- |
- Kuwa wa kwanza kutoa maoni!
- ukubwa wa font punguza ukubwa wa font zidisha ukubwa wa font
بسم الله الرحمن الرحيم
Jibu la Swali
Uturuki, Umbile la Kiyahudi, na Kambi nchini Syria
(Imetafsiriwa)
Swali:
Mnamo tarehe 14/4/2025, Shirika la habari la ‘Turk Press’ lilichapisha kwenye tovuti yake sababu za pingamizi ya umbile la Kiyahudi ya kuanzishwa kwa kambi ya anga ya Uturuki katika Uwanja wa Ndege wa T4 ndani ya ardhi ya Syria. Lilisema kuwa miongoni mwa sababu hizo ni “sababu ya kijeshi kwamba uwepo wa Uturuki ungezuia uhuru wa matembezi wa Jeshi la Wanahewa la 'Israel' juu ya Syria na kulazimisha uratibu wa usalama ambao Tel Aviv haiutaki kwa sasa.” Jarida la ‘Wall Street Journal’ lilichapisha kwenye tovuti yake tarehe 12/4/2025, kwamba Trump alionyesha nia yake ya kupatanisha wakati wa mkutano wake na Netanyahu wiki iliyopita “akisisitizia imani yake katika uwezo wake wa kutatua tatizo hilo, maadamu tu una akili timamu, lazima uwe na busara.” Je, hii ina maana kwamba umbile la Kiyahudi linaweza kuizuia Uturuki kuwa na uwepo wa kijeshi nchini Syria, licha ya makubaliano ya Uturuki na Syria? Je, Marekani ina dori katika suala hili ambayo inaweza kufafanua nia ya Trump kufanya upatanishi?
Jibu:
Ili kufafanua jibu, hebu turudi nyuma na tuhakiki nukta zifuatazo:
Kwanza: Wakati wa ziara ya Netanyahu nchini Hungary, Trump alimwalika kuja Marekani. Ulikuwa mwaliko wa ajabu:
1- Netanyahu alikuwa katika ziara ya siku nne nchini Hungary, kuanzia tarehe 2 Aprili 2025. Hii ilikuwa ni ziara yake ya kwanza katika nchi ya Ulaya tangu Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) ilipotoa kibali cha kukamatwa kwake mwaka jana.
2- Katika hali isiyo ya kawaida, Rais Trump wa Marekani aliwasiliana na Netanyahu na Orbán (Waziri Mkuu wa Hungary) wakati wa mkutano wao huko Budapest, akitoa mwaliko kwa Netanyahu kuzuru Ikulu ya White House: "Trump alifichua, wakati wa mazungumzo yake na waandishi wa habari akiwa ameabiri Air Force One, kwamba alikuwa na maongezi ya simu na Netanyahu jana, Alhamisi, na kwamba walijadiliana masuala ya kisiasa ya kimataifa, akitaja kwamba Waziri Mkuu huyo wa ‘Israel’ huenda akazuru Marekani hivi karibuni. Afisa mmoja wa Israel alithibitisha kwa Axios kwamba Trump alitoa mwaliko rasmi kwa Netanyahu kuzuru Ikulu ya White House, lakini tarehe ya mkutano bado haijawekwa. (Axios; Cairo News, 4/4/2025).
3- Umbile la Kiyahudi lilishangazwa na mwaliko huu wa dharura, haswa baada ya Ikulu ya White House kukataa kufanya hivyo baada ya sikukuu za Kiyahudi: (Kuna wasiwasi katika afisi ya Waziri Mkuu wa 'Israel' Benjamin Netanyahu kuhusu msisitizo wa Ikulu ya White House wa kufanya mkutano kati ya Rais wa Marekani Donald Trump na Netanyahu kesho, Jumatatu, na sio baada ya sikukuu ya Passover ya Kiyahudi, katika kipindi cha wiki mbili, kama afisi ya Netanyahu ilivyotaka. Taarifa iliyotolewa jana na afisi ya Netanyahu ilisema kwamba “ataelekea Washington kufuatia mwaliko aliopokea kutoka kwa Rais wa Marekani, Donald Trump, watajadili suala la ushuru, juhudi za kuwaregesha mateka wetu, mahusiano kati ya ‘Israel’ na Uturuki, tishio la Iran na vita dhidi ya Mahakama ya Kimataifa ya Jinai.” Wasiwasi unazidi kuongezeka katika afisi ya Netanyahu kutokana na msisitizo wa White House wa kufanya mkutano kesho, na uwezekano kwamba Trump atamshangaza Netanyahu kwa mada moja au zaidi ambazo ‘Israel’ haikutarajia, kwa mujibu wa yale Chaneli 12 iliyoripoti leo, Jumapili.” (Arab 48, 6/4/2025).
4- Netanyahu aliondoka Hungary na kuelekea moja kwa moja Washington bila kuregea umbile hilo, katika ishara nyengine ya dharura!
Pili: Mpangilio huu wa haraka unaonyesha jambo la dharura. Kuchunguza mada zilizotangazwa za majadiliano ya mkutano wao kunaonyesha kwamba angalau suala moja lilikuwa motisha kuu ya mwaliko huu wa haraka, uwezekano mkubwa ni hali ya Syria, kwa sababu zifuatazo:
1- Tukichunguza matamshi ya Rais Trump wa Marekani kwa kikundi kidogo cha waandishi wa habari wakati wa mkutano wake na Netanyahu mnamo tarehe 7/4/2025, baada ya Ikulu ya White House kufutilia mbali mkutano na waandishi wa habari aliopangiwa kufanya baada ya mkutano na Netanyahu, tunagundua kuwa kauli zake kuhusiana na uwanja wa Syria na mahusiano na Uturuki zilikuwa chanya sana, kuhusiana na uhusiano wake na Rais wa Uturuki Erdoğan na mawasiliano yao. Alisema:
("Nilimpongeza Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan. 'Nilisema: "Hongera, umefanya jambo ambalo hakuna mtu aliyeweza kulifanya katika miaka 2,000. Umeichukua Syria.' Kwa majina tofauti, lakini kitu kimoja," ... uliichukua kupitia njia ya mawakala." Trump aliendelea: "Erdogan alisema, 'Hapana, hapana, hapa.’ Mimi sikuichukua Syria. Nilimwambia, ‘Ni wewe, lakini ni sawa, sio lazima ukubali.’ Akasema, ‘Sawa, labda nilifanya hivyo.’” Trump aliongeza: “Erdogan ni mtu imara, na ni mwerevu sana, na alifanya jambo ambalo hakuna mtu aliyeweza kulifanya… Inabidi ukubali ushindi wake.” Akizungumza na mgeni wake, Benjamin Netanyahu, Trump alisema: “Bibi, ikiwa una tatizo na Uturuki, nadhani ninaweza kulitatua.’ Tatizo lolote ulilonalo na Uturuki, nadhani naweza kulitatua. Namaanisha, mradi una akili timamu, inabidi uwe na busara. Ni lazima tuwe na busara.” (Axios; Turk Press, 8/4/2025). Trump amelitaka umbile la Kiyahudi kuwa na akili timamu katika mambo yanayohusiana na Uturuki nchini Syria.
2- Umbile la Kiyahudi halikuwa na chaguo ila kujisalimisha kwa ombi hili la Marekani: (Waziri Mkuu wa 'Israel' Benjamin Netanyahu alisisitiza kwamba Tel Aviv haitaruhusu Syria kutumika kama kambi ya mashambulizi dhidi yake, akibainisha kuwa uhusiano na Uturuki umekuwa wa kirafiki lakini hivi karibuni "umezorota." Alisema baada ya mkutano wake na Rais wa Marekani Donald Trump: "Tumekuwa na tumekuwa na mahusiano ya kijirani na Uturuki, ambayo yamezorota, na hatutaki kuiona Syria ikitumiwa na mtu yeyote, ikiwemo Uturuki, kama kambi ya mashambulizi nchini 'Israel'," Aliongeza: "Tulijadili jinsi tunavyoweza kuepuka mzozo huu kwa njia mbalimbali, na nadhani hatuwezi kuwa na mpatanishi bora zaidi kuliko rais wa Marekani kwa madhumuni haya." Al-Quds Al-Arabi, 8/4/2025)
3- Umbile la Kiyahudi lilianzisha mashambulizi makali ya anga kwenye viwanja vya ndege vya Syria. RT iliripoti mnamo tarehe 2/4/2025, kutoka kwa taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Syria: "Vikosi vya Israel vilianzisha mashambulizi ya anga katika maeneo matano tofauti nchini humo ndani ya dakika 30, na kusababisha karibu uharibifu kabisa wa Uwanja wa Ndege wa Kijeshi wa Hama na kujeruhiwa kwa makumi ya raia na wanajeshi." Wizara ya Mambo ya Nje ya Syria ilizingatia kwamba "ongezeko hili lisilo la msingi la mashambulizi ni jaribio la makusudi la kuivuruga Syria na kurefusha mateso ya watu wake." Viwanja vya ndege hivi vilivyo katikati mwa Syria, ndipo mahali ambapo Uturuki inapanga kuweka kambi kama sehemu ya makubaliano na serikali mpya ya Syria:
(Waziri wa mambo ya nje wa Israel aliituhumu Uturuki kwa kucheza "dori hasi" nchini Syria, na kumuonya waziri mkuu wa mpito wa Syria, Ahmed al-Sharaa, kwamba "atalipia gharama kubwa sana" ikiwa ataruhusu "majeshi adui" kuingia nchini mwake. Kwa sasa Ankara inajadili makubaliano ya pamoja ya ulinzi na serikali mpya ya al-Sharaa, na ripoti zimeibuka kwamba Uturuki iko katika mchakato wa kupeleka ndege na mifumo ya ulinzi wa anga katika kambi za Syria za T4 na Aleppo. Baadhi ya wachambuzi wamelinganisha mashambulizi makubwa ya anga ya Israel kwenye uwanja wa ndege wa Hama wiki hii na uvamizi mdogo uliolenga viunga vya T4, wakidadisi kuwa Uturuki huenda ikawa tayari imeshahamisha baadhi ya vifaa vyake huko. (BBC, 5/4/2025.) Taarifa za habari zilienea kuhusu kuuawa kwa wahandisi watatu wa Kituruki kwenye Uwanja wa Ndege wa Hama kutokana na shambulizi la mabomu la umbile la Kiyahudi. ( Duru za kijeshi za Syria zinafichua kuwa wahandisi watatu wa Uturuki waliuwawa katika mashambulizi ya mabomu ya ‘Israel’ ya Uwanja wa Ndege wa Kijeshi wa Hama Jumatano iliyopita, ikiashiria kuwa wahandisi hao walikuwa wakifanya kazi ya kufunga vifaa vya kiufundi katika Uwanja wa Ndege wa Hama, ikiwemo mifumo ya ulinzi wa anga ambayo Uturuki ilikuwa imeleta kwenye uwanja huo wa ndege. (Erem News, 4/4/2025).
4- Inaonekana kuwa Uturuki ilikasirishwa sana na umbile la Kiyahudi kutokana na uvamizi wake wa hivi majuzi, haswa katika viwanja vya ndege vya Syria, na ikawasiliana kwa haraka na Marekani ili kukomesha (mashambulizi ya) umbile la Kiyahudi nchini Syria, haswa kwa vile Uturuki inatekeleza misheni iliyokubaliwa na Marekani nchini Syria. Kwa hivyo, mwaliko wa haraka kutolewa kwa Waziri Mkuu wa umbile la Kiyahudi huko Washington, na Trump kumtaka kutatua matatizo na Uturuki kwa busara.
Tatu: Kinachoonyesha kuwa suala hili lilikuwa la dharura zaidi katika mkutano huo ni kauli nyengine nyingi zinazoonyesha hili:
1- Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki alisema, "Marekani inahitaji, kwa kusema, kuweka mipaka kwa Netanyahu na kuasisi muundo." (Shirika la Anadolu, 9/4/2025).
2- Mazungumzo ya moja kwa moja kati ya umbile la Kiyahudi na Uturuki yalitangazwa.
RTV ilimnukuu Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki mnamo tarehe 9/4/2025, akisema, "Hakan Fidan alisema katika taarifa zake kwamba ili kuzuia 'kutoelewana' nchini Syria, wanaanzisha 'mawasiliano ya moja kwa moja' na 'Israel'." Fidan alieleza kuwa 'Israel' imefafanua mkakati wa 'kutoacha chochote' kwa utawala mpya nchini Syria. Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki alisisitiza haja ya kukomesha uvamizi wa ‘Israel’ katika eneo la Syria na kuacha kulipua miundombinu yake. Alidokeza kuwa ukosefu wa utulivu katika nchi jirani ya Uturuki utaiathiri na kuidhuru, akionya kwamba Ankara 'haiwezi kukaa kimya kuhusu hili.' (Hatuna nia ya kuingia katika mapigano yoyote au makabiliano na nchi yoyote katika eneo, ikiwemo 'Israel'... Tunashirikiana na utawala mpya wa Syria katika uwanja wa usalama na katika kupambana na ugaidi).
3- Reuters iliripoti wiki iliyopita kwamba timu za jeshi la Uturuki zilikagua angalau kambi tatu za anga nchini Syria ili kupeleka vikosi vya Uturuki huko kama sehemu ya makubaliano yaliyopangwa ya ulinzi wa pande zote kabla ya 'Israel' kulenga maeneo hayo kwa mashambulizi ya anga. Fidan aliiambia CNN ya Kituruki mnamo siku ya Jumatano: "Huku tukifanya operesheni fulani nchini Syria, lazima kuwe na utaratibu wa kuzuia mzozo na 'Israel' ambayo ndege zake zinaruka katika eneo hilo, sawa na mifumo tuliyo nayo pamoja na Marekani na Urusi." (Al Arabiya, 10/4/2025).
4- Chanzo cha habari cha Syria kiliiambia “Independent Arabia” kwamba "hakika kuna mazungumzo ya makubaliano. Makubaliano haya ni makubaliano yasiyo ya mzozo, sio makubaliano ya kutengana, kwa sababu hakuna mgongano kati ya Uturuki na 'Israel' nchini Syria. Kwa maana nyengine, makubaliano hayo ni kuchora mipaka ili iwapo kuna ndege ya 'Israel' katika anga ya Syria, mahali inapokwenda inaripotiwa."
(Independent Arabia, 9/4/2025) Yaani, sawia na makubaliano ya awali ya Uturuki na Urusi ya kuzuia mgongano baina yao nchini Syria!
5- Haya yote yanadhihirika kutokana na kauli zilizotolewa na maafisa wa Uturuki, kama ilivyoripotiwa na Asharq Al-Awsat mnamo tarehe 13/4/2025:
[Uturuki ilithibitisha kwamba itaendelea na mazungumzo yake ya kiufundi na 'Israel' ili kufikia utaratibu wa kupunguza kasi ya mzozo, kuweka sheria za ushiriki, na kuzuia kutokea kwa matukio au mapigano katika ardhi ya Syria. Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki alisema kuwa nchi yake inataka kupata utulivu nchini Syria na kuepuka chokochoko zozote, na inajitahidi kuepuka kuingia katika mzozo wowote na nchi yoyote ndani ya Syria. Wajumbe wawili (Waturuki na Waisraeli) walifanya mkutano huko Baku, mji mkuu wa Azerbaijan, Jumatano iliyopita, kwa ajili ya mazungumzo yaliyolenga kuepusha matukio au mapigano nchini Syria, baada ya uhasama kuzidi katika wiki mbili zilizopita.] (Asharq Al-Awsat 13/4/2025).
6- Al Jazeera iliripoti kwenye tovuti yake mnamo tarehe 14/4/2025, kulingana na ripoti ya mwandishi Andrea Muratore iliyochapishwa na tovuti ya Italia "Inside Over": kwamba Uturuki inacheza dori muhimu kwa utawala mpya wa Marekani kama daraja la kutatua masuala mengi tete katika Mashariki ya Kati na duniani kote, baada ya miaka mingi ya mvutano na utawala uliopita. Mwandishi huyo alisema katika ripoti yake kwamba Rais wa Marekani Donald Trump amethibitisha mara kwa mara kupendezwa na shakhsiya ya Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan na ustadi wake wa kisiasa, na tangu mwanzo wa muhula wake wa pili ametuma ishara za wazi za mapenzi zinazoonyesha nia yake ya kutaka msaada wake katika kutatua masuala kadhaa. (Al Jazeera 14/4/2025)
Haya yote yanaashiria kwamba Marekani inawachukulia maadui wa Kiyahudi na utawala wa Uturuki kama washirika, ikisimamia mambo baina yao ili kutumikia maslahi yake!
Nne: Inatia uchungu kwamba Marekani ndiyo inayosimamia mambo katika nchi zetu ipendavyo, ikitoa kipaumbele katika eneo hilo kwa umbile la Kiyahudi lililonyakua Ardhi Iliyobarikiwa - Palestina, ardhi ya Isra' na Mi'raj. Watawala wa nchi za Kiislamu wako kwenye mkondo na wito wa Marekani. Hata ardhi ya Khilafah, dola yake ya mwisho, Dola ya Uthmaniyya, ambayo Mayahudi walitaka kutia mguu wao ndani yake, katika Ardhi Iliyobarikiwa kwa badali ya kulipa mamilioni ya sarafu za dhahabu, walikanushwa vikali na Khalifa, ambaye alisema:
"Palestina si mali yangu, bali ni ya Umma wa Kiislamu. Watu wangu wamepambana kwa ajili ya ardhi hii na kuinywesheza kwa damu yao. Mayahudi na wabakie na mamilioni yao, na kama dola ya Khilafah itasambaratika, basi wanaweza kuichukua Palestina bila thamani." Na ndivyo ilivyotokea!
Uturuki, baada ya kuangamia kwa Khilafah Uthmani, inazuiwa na umbile la Kiyahudi kuasisi kambi ya kijeshi nchini Syria, hata baada ya utawala wa Syria kukubaliana nayo. Hii ndiyo hali ya Waislamu baada ya kuvunjika Khilafah. Na ni jambo baya sana!
Nguvu na utukufu wa Waislamu upo katika Khilafah yao, na Hizb ut Tahrir, kiongozi asiyewadanganya watu wake, inawataka watu wenye nguvu katika nchi za Kiislamu kuiunga mkono katika kuhuisha maisha kamili ya Kiislamu hapa duniani kwa kusimamisha tena Khilafah. Hapo izza ya Waislamu utaregeshwa.
[وَيَوْمَئِذٍ يَفْرَحُ الْمُؤْمِنُونَ * بِنَصْرِ اللهِ يَنْصُرُ مَنْ يَشَاءُ وَهُوَ الْعَزِيزُ الرَّحِيمُ]
“Na siku hiyo Waumini watafurahi * Kwa nusura ya Mwenyezi Mungu humnusuru amtakaye. Naye ndiye Mwenye nguvu Mwenye kurehemu.” [Ar-Rum: 4-5].