Logo
Chapisha ukurasa huu

بسم الله الرحمن الرحيم

Jibu la Swali

Mashambulizi ya Droni na Yanayojiri katika Vita nchini Sudan

(Imetafsiriwa)

Swali:

Siku za hivi karibuni zimeshuhudia maendeleo ya ajabu katika vita. Droni zilishambulia Port Sudan, mji mkuu wa utawala, kwa siku sita mfululizo, na kushambulia uwanja wa ndege wa kiraia, kambi ya anga, na maghala ya mafuta, na kusababisha mgogoro wa mafuta kote nchini. Droni pia zilishambulia mji wa Kassala kwenye mpaka wa Eritrea upande wa mashariki, pamoja na miji mingine. Haya yote yalisababisha vikosi vya jeshi kuondoka kuelekea upande wa El Fasher na kuzingatia kulinda Sudan mashariki, kama BBC ilivyoripoti mnamo tarehe 10/5/2025. Je, hii ina maana kwamba shambulizi la mashariki mwa Sudan linalenga kuliondoa jeshi kutoka Darfur, na kuiacha ikiwa chini ya udhibiti wa Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF) pekee? Je, matukio haya ni utangulizi wa Jukwaa la Jeddah (kongamano la mazungumzo)? Au kuna malengo mengine? Shukran.

Jibu:

Ili kufichua madhumuni ya mashambulizi ya droni kwenye shabaha muhimu mashariki mwa Sudan, tunafafanua yafuatayo:

Kwanza: Matukio yaliyotangulia mashambulizi makali dhidi ya Sudan mashariki, hasa katika mji wa Port Sudan:

1- Jeshi la Sudan lilipata mafanikio makubwa kwa kuvifukuza Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF) kutoka miji muhimu ya kati ya Khartoum, Bahri, na Omdurman. Ushindi huu mkubwa uliongeza ari ya jeshi la Sudan, ambalo lilianza kujiandaa kuviandama Vikosi vya Msaada wa Haraka huko Darfur. Hii iliongeza ari ya jeshi kuiandama RSF ambayo inachukuliwa kuwa kawaida baada ya mafanikio haya. Mwenendo huu huwalazimu viongozi kutabanni uhalisia mpya chini ya shinikizo la raia na shinikizo kutoka kwa maafisa wa ngazi za chini wa jeshi, yaani, wale ambao hawajui mienendo ya nje:

"Mwenyekiti wa Baraza la Utawala wa Sudan, Abdel Fattah al-Burhan, alithibitisha mnamo Alhamisi azma ya jeshi kukomboa nchi kutoka kwa "mamluki na vibaraka na kuondoa Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF)." (Anadolu Agency, 13/3/2025). Kauli hii ililenga kutabanni uhalisia mpya, na kutokana na athari kubwa uhalisia huu mpya uliokuwa nayo kwa watu na ndani ya jeshi, sekta za jeshi zimeanza kupambana na RSF katika baadhi ya maeneo ya Darfur. Vikosi vya Jeshi vimetetea kwa ushujaa nafasi zao. Mji wa El Fasher ndio pekee kati ya miji mikuu mitano ya Darfur ambayo imesalia chini ya udhibiti wa jeshi. Jeshi la Sudan limeanza kukimbilia Darfur.

"Matukio ya hivi punde yanaashiria kusonga mbele kwa vikosi vikubwa vya jeshi na vikosi vya pamoja kutoka mji wa kaskazini wa Ad-Dabba ili kuondoa mzingiro wa El Fasher, huku vikosi vyengine vinavyoshirikiana na vikundi hivyo vikikimbilia majimbo ya Kordofan na kupata ushindi mkubwa katika njia yao ya kuelekea mji huo kutoka mhimili mwingine." (Al-Quds Al-Arabi, 19/4/2025). Mwenendo huu, ambao watu wanausukuma baada ya ushindi wa Khartoum na ulio na mvuto mkubwa ndani ya jeshi, sio mtazamo wa Marekani. Kwa hiyo, Al-Burhan alijaribu kudhibiti mwelekeo huu. (Al-Burhan alionya dhidi ya kampeni za upotoshaji zinazokuza wazo kwamba vita vinalenga makabila maalum, akisisitiza kwamba "vita vyetu ni dhidi ya mtu anayebeba silaha dhidi ya serikali, sio dhidi ya kabila lolote," akizingatia kwamba uvumi huu unalenga "kuhamasisha watu na kuwaburuza katika mauaji." Alifafanua kuwa "uasi wa kiongozi wa kikabila haimaanishi kabila zima," (RT, 29/4/2025). Ilikuwa ni kana kwamba alitaka kusitisha haraka msafara wa jeshi kuelekea Darfur, kutokana na kwamba baadhi ya makabila ya huko yanaamini kwamba jeshi liko dhidi yao, kana kwamba anaomba kucheleweshwa.

2- Baada ya kushindwa vibaya na RSF katika eneo la kati na kupoteza sehemu zao kuu jijini Khartoum, Bahri na Omdurman, na pia kupoteza wapiganaji wao wengi na makamanda wa uwanja, waligubikwa na kushindwa na udhaifu. Kisha wakaelekea kwenye ngome yao huko Darfur, ambayo wengi wao waliidhibiti, na wakauzingira mji wa El Fasher. Jumuiko hilo la Vikosi vya Msaada wa Haraka lilikuwa kwa mujibu wa maagizo ya Marekani kwa Sudan. Ni jambo la kawaida, kutokana na mazingira, kwamba baadhi ya RSF wangetawanyika na kukabiliwa na ugumu wa kusajili kutoka kwa makabila ya tiifu, ikizingatiwa kwamba walikuwa wakipigana vita vya kushindwa dhidi ya mpinzani mwenye nguvu, jeshi la Sudan. Hii ina maana kwamba ari ya RSF ilikuwa chini. Kwa hiyo, vikosi vya jeshi mjini El Fasher vilitosha kurudisha nyuma mashambulizi yao ya mara kwa mara, ikimaanisha kwamba mashambulizi yao dhidi ya El Fasher hayakuwa na kasi. Kwa hiyo, jitihada kubwa zilihitajika kurejesha ari kwa majeshi ya Hemedti na kuonyesha ubora na nguvu zao, na uwezo wao wa kushambilia na kutishia maeneo ya mbali ambayo yalikuwa salama kwa jeshi la Sudan, kama vile Sudan ya Mashariki.

3- Licha ya utiifu wa watawala wao kwa Waingereza, Imarati (UAE) imeendelea kumuunga mkono kibaraka wa Marekani na kamanda wa Rapid Support Forces (RSF), Mohamed Hamdan Dagalo (Hemedti), kwa matumaini ya kupata ushawishi juu yake na wafuasi wake. Kitendo hiki ni sawa na kile inachokifanya nchini Libya kwa kumuunga mkono kibaraka wa Amerika, Haftar. Sudan imerudia kueleza kutoidhinishwa kwake na UAE na kuituhumu kwa kutoa msaada mkubwa wa kijeshi kwa RSF. Katika kujibu tuhma hizo, UAE ilifunga ubalozi wake nchini Sudan na haikuuhamishia mjini Port Sudan, kama nchi nyingine zilivyofanya baada ya kuzuka kwa vita jijini Khartoum mnamo Aprili 2023. Hata hivyo, Sudan iliendelea kudumisha ubalozi wake nchini UAE. Kwa kuzingatia hasira hii na kuzidi kwake, Sudan ilifungua kesi dhidi ya UAE katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki, ikiituhumu kushiriki katika mauaji ya halaiki yaliyotekelezwa na RSF nchini Sudan. Hata hivyo, mahakama hiyo ilikataa ombi hili la Sudan:

"Mahakama mnamo siku ya Jumatatu ilisema haiwezi kuhukumu kesi dhidi ya UAE, ilikataa ombi la Sudan la hatua za dharura na kuamuru kesi hiyo kuondolewa katika orodha yake." (Reuters, 6/5/2025). Kisha Sudan ilichukua hatua nyingine kali dhidi ya UAE, kukata mahusiano ya kidiplomasia na UAE na na kuondoa ubalozi wa Sudan. Kisha, matukio yanayohusiana na UAE yaliendelea. "Jeshi la Sudan lilitangaza mnamo siku ya Jumapili kuangamizwa kwa ndege ya mizigo ya Imarati iliyokuwa imebeba vifaa vya kijeshi kwa Vikosi vya Msaada wa Haraka... Ilisema kuwa ndege hiyo ilikuwa imebeba vifaa vya kijeshi, ikiwa ni pamoja na droni za kujiua na droni za kimkakati." (Sudan Tribune, 4/5/2025).

Pili: Madhumuni ya maendeleo haya na matokeo yake:

1- Kutokana na kuongezeka kwa mapigano jijini Khartoum tangu 2023, Baraza la Utawala lililazimika kuhamishia mji mkuu kwa muda hadi mji wa Port  Sudan, ikizingatiwa kuwa ni eneo salama zaidi. Misheni za kidiplomasia za kigeni, mashirika ya kimataifa ya kutoa misaada, na wakaazi wengi waliokimbia eneo la kati kwa ajili ya usalama walihamishiwa na wanachama wa Baraza Kuu, na kuwa wakimbizi. Eneo hili linawakilisha uhai kwa Sudan wakati wa vita – kwani liko na bandari inayoleta bidhaa kutoka nje ya nchi na uwanja wa ndege pekee wa kimataifa unaofanya kazi nchini humo, huku uwanja wa ndege wa Khartoum ukiwa bado umefungwa licha ya kuwa chini ya udhibiti wa jeshi. Kama mshipa muhimu wa uhai na makao ya serikali ya mpito, mashambulizi ya mfululizo ya droni kwa siku kadhaa yalikuja kama mshtuko mkubwa kwa umma wa Sudan na jeshi. Mashambulizi haya yanaonyesha kuwa RSF sio nguvu ambayo imevunjwa, kama wengine walivyofikiria, lakini wana uwezo mkubwa zaidi kuliko walivyoonyesha hapo awali. Pia zinaonyesha kwamba jeshi halipaswi kutawanyika katika majangwa ya Darfur, lakini linapaswa kuimarisha na kulinda huduma hizi muhimu, kama vile bandari, uwanja wa ndege na maghala ya mafuta. Zaidi ya hayo, moto mkali uliozuka katika maghala ya mafuta unapendekeza kwa jeshi kwamba huduma zake za kilojistiki, muhimu kwa vita huko Darfur, zimeharibiwa, kwa hivyo ni lazima kuchukua muda wake na kuzirekebisha kabla ya kukimbilia Darfur.

2- Mashambulizi hayo kwenye vituo vya Port Sudan, Uwanja wa Ndege wa Kassala, na kituo cha Wanamaji cha Flamingo yalifanywa na droni za China, kulingana na uchambuzi kutoka kwa vyanzo kadhaa, ikiwemo BBC, tarehe 10/5/2025. Droni moja inaweza kubeba kilo 40, huku nyengine inaweza kubeba kilo 200 za vilipuzi na makombora ya kuongozwa. RSF haijawahi kutumia droni kama hizo hapo awali. Droni mithili ya hizo zimeonekana kwenye Uwanja wa Ndege wa Nyala, ambao unadhibitiwa na Vikosi vya Msaada wa Haraka. Huu ndio uwanja wa ndege ule ule ambapo jeshi lilisema liliangamiza ndege ya mizigo ya Imarati.

3- UAE ilikuwa miongoni mwa nchi za kwanza katika eneo hilo kupata droni za China miaka iliyopita. Mnamo tarehe 2/5/2019, Habari za Ulinzi ziliripoti kwamba UAE ilitumia droni hizi kumuunga mkono Khalifa Haftar katika mashambulizi yake jijini Tripoli, Libya. Shirka la ‘Times Aerospace’ iliripoti kwamba UAE ilitumia droni hizi za Kichina kushambulia maeneo ya wanajihad nchini Iraq na Afghanistan mwaka 2014. Hii ina maana kwamba UAE imekuwa na silaha za aina mbalimbali nzito za droni za Kichina kwa miaka mingi, na kuna uwezekano kwamba wao wako nyuma ya mashambulizi haya mashariki mwa Sudan, ama moja kwa moja kutoka baharini au kwa kuzipatia RSF. Wamekasirishwa na kukashifu kwa serikali ya Burhan Mahakama ya Kimataifa, kukata mahusiano nao, na kuangamizwa kwa ndege yao ya mizigo.

4- Angazo la mashambulizi hayo lilikuwa kwenye viwanja vya ndege, bandari, na kambi ya wanamaji ya Flamingo. Moto mara nyingi ulizuka, na kuchukua masiku kuudhibiti, ikionyesha kuwa maghala ya mafuta yalikuwa yakilengwa. Waziri wa Nishati na Petroli wa Sudan, Muhieddin Mohamed Naeem, alifichua kuwa bohari tano kuu za kuhifadhi mafuta ziliteketezwa kutokana na mashambulizi ya droni katika siku ya kwanza ya kampeni (Sauti ya Sudan, 6/5/2025). Kutokana na kuendelea kulenga vituo vya nishati, waziri huyo alitoa maagizo ya kufungwa kwa bomba la kubeba mafuta ya Sudan Kusini kutokana na ulipuaji wa droni katika kituo cha kusukuma mafuta mashariki mwa Atbara (Al Jazeera Net, 11/5/2025).

5- Ulengaji huu ulilenga mafuta, ili kulinyima mafuta jeshi la Sudan, jambo ambalo lingezuia kuanzisha operesheni kubwa huko Darfur, haswa katika mji wa El Fasher. Hii ni pamoja na kuionyesha serikali katika nafasi dhaifu, kwani haiwezi kulinda makao yake makuu, pamoja na kupata mafuta na umeme kwa mahitaji yote ya Sudan. "Kampuni ya Umeme ya Sudan ilitangaza kwamba "kituo cha umeme cha Sudan kiliharibiwa kwa sababu ya kulengwa na droni na kukatika kwa umeme." (Anadolu Agency, 8/5/2025)

6- Ni wazi kutokana na hayo yote kwamba mashambulizi makubwa ya mashariki mwa Sudan hususan kwenye vituo vya kimkakati vya mji wa Port Sudan yanahusishwa na vita vya Darfur. Wanalenga kulazimisha jeshi kuondoka kushambulia El Fasher na kuelekea mashariki kutetea Port Sudan. BBC iliripoti mnamo tarehe 10/5/2025, kwamba vikosi vya jeshi vilivyokuwa vinaelekea El Fasher vililazimishwa na shambulizi la mashariki mwa Sudan kuregea na kuangazia kulinda Sudan mashariki.

Tatu: Hitimisho la Matukio haya

1- Inaelekea kwamba, baada ya mashambulizi hayo mazito, jeshi la Sudan limeanza kuhofia uwezo mpya wa Vikosi vya Msaada wa Haraka na kupoteza uwezo wa kupata mafuta yanayohitajika kuendesha magari yake katika vita walivyopanga El Fasher na Darfur kwa jumla. Hii ni pamoja na haja ya kuimarishwa kwa Sudan mashariki kwa hofu ya mawimbi zaidi ya mashambulizi, na hivyo kupunguza shinikizo la jeshi kwa Darfur na wasiwasi wake na eneo la mashariki.

2- Kuhusiana na RSF, vikosi vyake vitashika kasi na kuwa katika ari bora ya kufikia matokeo huko El Fasher, yote yakiwa na msaada kutoka UAE na utoaji wa droni nzito za China.

3- Inatarajiwa kuwa mashambulizi dhidi ya El Fasher yataongezeka na kwamba sekta za jeshi zilizokuwa zikielekea kumuunga mkono El Fasher zitarudi nyuma, na kwamba Baraza Kuu litachukua muda kurekebisha uharibifu huu mashariki mwa Sudan. Haiwezekani kwamba mazungumzo ya Jeddah yataanza tena kabla ya RSF kuchukua udhibiti wa El Fasher, au kuwa na uzito ndani yake, ambayo ni muhimu katika Darfur. Kisha Amerika itaunda usawa wa nguvu na udhibiti kati ya vikosi viwili vya Sudan (jeshi na Vikosi vya Msaada wa Haraka), ili kwamba ikiwa mazungumzo ya Jeddah yataanza tena, RSF itakuwa imetupilia mbali vazi la kushindwa na itasimama kwa ujasiri katika nguvu zao na uthabiti wa udhibiti wao na kuwa wameanzisha serikali ya kweli huko Darfur, yaani, kuunda hali zinayofaa kwa mgawanyiko kuwa tayari na kuwa uhalisia ambao lazima ukubaliwe.

Nne: Inatia uchungu kwamba mkoloni kafiri Marekani inaweza kusimamia vita vinavyotoa uhai nchini Sudan na kuwatumia vibaraka wake kuvitekeleza kwa uwazi, si kwa siri, na hadharani, bila kufichwa. Burhan na Hemedti wanapigana na damu ya watu wa Sudan bila sababu yoyote isipokuwa kutumikia maslahi ya Amerika, kwani inataka kurudia mgawanyiko wa Sudan kama ilivyokuwa katika kutenganisha kusini na Sudan. Sasa inafanya kila iwezalo kutenganisha Darfur na mabaki ya Sudan. Kwa hivyo, jeshi linaelekeza umakini wake katika maeneo mengine ya Sudan, na RSF inaelekeza umakini wao katika Darfur. Iwapo watu wenye ikhlasi ndani ya jeshi watajishughulisha katika kuregesha udhibiti wa Darfur, RSF itahamishia vita katika maeneo mengine nchini Sudan ili kulivuruga jeshi, hivyo basi vikosi vyake vitaondoka Darfur hadi mashariki mwa Sudan, ambapo RSF inazidisha mashambulizi yao kwa kutumia droni. Hii ni kuwezesha RSF kuchukua udhibiti kamili wa Darfur!

Kwa kumalizia, tunakuombeni kwa namna ile ile kama tulivyokuombeni katika jibu letu la awali la tarehe 19/12/2023:

Enyi watu wetu nchini Sudan ya Uislamu Mtukufu... Sudan ya Msikiti wa Dongola, msikiti wa kwanza kujengwa na Waislamu wa kwanza Sudan... Sudan ya ushindi mkubwa wa Kiislamu katika zama za Khalifa Othman, Mwenyezi Mungu amuwie radhi, ambapo alimuamuru gavana wa Misri kuleta nuru ya Uislamu Sudan, hivyo akawatuma askari wa Uislamu wakiongozwa na Abdullah Ibn Abi Al-Sarh, na kufunguliwa kwake kukatokea mwaka wa 31 H. Na kwa hivyo, Uislamu ukaenea kwa kasi, kwa upendeleo wa Mwenyezi Mungu, mpaka ukaijaza Sudan yote: kutoka kaskazini hadi kusini yake na kutoka mashariki hadi magharibi yake ... Kisha ukaendelea wakati wa zama za makhalifa wa Waislamu.

Enyi watu wetu wa Sudan, mliopigana dhidi ya Waingereza kuanzia 1896 hadi katikati ya Vita vya Kwanza vya Dunia mwaka 1916, wakati shujaa mchamungu na hodari, Ali bin Dinar, Wali (gavana) wa Darfur, alipouawa shahidi. Mwanachuoni huyo na mpiganaji huyo alisifika kwa kufanya ukarabati Miqat ya Madina na watu wa Ash-Sham, Dhu al-Hulaifah, na kujenga visima vya kunyweshea maji mahujaji, ambavyo bado vinaitwa kwa jina lake hadi leo, Abyar Ali.

Enyi watu wetu wa Sudan, tunawaomba murekebishe hali kabla ya majuto, kwa maana hakuna wakati wa kujuta. Chukueni udhibiti wa pande mbili zinazopigana na muwaunge mkono kwa uthabiti kwenye njia sahihi. Inusuruni Hizb ut Tahrir katika kusimamisha Khilafah Rashida, kwani ndani yake umo utukufu wa Uislamu na Waislamu na udhalili wa ukafiri na makafiri. Na radhi za Mwenyezi Mungu ni kubwa zaidi.

[إِنَّ فِي ذَلِكَ لَذِكْرَى لِمَنْ كَانَ لَهُ قَلْبٌ أَوْ أَلْقَى السَّمْعَ وَهُوَ شَهِيدٌ]

“Hakika katika hayo upo ukumbusho kwa mwenye moyo au akatega sikio naye yupo anashuhudia.” [Qaf: 37]

23 Dhul Qi’dah 1446 H

21 Mei 2025 M

Template Design © Joomla Templates | GavickPro. All rights reserved.