Afisi ya Habari
Wilayah Yemen
H. 25 Rabi' I 1447 | Na: HTY- 1447 / 05 |
M. Jumatano, 17 Septemba 2025 |
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Chama cha Jumuiya ya Mageuzi ya Yemen (Islah), Sura ya Kiislamu ya Serikali Inayodai kuwa ni ya Kiislamu, Lakini iko Mbali Nao!
(Imetafsiriwa)
Mohammad Abdullah Al-Yadoumi, Mwenyekiti wa Baraza Kuu la chama cha Jumuiya ya Mageuzi ya Yemen (Islah), alitoa hotuba Ijumaa jioni, 12/9/2025, kuadhimisha miaka 35 tangu kuanzishwa kwa chama hicho, ambayo ilikuwa Septemba 13. Hotuba hiyo, iliyopeperushwa na Suhail TV na kudumu kwa zaidi ya dakika arubaini, ilijumuisha msimamo wa chama hicho juu ya masuala ya ndani na ya kimataifa.
Chama hicho cha Jumuiya ya Mageuzi ya Yemen (Islah) kilianzishwa mnamo tarehe 13 Septemba 1990, miezi michache tu baada ya kuunganishwa kwa Yemen Kaskazini na Kusini, chini ya uongozi wa Sheikh Abdullah bin Hussein al-Ahmar (Sheikh wa kabila la Hashid), na kukipa ushawishi wa kikabila na kisiasa. Islah ilishiriki katika uchaguzi wa kwanza wa bunge mwaka 1993, na kushinda takriban viti 62 kati ya 301. Iliunda muungano wa pande tatu na General People's Congress (GPC), iliyoongozwa na marehemu Ali Abdullah Saleh, na Yemen Socialist Party (YSP) kuendesha serikali hiyo. Hata hivyo, baada ya vita vya kiangazi vya 1994 na kuondolewa kwa YSP, Islah alikuwa mshirika mkuu wa serikali pamoja na GPC. Licha ya kubadilika na kuwa upinzani baada ya mwaka 1997, ilibaki kuwa mshirika madarakani kupitia Baraza la Wawakilishi, na wajumbe wake walishika nyadhifa mbalimbali katika taasisi mbalimbali za serikali hadi mwaka 2011 lilipozidi kuwa na nguvu na wajumbe wake kushika nyadhifa muhimu za uwaziri katika kile kilichoitwa serikali halali.
Ingawa kiongozi wake anakanusha kuwa na uhusiano wowote na Ikhwan al-Muslimina, lakini tangu kuanzishwa kwake, imekuwa ni tawi la kisiasa na kifikra la kundi hilo. Chama hicho kinathibitisha katika sheria zake kwamba Uislamu ndio njia yake ya kuleta mageuzi ya kisiasa na kijamii. Chama hicho kinatazamwa na watu wengi kama sura ya Kiislamu ya serikali, huku kikiibua kauli mbiu ya Uislamu. Hata hivyo, uhalisia ni kwamba Uislamu sio tu ni seti ya kauli mbiu; ni mfumo kamili wa maisha, na hakuna dola inayoutabikisha leo. Dunia inatawaliwa na ubepari. Vyama hivi vinavyonyanyua kauli mbiu ya Uislamu vinapigia debe fikra zinazochipuza kutokana na ubepari, kama vile demokrasia, jamhuri, uhuru kamili, riba, muundo wa makampuni ya biashara ya hisa (Joint-stock), ajenda ya jinsia, kushikamana na mikataba ya Umoja wa Mataifa na Azimio la Kilimwengu la Haki za Binadamu, na mafungamano fisidifu na mabovu kama vile Uzalendo. Wale wanaotetea fikra hizi zinazogongana na Uislamu, ni watu masekula, hata kama wananyanyua kauli mbiu ya Uislamu. Madhumuni yao katika kuinua kauli mbiu ya Uislamu ni kuwahadaa watu wajikusanye pambizoni mwao, kwa sababu watu ni waaminifu kwa Dini na imani zao.
Hotuba ya Al-Yadoumi haihitaji tafakuri au mazingatio ili kugundua ukubwa wa usekula uliomo ndani na umbali wake kutoka kwa Uislamu, ambao Mwenyezi Mungu aliuweka sheria na mfumo kamili maisha, Dini na dola. Al-Yadoumi alikitaja chama chake kuwa ni miongoni mwa vinara wa ujenzi wa demokrasia katika nchi yetu, na akarudia maneno ya ‘nchi’ na ‘utaifa’, na pia akagusia ubwana wa jamhuri na mafanikio ya mfumo wa jamhuri na kuomba kwa Umoja wa Mataifa na misamiati mengine.
Kwa hiyo, tumeona ni wajibu wetu kubainisha baadhi ya mambo ili picha iwabainikie watu ili watambue tofauti baina ya Uislamu na mfumo wa kibepari na fahamu zinazotokana nao:
Mfumo wa kibepari umejengwa juu ya msingi wa kutenganisha dini na maisha, na fikra hii ndio itikadi (aqida) yake. Kulingana na msingi huu wa kifikra, mwanadamu ndiye anaye asisi mfumo wake wa maisha, na ilikuwa ni lazima kuhifadhi uhuru wa binadamu, yaani uhuru wa imani, uhuru wa maoni, uhuru wa kumiliki, na uhuru wa kibinafsi. Uhuru wa kumiliki ulisababisha mfumo wa uchumi wa kibepari. Ubepari ndio sifa kuu ya mfumo huu na matokeo mashuhuri zaidi ya itikadi yake. Kwa hiyo, uliitwa mfumo wa kibepari, kwa kukiita kitu kwa sifa yake kuu. Asili ya mfumo huu ilikuwa kwamba makasisi na wafalme wa Ulaya na Urusi walitumia dini kama njia ya kuwanyonya, kuwakandamiza na kuwakamua watu. Walitumia makasisi kama chombo kwa hili. Hili lilisababisha mzozo mbaya ambapo wanafalsafa na wanafikra walishiriki, baadhi yao wakikana dini kabisa, na wengine waliitambua dini lakini wakataka itenganishwe na maisha. Mpaka maafikiano kati ya wengi wa wanafalsafa na wanafikra yalitulia juu ya wazo moja: kutenganisha dini na maisha. Hii kimaumbile ilisababisha kutenganishwa dini na dola. Je, Uislamu una upungufu kiasi kwamba tunapaswa kuuacha na badala yake kuutabanni ubepari?! Matendo yao ni maovu kiasi gani!
Demokrasia iliyotabanniwa na mfumo huu wa kibepari inatokana na ukweli kwamba mwanadamu ndiye anayeasisi mfumo wake. Kwa hiyo, taifa ndio chimbuko la mamlaka. Taifa ndilo linaloweka mifumo, kuajiri mtawala atawale, na linaweza kumvua madaraka kila linapotaka. Linaweka mfumo linaoutaka, kwa sababu utawala ni mkataba wa uajiri kati ya watu na mtawala ili kutawala kwa mujibu wa mfumo ambao watu wanauweka ili kuwatawala. Inahamisha ubwana na mamlaka kwa watu na kuwafanya kuwa chanzo cha mamlaka katika dola, ikiwemo mamlaka ya kutunga sheria inayotunga katiba na sheria. Uislamu, kwa upande mwingine, unaufanya Wahyi kuwa ndio chanzo cha sheria, na katiba na sheria zinatokana na maandiko yake pekee kupitia ufahamu wa kisheria unaofanywa na wanazuoni wa fiqh (Mujtahidina), sio watungaji sheria wa kisekula. Kwa hiyo, Uislamu umeamua ubwana ni kwa ajili ya Shariah, sio watu. Huu ni mgongano wa wazi baina ya Uislamu na demokrasia, kwa sababu mwanasiasa hawezi kuwa wa kidemokrasia isipokuwa akanushe Uislamu na kuasi maandiko ya Wahyi yanayoamrisha kushikamana na Shariah ya Mwenyezi Mungu na kukataa kila kitu chengine. Mwenyezi Mungu (swt) asema:
[وَمَنْ لَمْ يَحْكُمْ بِمَا أَنزَلَ اللَّهُ فَأُوْلَئِكَ هُمْ الْكَافِرُونَ]
“Na wasio hukumu kwa aliyo teremsha Mwenyezi Mungu, basi hao ndio makafiri.” [Al-Ma’idah: 44].
Fungamano la kizalendo wanalolipigia debe linajumuisha wanadamu, wanyama, na ndege. Hujitokeza tu wakati mtu, ardhi, na nchi zinakabiliwa na hatari, iwe kwa kushambuliwa au kukamata, na kutoweka baada ya hatari hii kupita. Kwa hiyo, inaweza kusemwa kwamba fungamano hili si sahihi kwa mtu kulichukua kama sababu ya mkusanyiko wake, maadamu ni duni, la kihamasa, na la muda mfupi. Linatokana na uaminifu kwa dola ya kitaifa inayotawala kwa mfumo wa kisekula na linatukuza mipaka bandia ya kijiografia iliyoundwa na Mkataba wa Sykes-Picot, ambao uligawanya ardhi za Waislamu katika dola dhaifu, ambao ulilazimu uundaji wa vitambulisho ili kuhalalisha tofauti za watu na kuchochea chuki na bughudha kati ya wale ambao, hivi majuzi tu walikuwa wana wa Umma mmoja wenye mizizi ya kina ya kihistoria. Uzalendo sio kigezo halali kwa Umma wa Kiislamu, kwani uaminifu lazima uwe kwa Mwenyezi Mungu. Uzalendo, kama unavyoeleweka leo, umejitolea kuhalalisha utiifu kwa serikali za kidhalimu na tawala za kisekula na kuhifadhi vijidola vidogo dhaifu, licha ya ukweli kwamba Uislamu unaharamisha Waislamu kuwa na zaidi ya mtawala mmoja. Unaamuru hata kupinduliwa kwa mtawala wa pili ikiwa atatokea na Waislamu wana Imam anayewatawala. Uzalendo pia umejitolea kutambua uhuru, ikimaanisha uhuru wa nchi za Kiislamu kila mmoja kipeke yake na mgawanyiko. Hili limepelekea kugawanyika kwa Ummah ambao Mwenyezi Mungu aliuamuru kuwa mmoja, na kuudhoofisha mbele ya maadui zake. Uzalendo umekuwa mshale wa chuki uliomwezesha mkoloni kafiri kuikalia nchi hii na kunyonya damu na rasilimali zake. Mwenyezi Mungu (swt) asema:
[أَلَمْ تَرَ إِلَى الَّذِينَ يَزْعُمُونَ أَنَّهُمْ آمَنُواْ بِمَا أُنزِلَ إِلَيْكَ وَمَا أُنزِلَ مِن قَبْلِكَ يُرِيدُونَ أَن يَتَحَاكَمُواْ إِلَى الطَّاغُوتِ وَقَدْ أُمِرُواْ أَن يَكْفُرُواْ بِهِ وَيُرِيدُ الشَّيْطَانُ أَن يُضِلَّهُمْ ضَلَالاً بَعِيداً]
“Huwaoni wale wanao dai kwamba wameamini yale yaliyo teremshwa kwako na yaliyo teremshwa kabla yako? Wanataka wakahukumiwe kwa njia ya upotofu, na hali wameamrishwa wakatae hayo! Na Shet'ani anataka kuwapotezelea mbali.” [An-Nisa’: 60]. Mwenyezi Mungu (swt) asema:
[إن هذه أمتكم أمة واحدة وأنا ربكم فاعبدون]
“Kwa hakika huu umma wenu ni umma mmoja, na Mimi ni Mola wenu Mlezi. Kwa hivyo niabuduni Mimi.” [Al-Anbiya: 92].
Ama kile kinachoitwa sheria ya kimataifa, iliibuka na kuwako dhidi ya dola ya Kiislamu ilipowakilishwa na Khilafah Uthmani. Kama dola ya Kiislamu, iliivamia Ulaya, ikitangaza jihad, na ikaanza kuziteka nchi zake, moja baada ya nyengine, ikibeba ujumbe wa Uislamu ili kuwaokoa watu wake kutokana na dhulma ya wafalme na ukasisi wa Kanisa na watu wake, hadi ikafika kwenye kuta za Vienna. Hofu na uoga vilishika nyoyo za wafalme Mkruseda na mabwana wakubwa juu ya mamlaka yao. Sheria hii inafadhiliwa na Umoja wa Mataifa, ambayo inatekeleza mipango ya wakoloni na ina historia ya giza. Iliibuka baada ya Vita Vikuu vya Pili vya Dunia baada ya kusainiwa kwa hati ya mwanzilishi wake katika Kongamano la San Francisco, kwa mpango wa Marekani mwaka 1945, kurithi kile kilichoitwa Ligi ya Mataifa, ambayo nayo ilirithi familia ya kimataifa iliyoibuka barani Ulaya katika karne ya kumi na sita ili kukabiliana na tishio la Uislamu. Shirika hili, pamoja na Baraza lake la Usalama, leo limekuwa chombo cha Marekani cha kutumikia miradi na njama zake za kikoloni dhidi ya Uislamu na Waislamu hasa, na ulimwengu kwa jumla. Kisha wanakuja wale wanaouomba, na kujikinga chini ya kivuli chake, na kunyenyekea kwa wajumbe wake! Je hawafahamu?!
Kwa kumalizia: Uislamu ni Dini na mfumo wa kilimwengu uliokuja kushughulikia maslahi ya waja kwa haki na uadilifu. Ni Dini na mfumo ulioteremshwa kupitia Wahyi, na ni imekamilika na imara, isiyo na upungufu au udhaifu. Mwenyezi Mungu (swt) asema:
[الْيَوْمَ أَكْمَلْتُ لَكُمْ دِينَكُمْ وَأَتْمَمْتُ عَلَيْكُمْ نِعْمَتِي وَرَضِيتُ لَكُمْ الإسلام دِيناً]
“Leo nimekukamiliishieni Dini yenu, na nimekutimizieni neema yangu, na nimekupendeleeni UISLAMU uwe ndiyo Dini.” [Al-Ma’idah: 3].
Je, mtu yeyote anawezaje kufikiria kwamba mfumo mtukufu kama huu wa ulimwengu na Dini imara na kamilifu kama hii, achilia mbali Muislamu, kukosa chombo cha utawala ambapo inahitaji mfumo ulioundwa na mwanadamu?! Je, hii haiashirii kwamba Dini hii na mfumo huu una upungufu, na hivyo ni upotoshaji wa kauli ya Mwenyezi Mungu:
[الْيَوْمَ أَكْمَلْتُ لَكُمْ دِينَكُمْ]
“Leo nimekukamiliishieni Dini yenu” [Al-Ma’idah: 3].
Mfumo huu imara na kamili hauna upungufu unaoweza kufidiwa na dini na mifumo mingine. Kwa hiyo, Waislamu lazima wajifunge kwenye mipaka ya mfumo wa Kiislamu pekee, ambao ni mfumo wa Khilafah, na wakatae kila kitu chengine.
Enyi Watu wetu wa Yemen: Sisi katika Hizb ut Tahrir tunakulinganieni nyinyi na Waislamu wote kwa ikhlasi, kujitolea, na mwamko kujiweka mbali na wale wanaopigia debe kushimakana na sheria za Umoja wa Mataifa na fahamu za Kimagharibi kama vile demokrasia, usekula, mfumo wa jamhuri na mengineyo. Wale wanaochochea moto wa usekula na umadhehebu unaogongana na Dini yenu ya haki. Tunatoa wito kwenu mufanye kazi nasi katika kutabikisha Uislamu kwa ukamilifu wake, kuhifadhi kitambulisho chetu cha Kiislamu, na kushiriki katika juhudi za kuregesha mfumo wa utawala wa Kiislamu chini ya Khilafah Rashida ya pili kwa njia ya Utume. Mwenyezi Mungu (swt) asema:
[يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اسْتَجِيبُوا لِلَّهِ وَلِلرَّسُولِ إِذَا دَعَاكُمْ لِمَا يُحْيِيكُمْ]
“Enyi mlio amini! Muitikieni Mwenyezi Mungu na Mtume anapo kuitieni jambo la kukupeni uzima wa milele.” [Al-Anfal: 24].
Afisi ya Habari ya Hizb ut Tahrir
katika Wilayah Yemen
Hizb-ut Tahrir: Afisi ya Habari Wilayah Yemen |
Address & Website Tel: 735417068 http://www.hizb-ut-tahrir.info |
E-Mail: yetahrir@gmail.com |