Afisi ya Habari
Wilayah Pakistan
| H. 10 Jumada II 1447 | Na: 16 / 1447 |
| M. Jumatatu, 01 Disemba 2025 |
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Vikosi vya Pakistan Lazima Vitumwe Kuikomboa Ardhi Iliyobarikiwa ya Palestina, Sio Kutimiza Ndoto za Adui wa Mwenyezi Mungu (swt), Trump, na Mayahudi!
(Imetafsiriwa)
Kutumwa kwa vikosi vya jeshi la Pakistani Gaza kuwanusuru watu wake na kupigana na Mayahudi ambao wameendelea na operesheni ya mauaji ya halaiki huko, tangu tarehe 7 Oktoba 2023 hakukujadiliwa kamwe, kwa kisingizio kwamba Gaza iko mbali, na kwamba wajibu wa Sharia wa kuinusuru unawaangukia wale walio karibu zaidi. Lakini mara tu bwana wa serikali ya Pakistan na adui wa Mwenyezi Mungu (swt), Trump, alipoamuru serikali hii kutuma vikosi ili kufikia ndoto zake mjini Gaza, ghafla Pakistan ikawa nchi jirani na Gaza, na vikosi vya jeshi la Pakistan vimewekwa tayari kufanya operesheni za kijeshi nje ya mipaka ya kitaifa ya Pakistan. Hivyo uongo wa serikali hii ulifichuliwa kuhusu kutoweza kwake kutuma vikosi vya jeshi kuwanusuru watu wetu mjini Gaza. Usaliti wake kwao ulithibitishwa. Pia ilithibitishwa kwamba serikali hii, kama ilivyotuzoea kwa miongo kadhaa iliyopita, ni mshale katika podo la kafiri mkoloni, hasa Amerika, ambayo kwa muda mrefu imetumia serikali hii, rasilimali za nchi hii, na nguvu zake za kijeshi kufikia maslahi yake na kuitumikia katika eneo hilo. Hii hapa sasa inatumia Pakistan kufikia maslahi yake na maslahi ya umbile la Kiyahudi, hadi ifike ardhi iliyobarikiwa ya Palestina. Hii ni fedheha na aibu iliyoje, ambayo serikali rasmi ya Pakistan imetuletea!
Katika muktadha huu, kulikuwa na mkutano na waandishi wa habari uliofanywa na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Pakistan Ishaq Dar mnamo Jumamosi tarehe 29 Novemba 2025, ambao ulikuwa na udanganyifu, hadaa nyingi, na utayari wa kufanya chochote ambacho Amerika inamtaka kwa ajili ya maslahi yake muhimu, kinachowakilishwa na kuhifadhi usalama na ushawishi wa dola inayokalia kimabavu ya Kiyahudi katika Ardhi Iliyobarikiwa ya Palestina. Miongoni mwa udanganyifu huu ni:
Kwanza: Kauli ya Ishaq Dar kuhusu kupokonya silaha Hamas, “Hatuko tayari kwa hilo. Hii si kazi yetu... Kwa mujibu wa taarifa yangu, ikiwa itajumuisha kupokonya silaha Hamas, basi hata mwenzangu wa Indonesia ameelezea rasmi kutoridhishwa kwake,” na hii ni kupotosha na kudanganya. Kwani vikosi vya “amani” vilivyopendekezwa na kiongozi wa kampeni ya Kikrusedi mjini Gaza, Trump, ni jina ambalo halilingani na uhalisia, kwani ni vikosi vilivyo chini ya utawala, usimamizi, na amri ya kituo cha vita kinachoendeshwa na Amerika karibu na Gaza, kituo hicho ambacho sasa kinaratibu shughuli za mauaji na uharibifu mjini Gaza, hata baada ya makubaliano ya Sharm el-Sheikh ambapo Shahbaz Sharif na utawala wake walikuwa mashahidi wa uongo. Kwa hivyo, ni nani atakayeamini kwamba vikosi vinavyoongozwa na Amerika na Mayahudi vitakuwa vikosi vya kulinda amani, badala ya vikosi vya mamluki vinavyofanya kazi chafu ambayo Amerika na dola ya Kiyahudi wanafanya sasa?! Na kama kweli ni vikosi vya amani, vikosi hivi vitahifadhi amani ya nani?! Je, sio Amerika ya Trump inayomiliki mradi na pendekezo hili?! Imefanya nini kuhusu ukiukaji wa makubaliano ya amani unaodaiwa na Mayahudi?! Je, imewalazimisha au hata kulaani mwendelezo wa dola ya Kiyahudi wa kuwaua na kuwatesa watu wa Gaza, au imeratibu, kushiriki, na hata kusimamia operesheni za mauaji kama mfadhili mkuu, msaidizi, na mfadhili wa dola ya Kiyahudi katika mauaji yake?!
Pili: Kuhusu kupokonywa silaha kwa upinzani na kauli ya waziri, “Hatuko tayari kwa hilo. Hii si kazi yetu, bali ni ya vyombo vya kutekeleza sheria vya Palestina. Kazi yetu ni kulinda amani, si kutekeleza amani. Hakika tuko tayari kuchangia jeshi - waziri mkuu tayari ametangaza baada ya kushauriana na mkuu wa jeshi kwamba tutachangia,” huu ni uongo mwingine. Kwani ikiwa vikosi hivyo ni vya kulinda amani, je, vitawafukuza na kupigana na Mayahudi, ikiwa watafanya hatua yoyote ya kijeshi dhidi ya watu wa Gaza au upinzani?! Au watakuwa vikosi vya kuwazuia watu wa Gaza kumpinga mvamizi Myahudi, kama ilivyoainishwa na kuhitajika kwao kimataifa na na Amerika?! Basi waziri huyu anazungumzia silaha gani za upinzani?! Je, hajui kwamba Mayahudi wamewaua shahidi na kuwaangamiza wapiganaji wengi wa upinzani mjini Gaza, huku yeye na “mkuu wa jeshi anayependwa” na Trump wakiangalia na hawakusogeza msisimko kwa zaidi ya miaka miwili?! Zaidi ya hayo, je, kuunga mkono vikosi vya Mamlaka ya Palestina, ambayo inafanya kazi kama chombo cha usalama kwa Mayahudi, si kuunga mkono dola ya Kiyahudi, kupigana nao, na kujiunga na Mayahudi dhidi ya watu wa Gaza na yeyote anayesalia katika upinzani?! Dori ya vikosi hivi itakuwa kukamilisha kazi chafu iliyoanzishwa na Amerika na Mayahudi, wakisimama bega kwa bega na vibaraka wa “Mamlaka ya Oslo” ya Mahmoud Abbas ili kuondoa mabaki yoyote ya upinzani mjini Gaza na hakuna chengine zaidi.
Tatu: Kuhusu kauli ya Dar kwamba Indonesia ilitoa wanajeshi 20,000, na Waziri Mkuu Shahbaz Sharif pia alionyesha “kimsingi” kwamba Pakistan ingekubali ushiriki wake, kauli hii inaonyesha kutojua uhalisia wa umbile la Kiyahudi linalokalia kimabavu Ardhi Iliyobarikiwa na Al-Masjid Al-Aqsa iliyobarikiwa. Kwani umbile la Kiyahudi halitahitaji zaidi ya wanajeshi 20,000 wa mapigano wa Indonesia au Pakistan ili kuliangamiza na kulifuta lisiendelee kuwepo. Ushahidi wa hilo ni kutoweza kwa umbile hili kuvunja mapenzi ya watu wasio na silaha wa Gaza pamoja na wapiganaji elfu chache wa upinzani wanaobeba silaha nyepesi, licha ya usaidizi wake usio na kikomo kutoka Amerika na muungano mwingine wote wa kimataifa wa Makruseda, ikijumuisha nchi nyingi za eneo hili, hasa miongoni mwao nchi jirani: Jordan, Misri, Uturuki, Imarati, na zengine. Je, unafikiri, Bw. Dar, kwamba dola ya Kiyahudi inaweza kuhimili vikosi 20,000 vya mujahid vilivyo tayari vita kutoka kwa kipote cha wanajeshi wa Pakistan au Indonesia?!
Serikali, katika matawi yake ya kisiasa na kijeshi, inajua dori ya hila iliyopewa katika operesheni hii chafu. Kwa hivyo, inakimbilia kukwepa, kusema uongo, na kudanganya ili kuokoa aibu, ikiwa kuna uso wowote unaobaki nayo. Katika muktadha huu, inaeleweka kile kilichoripotiwa kuhusu hasira ya Waziri wa Ulinzi Khawaja Asif mwezi uliopita, ambaye “alilaani vikali kauli tata zilizotolewa na msemaji wa serikali Daniyal Chaudhry kwamba agizo la jeshi hilo lingejumuisha kupokonya silaha Hamas.” Swali kwa mtu huyu mwenye hasira: Ikiwa vikosi hivi si vya kupokonya silaha upinzani, je, vikosi hivi vitaruhusu upinzani kufanya operesheni za upinzani dhidi ya Mayahudi?! Na je, vikosi hivi vitawapa upinzani silaha na watu wa kufanya heshima ya Jihad na upinzani, au wataizuia na kupigana nayo kama ilivyoainishwa katika makubaliano ya Trump, na kama inavyotarajiwa kutokana na asili ya dori chafu ya vikosi hivi?! Kushindwa kwa Khawaja kukataa nia yake ya kushiriki katika kutuma vikosi vya mamluki vinavyofanya kazi chini ya uongozi wa Amerika na Mayahudi, na kusita kwake kuhusu maelezo, kunathibitisha kwamba atafanya kazi hiyo kama Trump na Mayahudi wanavyotaka na wameridhika nayo. Hasira yake inayodaiwa si kitu chengine ila ni kutupa vumbi machoni, kuzimua msimamo wa hila wa serikali, na kuchanganya karata ili iwe rahisi kwao kupitisha uhaini huu na kushiriki katika sura zake chafu.
Enyi Wanyoofu katika Vikosi vya Jeshi la Pakistan!
Ikiwa mtaruhusu vikosi vyenu kutumwa katika Ardhi Iliyobarikiwa ya Palestina, basi waacheni wawe vikosi vya kijeshi vya mujahid wa Pakistan ili kuikomboa Palestina nzima na kuisafisha Baytul Maqdis na mazingira yake kutokana na unajisi wa Mayahudi—na nyinyi, kwa jina la Mwenyezi Mungu (swt) mnaweza kufanya hivi ikiwa mngekuwa chini ya uongozi wa dhati unaoinua bendera ya Tawhid, sio bendera ya Umoja wa Mataifa inayokula njama dhidi ya Uislamu na Waislamu. Kwa hivyo ikamateni mikono ya uongozi wenu unaofuata kwa khiyari vidole vya Trump, wapindueni, na muwabadilishe kwa makamanda waaminifu kutoka miongoni mwenu ambao watanusuru Uislamu na Waislamu kwa kutoa nusra yao ya kijeshi (nusrah) kwa Hizb ut Tahrir, ambayo itasimamisha Khilafah Rashida kwa Njia ya Utume nchini Pakistan—na ambayo itakusanya majeshi na kuyatuma katika Ardhi Iliyobarikiwa ya Palestina, kama wakombozi kutoka kwa unajisi wa Amerika na Mayahudi, na kulipiza kisasi kwa zaidi ya mashahidi sabini elfu walioangamia katika kipindi cha miaka miwili iliyopita.
[يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا مَا لَكُمْ إِذَا قِيلَ لَكُمُ انْفِرُوا فِي سَبِيلِ اللَّهِ اثَّاقَلْتُمْ إِلَى الْأَرْضِ أَرَضِيتُمْ بِالْحَيَاةِ الدُّنْيَا مِنَ الْآخِرَةِ فَمَا مَتَاعُ الْحَيَاةِ الدُّنْيَا فِي الْآخِرَةِ إِلَّا قَلِيلٌ إِلَّا تَنْفِرُوا يُعَذِّبْكُمْ عَذَابًا أَلِيمًا وَيَسْتَبْدِلْ قَوْمًا غَيْرَكُمْ وَلَا تَضُرُّوهُ شَيْئًا وَاللَّهُ عَلَى كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ]
“Enyi mlio amini! Mna nini mnapo ambiwa: Nendeni katika Njia ya Mwenyezi Mungu, mnajitia uzito katika ardhi? Je, mmeridhia maisha ya dunia kuliko ya Akhera? Lakini starehe za maisha ya dunia kulinganisha na ya Akhera ni chache. Kama hamwendi atakuadhibuni adhabu chungu, na atawaleta watu wengine, wala nyinyi hamtamdhuru chochote. Na Mwenyezi Mungu ni Muweza wa kila kitu.” [Surah At-Tawbah 9:38–39]
Afisi ya Habari ya Hizb ut Tahrir katika Wilayah Pakistan
| Hizb-ut Tahrir: Afisi ya Habari Wilayah Pakistan |
Address & Website Tel: +(92)333-561-3813 http://www.hizb-pakistan.com/ |
Fax: +(92)21-520-6479 E-Mail: htmediapak@gmail.com |