- |
- Kuwa wa kwanza kutoa maoni!
- ukubwa wa font punguza ukubwa wa font zidisha ukubwa wa font
بسم الله الرحمن الرحيم
Kauli za Kisiasa na Uchambuzi wa Kisiasa
(Imetafsiriwa)
Na: Ustath Ahmad Al-Khatwany
Habari muhimu kwa uchambuzi kwa jumla ndio msingi wa tafakari ya kisiasa. Kwa hakika, ndio riziki ya kila siku ya wanasiasa. Bila hivyo, siasa haziwezi kueleweka, uchambuzi wa kisiasa hauwezi kuwepo, matukio hayawezi kutambuliwa, na madhumuni yake husalia kutojulikani.
Umma wa Kiislamu kwa muda mrefu umekumbwa na upotoshaji wa kauli za kisiasa. Hii ni kiasi kwamba umepoteza maeneo mingi kutokana na tafsiri potofu ya kauli hizo. Khilafah Uthmaniyya, kwa mfano, ilipoteza maeneo ya Balkan si kwa sababu ya udhaifu wa kijeshi, bali kutokana na kauli mbaya na za kupotosha za kisiasa. Uingereza na washirika wake wa Ulaya walitengeneza mgogoro wa Balkan bila ya chochote, kupitia kauli pekee. Waliwahadaa Wauthmani kuamini kwamba maasi makubwa ya wananchi yalikuwa yakifanyika katika majimbo ya Balkan, ya kudai uhuru na kujitenga. Hii ni ingawa madai haya hayakuwa na msingi wa kweli. Hakukuwa na ghasia, wala hata madai ya uhuru na kujitenga. Bado uenezaji wa mara kwa mara wa kauli hizi uliwakinaisha Wauthmaniyya kuamini kwamba harakati zenye nguvu za kujitenga kwa hakika zilikuwa zikifanya kazi katika eneo hilo. Dola ilimeza chambo na kuanza kuchukua hatua ipasavyo, ambayo ilisababisha uchovu wake na upanuzi wa kupita kiasi. Hatimaye, vuguvugu la utaifa kwa kweli lilienea na kulijaza eneo hilo, hata kufikia kitovu cha dola. Hii hatimaye ilipelekea kujitenga kabisa kwa Balkan na baadaye, hadi kuanguka kwa Khilafah Uthmaniyya yenyewe.
Kwa kuanzia, na ili kuelewa umuhimu wa kauli za kisiasa katika uchambuzi wa kisiasa, ni muhimu kujua vipengee vitano muhimu vya uchambuzi wa kisiasa:
1- Mchambuzi wa masuala ya kisiasa lazima kwanza afuatilie matukio yanayotokea katika nchi zote duniani, kukusanya habari kuyahusu, na kuyapanga kwa msingi wa umuhimu, akitofautisha kati ya yale yanayotokea kwa sadfa na yanayokusudiwa. Kwa ufuatiliaji wa kuendelea, uzoefu, na kupita kwa muda, ufuatiliaji huu unakuwa wa kitaalamu. Kisha mchambuzi hukuza uwezo wa kuchagua kile ambacho ni muhimu zaidi, na kile ambacho ni cha makusudi na muhimu.
2- Mchambuzi anahitaji maarifa ya awali ya msingi kuhusu hali ya matukio, mahali, watu na taarifa kama vile habari za kijiografia, kihistoria, kisiasa na kifikra, ili kufahamu kwa usahihi na kuelewa kwa kina matukio hayo na ripoti za habari.
3- Mchambuzi anapotaka kutoa uamuzi wa kisiasa, ni muhimu ushikamane na kanuni mbili zisizotenganishwa, na zinazofungamana:
a) Kutoyatenga matukio na dhurufu zake, muktadha, na mambo yanayohusiana nayo, kwa sababu kutenganisha matukio na yale yanayoyazunguka, na yanayohusiana nayo, kunayavua thamani yake, na kuyatenganisha na uhalisia.
b) Kuepuka kuchukua uamuzi wa kijumla na ulinganisho wa kina, kwa sababu uamuzi wa kijumla na hoja za mlinganisho (qiyas) hazina nafasi katika siasa. Kwa hakika, ni dosari kwa wanasiasa, na miongoni mwa viashiria muhimu vya kufeli katika uchambuzi wa kisiasa.
4- Kuchunguza habari na matukio kunahusisha, kwanza, kuthibitisha usahihi wake kupitia vyanzo vinavyotegemeka; pili, kuziunganisha na wakati zilipotokea; tatu, kuzichunguza ndani ya muktadha wa hali ziliyotokea; nne, kuelewa lengo lililokusudiwa nyuma ya wakati uliolengwa; na tano, kuangalia athari za mara moja kwao, kutoka kwa pande zote zinazohusika.
5- Kuunganisha tukio, au habari, kwa habari iliyopatikana hapo awali kuihusu. Kisha kuunganisha tukio na mifumo husika ya uchambuzi inayotekelezeka kwake na habari mithili ya hizo. Hatimaye kutoa hukmu ambayo inaaminika kuwa ndiyo iliyo karibu zaidi na usahihi, na inayolingana zaidi na uhalisia.
Kushindwa kuzingatia vipengee hivi katika uchambuzi wa kisiasa, na ushughulikiaji usio sahihi wa kiasi kikubwa cha kauli na habari zinazofurika kwenye vyombo vya habari vya leo na mitandao ya kijamii, pamoja na mbinu chafu zinazotumiwa kuziunda na kuzielekeza, bila shaka husababisha upotoshaji hatari wa habari na mkanganyiko wa kisiasa. Mkanganyiko huu huzichanganya akili, hupotosha fikra, hugeuza ufahamu kutokana na uwazi, na huelekeza fikra mbali na hukmu sahihi. Matokeo yake ya kimantiki ni kutokea kwa makosa mabaya ya kisiasa ambayo huwapotosha wachambuzi katika kufikia mahitimisho sahihi, na kuwafanya waanguke kwenye mitego ya mashirika ya kijasusi ya kimataifa. Hili, natija yake, lina taathira mbaya kwa Ummah na kwa wale wanaojitahidi kuleta mwamko wake.
Hivyo basi, ni muhimu kuzingatia vipengee hivi muhimu zaidi, kufuatilia kwa karibu habari nyingi zinazohusiana na matukio, kuchukua tahadhari wakati wa kushughulikia taarifa za kisiasa zinazotolewa na wanasiasa katika nchi kubwa na zenye ushawishi, na kufanya jitihada za kuelewa dhamira ya kauli hizi, kabla ya kuanza kuzichambua na kabla ya kuziunganisha na mifumo imara ya kisiasa inayojulikana kwetu.
Kwa mfano, wanasiasa wa Marekani walitoa kauli wakipendekeza kwamba vita na Iran vina karibia. Haya yaliambatana na kupelekwa kwa meli za kubeba ndege za Marekani hadi Mashariki ya Kati, pamoja na shehena za makombora na silaha za aina mbalimbali. Wakati huo huo, tahadhari ilitolewa kwa kambi ya Wamarekani na Waingereza huko Diego Garcia katika Bahari ya Hindi, na kusisitiza kwamba iko nje ya masafa ya kufika makombora ya Iran, na kwamba itacheza dori kubwa katika vita vijavyo. Ripoti hizi na matukio haya yaliunda mazingira ya vita na kutoa hisia kwamba vilikuwa karibu. Kisha, ghafla, habari kinzani zikaibuka kuhusu mazungumzo ya moja kwa moja yanayofanyika nchini Oman kati ya wajumbe wa Marekani katika Mashariki ya Kati, na maafisa wa Iran. Ilitangazwa kuwa raundi ya kwanza ya mazungumzo ilihitimishwa kwa hisia chanya, kana kwamba habari zote zinazohusiana na vita zimekuwa tu utangulizi wa kimaumbile wa kuanzisha msururu mrefu wa mazungumzo kati ya nchi hizo mbili.
Kadhalika, habari zinaendelea kumiminika kuhusu vita vinavyoendelea vinavyofanywa na Mayahudi dhidi ya Ukanda wa Gaza, zikionyesha kwamba watu wa Gaza hawana chaguo ila kuhama makaazi yao au kifo, na kusisitiza juu ya haja ya kusalimisha silaha za upinzani na viongozi wake kuondoka. Kisha, habari zinaibuka kuhusu mafanikio ya karibu ya mazungumzo yaliyofadhiliwa na Marekani. Amerika hiyo hiyo ambayo inataka kugeuza Gaza kuwa miradi ya mali isiyohamishika sasa inadai kuwa itaihakikishia Hamas kwamba umbile la Kiyahudi itajitolea kuendelea na awamu ya pili ya mazungumzo, eti ikiwemo kumalizika kwa vita na kujiondoa kutoka Gaza.
Iwapo wachambuzi wa masuala ya kisiasa wangechukua kauli za wanasiasa kijuu juu kwa mara ya kwanza na kujenga uchambuzi wao juu yake, mahitimisho yao yangekuwa kinyume kabisa na uhalisia. Wangeangukia kwenye udanganyifu katika kushughulikia mawimbi hayo ya kauli kinzani.
Kwa hivyo, kabla ya kuanza uchambuzi wowote, ni muhimu kungojea kwa subira na kwa uangalifu wakati wa kupokea taarifa za kisiasa. Ni baada tu ya hapo ndipo mtu anapaswa kuendelea na uchunguzi, uunganishi wa muktadha, kuepuka kutenganisha matukio, na kujiepusha na utoaji hukmu ya kijumla.