Logo
Chapisha ukurasa huu

بسم الله الرحمن الرحيم

Jinsia na Ufeministi ni Miradi ya Kubadilisha Utambulisho
Na: Ustadh Ahmad Al-Shamali
(Imetafsiriwa)

Gazeti la Al-Rayah – Toleo 570 - 22/10/2025 M

Harakati za ukombozi wa wanawake zimeibuka katika jamii za Magharibi, zikikumbatia mawazo potofu yanayotaka ukombozi kamili wa wanawake. Hii ni kutokana na dhulma na kunyimwa haki za msingi za wanawake ambako wamefanyiwa, chini ya mfumo wa kisekula ambao umewaingiza katika taabu na unyonge.

Magharibi, kupitia mashirika yake ya kimataifa, imefanya kazi kwa bidii kusafirisha ufisadi huu kwa nchi za Kiislamu, ikitumia vyama vyenye tashwishi vinavyohusishwa na balozi zake kwa ajili ya ufadhili, usaidizi, na ukuzaji, kwa lengo la kuharibu familia ya Kiislamu na kubadilisha fahamu za Kiislamu kuhusu wanawake. Ili kufanikisha hili, ilianzisha mikataba ya kimataifa kama vile Mkataba wa Kuondoa Aina Zote za Ubaguzi dhidi ya Wanawake (CEDAW) mnamo 1979 na Mkataba wa Kuondoa Aina Zote za Ubaguzi dhidi ya Wanawake (CEDAW) mnamo 2011. Pia ilifanya makongamano mingi ya kimataifa, haswa Kongamano la Wanawake jijini Mexico City mnamo 1975, Kongamano la Copenhagen mnamo 1980, Kongamano la Idadi ya Watu na Maendeleo jijini Cairo mnamo 1994, na Kongamano la Beijing mnamo 1995.

Mtu yeyote anayefuatilia shughuli za mashirika haya atagundua wazi mafungamano yao ya karibu na Magharibi, inayoongozwa na Marekani. Yanapokea ufadhili mkubwa kutoka kwa Mfuko wa Fedha wa Kimataifa, Benki ya Dunia, na mashirika mengine ya kimataifa, yote yakihudumia maslahi ya dola kubwa na sera zao, yenye lengo la kutia usekula na umagharibi kwa Waislamu, na kuwapotosha kutoka kwa Dini yao na mafundisho yake.

Mashirika haya yanabeba kaulimbiu nzuri kama vile “wanawake na elimu,” “wanawake na vyombo vya habari,” na “uwezeshaji wa wanawake kiuchumi.” Kwa kweli, huingiza fikra hatari katika jamii, hasa miongoni mwa wanawake, ikiwemo: usawa kamili kati ya jinsia, kuwakomboa wanawake kutokana na vikwazo vya Dini na familia, uhuru wa kimwili na kibinafsi, na ubadilishaji jinsia. Lengo la kaulimbiu hizi za kupotosha ni kuwadanganya wanawake, kuvunja familia ya Kiislamu na kuihujumu kutokea ndani, ili vizazi vipotee, na hukmu za Sharia za Kiislamu zinazohusiana na wanawake na familia zifutwe.

Hata hivyo, wanawake Waislamu hawahitaji vyama hivi au mtu yeyote anayedaiwa kutafuta kuwatendea haki. Uislamu umewahakikishia haki zao kamili na kuwaona kama mama, dada, mke, na binti. Umewafanya kuwa heshima ambayo lazima ihifadhiwe. Umewapa wanaume jukumu la kuwalinda, kuwatunza, na kuwatendea wema. Umeweka usimamizi wa mume juu ya mkewe kwa msingi wa utunzaji, sio udhalimu. Pia umewapa wanawake haki ya elimu, urithi, kuchagua mwenza, kujihusisha na biashara, kilimo, na viwanda, kushughulikia mikataba na miamala, kumiliki aina zote za mali, kukuza utajiri wao, na kusimamia mambo yao. Umewaruhusu kuteuliwa katika nyadhifa za kiidara za dola na kushiriki katika maisha ya kisiasa kwa kuwachagua wajumbe wa Baraza la Kitaifa na hata kutoa Bayah ya utiifu kwa Khalifa.

Kwetu sisi, wanawake ni kina mama tunaowatendea wema ili wawe njia yetu ya kuelekea Peponi. Mtume (saw) amesema kuwahusu, «فالزَمها فإنَّ الجنَّةَ تحتَ رِجلَيها» “Jitolee kwake, kwani Pepo iko chini ya miguu yake.” Pia ni mke tunayemtendea mema kwa kumtii Mwenyezi Mungu (swt) na Mtume Wake (saw). Mtume (saw) amesema, «خيرُكُم خيرُكم لِأهْلِهِ، وَأَنَا خيرُكم لِأَهْلِي»   “Mbora wenu ni bora kwa familia yake, na mimi ni bora kwenu kwa familia yangu.” Hao pia ni mabinti tunaowafanyia wema ili wawe ngao yetu na Moto Siku ya Kiyama. Mtume (saw) amesema, «مَنِ ابْتُلِيَ مِنَ البَنَاتِ بشيءٍ، فأحْسَنَ إلَيْهِنَّ كُنَّ له سِتْراً مِنَ النَّارِ»  “Atakayejaaliwa mabinti wawili, na akawatendea wema, watakuwa ni pazia yake kutokana na Moto.” Ni wanawake ambao Uislamu umewaheshimu kwa jumla. Mtume (saw) amesema, «نعم إنما النِّساءُ شقائقُ الرِّجالِ» “Ndio, hakika wanawake ni mapacha ya wanaume.

Ufeministi, kimsingi, ni falsafa ya Magharibi iliyotokana na migongano ya kihistoria. Huutazama uhusiano kati ya wanaume na wanawake kutoka kwa mtazamo wa usawa na migongano, sio kukamilishana. Kwa hivyo inatoa wito wa kuondolewa kwa tofauti za kimaumbile kati yao, na inaona kile kinachoitwa “familia ya kale” kama kizuizi kwa uhuru wa wanawake. Inakuza kauli mbiu ya usawa kamili kwa maana ya kufuata ulinganifu, inatoa wito wa uhuru wa kijinsia, na kupunguzwa, au wakati mwingine hata kukomeshwa, kwa dori ya umama. Inatafuta kuwatelekeza na kuwatenga wanaume. Matokeo ambayo jamii za Magharibi zimevuna kutokana na mjadala huu ni kuporomoka kwa familia, huku wanawake wakibeba mzigo maradufu wa kazi na kulea watoto peke yao, pamoja na kukabiliwa na unyonyaji katika soko la ajira na mahusiano ya karibu ya kawaida, na kupoteza usaidizi wa asili wa waume na familia.

Wakati mazungumzo ya ufeministi yanapotaka usawazishaji wa jinsia, yanalenga kuhujumu akili ya kawaida na kuendeleza upotofu wa kijinsia, kwa kukuza ndoa za jinsia moja na mabadiliko ya kijinsia. Hii imechangia kuenea kwa machafuko ya kimaadili na kijamii, kuongezeka kwa mahusiano yasiyo imara, na kuanguka kwa fahamu ya stara ya kimwili na kujitolea, na kusababisha migogoro ya utambulisho na kuvuruga miundo ya kijamii.

Miradi ya ufeministi na ya kijinsia inahujumu utambulisho wa kimaumbile wa wanadamu. Wanadai kwamba jinsia ya kimaumbile ni muundo wa kijamii ambao unaweza kubadilishwa, huku Uislamu ukithibitisha kwamba Mwenyezi Mungu (swt) aliwaumba wanadamu mwanamume na mwanamke,

[وَأَنَّهُ خَلَقَ الزَّوْجَيْنِ الذَّكَرَ وَالْأُنثَىٰ]

“Na kwamba Yeye ndiye aliye umba jozi, dume na jike.” [Surah An-Najm 45], ambayo ni kanuni ya kimaumbile, isiyobadilika. Mapendekezo haya pia yanagongana na hukmu za Kiislamu zinazoegemea juu ya tofauti ya kimaumbile kati ya wanaume na wanawake, kama vile zile zinazohusiana na urithi, talaka, na uangalizi wa kifedha.

Miradi hii haiishii tu katika kutetea usawa rasmi. Badala yake, inalenga kuvunja familia ya Kiislamu na kufuta kitambulisho cha Kiislamu, na kusababisha kizazi kinachoiona Dini kama chaguo la kitamaduni la pembeni. Kwa hivyo, lazima tuwe waangalifu nao, kuimarisha jamii kwa ufahamu wa kifikra wa Kiislamu, na kuimarisha hadhi ya wanawake kama Uislamu ulivyowakusudia, wenye heshima na ulinzi, washirika katika kujenga familia na jamii, na msingi wa mwamko wa Ummah.

Template Design © Joomla Templates | GavickPro. All rights reserved.