama ya maslahi ya ummah ambao nidhamu ya kisiasa ya kidemokrasia inadai kuuwakilisha.    

Mashirika na tabaka la matajiri ndio wachangiaji wakubwa wa GDP. Kulingana na fikra ya Kirasilimali, wao ndio wazalishaji mashuhuri wa rasilimali chache wanaoweza kutosheleza mahitaji yasiyo na kikomo ya ummah. Hii hutengeneza nadharia ya kuwa ustawi wa Warasilimali ni ustawi wa watu kwa kuwa mahitaji ya watu huweza kutoshelezwa kwa kuongeza uzalishaji. Hii ndiyo sababu ya kuwa hata kanuni zikipitishwa na kuonekana zikinufaisha mashirika haya, haionekani kuwa ni tatizo kwa sababu hiyo itawasaidia kuchangia vyema katika GDP ambacho ni kipimo cha uhai wa uchumi wa nchi [6]. Nadharia msingi ya Urasilimali inadai kuwa mahitaji ya mwanadamu hayana kikomo ambapo rasilimali zinazohitajika kutosheleza mahitaji haya ni chache. Kwa hivyo, tatizo la kiuchumi katika Urasilimali ni kufanya rasilimali zipatikane kupitia uzalishaji ili kutosheleza mahitaji yasiyo na kikomo.

Nidhamu ya Kiislamu

Mwenyezi Mungu (swt) ametuletea nidhamu ya kipekee ambao umesalimika na dosari za nidhamu ya Kidemokrasia iliyotungwa na mwanadamu. Kuna namna kadhaa za kuhakiki utumiaji mbaya wa mamlaka katika nidhamu ya Uislamu unaozuia mambo ya ufisadi kama kutafuta ushawishi.

Chini ya Khilafah, ubwana ni kwa shari’ah ya Mwenyezi Mungu (swt) ambayo haiathiriwi na hisia au maoni ya watu na haiwezi kuchezewa kukidhi maslahi ya tabaka la matajiri. Hukmu za shari’ah lengo lake zinamnufaisha wanadamu na sio tabaka la matajiri kwa gharama ya ustawi wa watu. Kinyume na nidhamu ya kidemokrasia, hakuna chaguzi za vipindi katika Khilafah. Kwa mujibu wa Kipengee cha 39 na 40 cha Kielelezo cha Katiba ya Hizb ut Tahrir, hakuna ukomo wa muda wa Khalifah katika nafasi yake isipokuwa hali ya Khalifah iwe imebadilika ambapo ima moja kati ya sifa za kutawazwa zimebatilika au amepoteza uwezo wa kutekeleza majukumu yake. Zaidi ya hayo, hakuna kampeni za uchaguzi kama kwenye Demokrasia, ambapo kunahitajika fedha nyingi, kwani kazi ya kutathmini na kupendekeza kwa ajili ya Khalifah hufanywa na Majlis-al-Ummah. Majlis al-Ummah hupima vigezo vya wagombea wafaao kulingana na masharti ya mkataba na kuwasilisha hati za utambulisho kwa Ummah. Mchakato huu umeelezewa katika Kipengee cha 34.

Mahkamatul-Madhalim (Mahakama ya Dhulma) ambayo ni sehemu ya nidhamu ya Mahakama ya Khilafah huwa na ufuatiliaji juu ya ushawishi aina hii kwa maafisa wa serikali. Katika hali ya ushiriki wa matendo kama hayo ya ufisadi kwa Khalifah, Mahkamatul-Madhalim ina haki ya kumuondoa kama ilivyotajwa katika Kipengee cha 41 cha Kielelezo cha Katiba ya Hizb ut Tahrir.

Kitovu cha nidhamu ya Kiuchumi ya Uislamu ni juu ya usambazaji wa rasilimali na sio juu ya uzalishaji wa rasilimali. Uislamu unaelezea tatizo la kiuchumi ni kuwepo kwa umasikini na kutoweza kutosheleza mahitaji ya msingi kama chakula, malazi na mavazi. Muundo wa nidhamu ya kiuchumi ya Kiislamu ni kuwa huandalia njia ya kusambaa na kueneza utajiri kinyume na nidhamu ya kiuchumi ya Kirasilimali inayopelekea kukusanya utajiri katika mikono ya wachache.

Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) alisema:

«لَيْسَ لِابْنِ آدَمَ حَقٌّ فِي سِوَى هَذِهِ الْخِصَالِ بَيْتٌ يَسْكُنُهُ وَثَوْبٌ يُوَارِي عَوْرَتَهُ وَجِلْفُ الْخُبْزِ وَالْمَاءِ»

“Mwanaadamu hana haki bora zaidi kuliko kuwa na nyumba anayoishi, na nguo anayojisitiri uchi wake na kipande cha mkate na maji.” [Tirmidhi]

Hitimisho

Waislamu lazima tuipinge nidhamu hii uhadaifu ya Kidemokrasia iliyojaa ukinzani na migongano na kulingania nidhamu ya Mwenyezi Mungu (swt) yaani nidhamu adilifu ya Khilafah, nidhamu pekee inayoweza kumuondosha mwanaadamu kutoka kwenye Giza la demokrasia hadi kwenye Nuru ya Uislamu.

Mwenyezi Mungu (swt) asema:

الَر كِتَابٌ أَنزَلْنَاهُ إِلَيْكَ لِتُخْرِجَ النَّاسَ مِنَ الظُّلُمَاتِ إِلَى النُّورِ بِإِذْنِ رَبِّهِمْ إِلَى صِرَاطِ الْعَزِيزِ الْحَمِيد

“Alif Laam Ra. (A.L.R.) Hichi ni Kitabu tulicho kiteremsha kwako ili uwatowe watu kwenye giza uwapeleke kwenye muangaza, kwa idhini ya Mola wao Mlezi, uwafikishe kwenye Njia ya Mwenyezi Mungu Msifiwa.” [14:1].

Imeandikwa kwa Ajili ya Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir na

Abdul Fattaah Ibn Farooq

Vyanzo:
https://carnegieendowment.org/2019/11/25/electoral-bonds-safeguards-of-indian-democracy-are-crumbling-pub-80428
https://www.thehindu.com/news/national/supreme-court-declines-stay-on-electoral-bonds-scheme/article30605530.ece
https://www.theatlantic.com/business/archive/2015/04/how-corporate-lobbyists-conquered-american-democracy/390822/
https://en.wikipedia.org/wiki/History_of_lobbying_in_the_United_States
https://www.investopedia.com/articles/investing/043015/why-lobbying-legal-and-important-us.a
https://www.managementstudyguide.com/what-is-lobbying.htm

Template Design © Joomla Templates | GavickPro. All rights reserved.