- |
- Kuwa wa kwanza kutoa maoni!
- ukubwa wa font punguza ukubwa wa font zidisha ukubwa wa font
بسم الله الرحمن الرحيم
Maandamano ya Umwagaji damu nchini Indonesia na Chanzo Chake
(Imetafsiriwa)
Gazeti la Al-Rayah - Toleo 565 - 17/09/2025 M
Na: Ustadh Abdullah Aswar
Tangu tarehe 25 Agosti, 2025, Indonesia imekuwa ikishuhudia wimbi la maandamano makubwa yaliyorekodiwa katika maeneo 107 katika mikoa 32. Huku baadhi ya maandamano yakiendelea kuwa ya amani, mengi yalizidi kuwa ghasia zilizohusisha uharibifu na uchomaji moto. Maeneo kadhaa yalishuhudia machafuko makubwa zaidi, ikiwemo mji mkuu Jakarta, Java ya Kati, Java Mashariki, Java Magharibi, Yogyakarta, Sumatra Kaskazini, Nusa Tenggara Magharibi, Sulawesi Kusini, na Kalimantan Magharibi. Vituo vya umma, afisi za serikali, na hata mali za usalama wa taifa zilipata uharibifu mkubwa. Jijini Jakarta, kwa mfano, vituo 22 vya mabasi ya TransJakarta na vituo vya treni ya chini ya ardhi vya MRT viliharibiwa, huku hasara ikikadiriwa kuwa karibu rupiah bilioni 50.4 za Indonesia.
Huko Makassar, Sulawesi Kusini, majengo ya baraza la bunge la mkoa na manispaa (DPRD) yalichomwa moto na kusababisha vifo vya watu watatu na majeruhi watano. Ghasia kama hizo zilizuka katika miji mingine, zikilenga afisi za bunge, makao makuu ya serikali za mitaa, vituo vya polisi, majumba ya kumbukumbu, makaazi ya viongozi na vifaa vya umma kama vile taa za barabarani, kamera za CCTV na miundombinu ya usafirishaji, ambayo yote yalipata uharibifu mkubwa.
Pamoja na uharibifu wa miundombinu muhimu, ghasia hizi ziligharimu maisha ya watu wasio na hatia na kusababisha hasara inayokadiriwa kufikia makumi hadi mamia ya mabilioni ya rupia kwa serikali.
Maandamano ya kwanza yalizuka kati ya Agosti 10 na 13 huko Pati, Java ya Kati, yaliyochochewa na pendekezo la kuongeza ushuru wa ardhi na majengo (PBB-P2) hadi 250%. Ongezeko la ushuru pia lilitokea katika maeneo mengine, na kufikia juu kama 1000% huko Cirebon. Ongezeko hili lilitokana na upunguzaji wa bajeti ya eneo ya 2025-2026 uliowekwa na Rais Prabowo Subianto, unaofikia dolari bilioni 234, ambao ulipunguza fedha za mkoa kwa robo hadi dolari bilioni 40 pekee, kiwango cha chini zaidi katika muongo mmoja. Hii ililazimisha serikali za mitaa kuongeza ushuru wa mali na ardhi. Wakati huo huo, matumizi ya ulinzi yalipanda kwa 37%, na mpango wa chakula cha bure uliongezeka karibu mara mbili hadi dolari bilioni 20.5.
Muda mfupi baadaye, kati ya Agosti 15 na 20, maandamano yalienea hadi Jakarta, yakilenga marupurupu ya kifahari ya wabunge, hasa posho ya nyumba ya kila mwezi ya rupiah milioni 50 (kama dolari 3,000), ambayo ni mara kumi ya mshahara wa chini zaidi katika mji mkuu.
Kufikia Agosti 25, maandamano yalikuwa yamefikia miji mikubwa kama vile Bandung, Makassar, Medan, na Bali, huku matakwa yakiwa kuanzia kufuta sera za urafiki wa kipote cha mabepari hadi kuvunjwa bunge (DPR). Hasira ya umma iliongezeka baada ya matamshi ya uchochezi ya wabunge fulani, ikiwemo kuwaita wakosoaji kuwa “watu mabwege zaidi duniani,” jambo ambalo lilizidisha hasira. Mnamo Agosti 28, maelfu ya waandamanaji, wanafunzi, wafanyikazi, na madereva wa teksi za pikipiki za programu, walipambana na vikosi vya usalama mbele ya jengo la bunge jijini Jakarta, wakitaka marekebisho ya leba, kukomeshwa kwa uajiri wa wafanyikazi, na nyongeza ya mshahara wa chini.
Tukio la kusikitisha lilitokea wakati dereva wa teksi ya pikipiki, Affan Kurniawan, aliuawa baada ya kugongwa na gari la polisi usiku wa Agosti 28. Kifo chake kilizua ghadhabu iliyoenea na kuchochea ghasia katika miji mingine.
Maandamano nchini Indonesia si tu kuhusu kodi kubwa na marupurupu ya kifahari ya wabunge, bali yanaonyesha mkusanyiko wa hasira ya umma kutokana na kushindwa kwa muda mrefu kwa serikali kukidhi matakwa ya watu wake, iwe chini ya tawala zilizopita, au ndani ya chini ya mwaka mmoja wa utawala wa Rais Prabowo, hasa katika nyanja ya kiuchumi, pamoja na ukosefu wa huruma wa kipote cha wanasiasa kwa mateso ya watu.
Kwa mujibu wa data ya Benki ya Dunia kutoka 2023, karibu 60% ya wafanyikazi wa Indonesia bado wanategemea sekta isiyo rasmi, bila mapato ya kudumu au ulinzi wa kijamii. Mambo yalizidi kuwa mabaya kutokana na kupungua kwa tabaka la kati, huku mamilioni ya watu wakiingia kwenye mabano ya kipato cha chini, au kurudi kwenye umaskini.
Data kutoka Kituo cha Mafunzo ya Kiuchumi na Sheria (CELIOS) zinaonyesha kuwa takriban Waindonesia milioni 10 walipatia mzoroto wa kiuchumi katika kipindi cha miaka mitano iliyopita. Wakati huo huo, bei za vyakula zilipanda, nafasi za kazi zilipungua, na zaidi ya wafanyikazi 42,000 walifutwa kazi tangu mapema 2025. Katikati ya mgogoro wa kiuchumi, serikali ilitoza viwango vya juu vya kodi na kuongeza ada kubwa mpya kwa miamala ya umma. Iliposhindwa kufikia malengo yake ya mapato kutokana na ukuaji mdogo na kuongezeka kwa deni, iliamua kupunguza bajeti na kuelekeza fedha kwenye miradi mikubwa ya kipaumbele. Wakati huo huo, posho za wabunge ziliongezwa.
Katikati ya mateso ya watu, video moja ilisambaa kwenye mitandao ya kijamii ikiwaonyesha wabunge wakicheza wakati wa kikao cha kila mwaka cha bunge mwezi Agosti, mara baada ya kutangazwa kwa nyongeza ya posho ya nyumba.
Kiuhalisia, Indonesia ni nchi yenye uwezo mkubwa wa maliasili. Inashika nafasi ya kwanza ulimwenguni katika uzalishaji wa bati na nikeli, ya tatu kwa makaa ya mawe, na ya sita kwa dhahabu. Ilhali rasilimali nyingi hizi zinadhibitiwa na sekta binafsi, za ndani na nje. Kwa mfano, China inadhibiti takriban 75% ya hisa za nikeli za Indonesia.
Kivitendo, mapato mengi ya serikali hutoka kwa ushuru, ambayo huchangia zaidi ya 80% ya mapato yote. Hii ina maana kwamba mapato ya maliasili huchangia chini ya 20%, ikishirikiwa na mali nyingine zinazomilikiwa na serikali.
Udhibiti huu wa kina wa kibinafsi juu ya mali za kimkakati za kitaifa umeongeza pengo katika uadilifu wa kijamii. Kila serikali inapokabiliwa na nakisi ya bajeti, njia pekee ya serikali ni kutoza ushuru na ada zaidi kwa watu. Mzunguko huu umewaingiza wananchi katika dhiki na hasira zaidi.
La kusikitisha, matakwa yaliyotolewa na waandamanaji na wafanyaji ghasia yamesalia kwa kiasi kikubwa kindoto, yakilenga kufuta posho ya nyumba ya wabunge. Bado mizizi halisi ya tatizo iko katika muundo wa kisiasa na kiuchumi wa nchi, uliojengwa juu ya ubepari.
Kiuchumi, kanuni ya umiliki kamili wa kibinafsi inawawezesha mabepari na mabwenyenye kudhibiti rasilimali za kimkakati za kitaifa. Kisiasa, kupitia mfumo wa kidemokrasia, wanalinda maslahi yao ya kiuchumi iwe kupitia uchaguzi, vikundi vya ushawishi, au vitendo vya ufisadi kama vile hongo.