- |
- Kuwa wa kwanza kutoa maoni!
- ukubwa wa font punguza ukubwa wa font zidisha ukubwa wa font
بسم الله الرحمن الرحيم
Jibu la Swali
Matukio nchini Syria na Kurudi Nyuma kwa Vikosi vya Kidemokrasia vya Syria
(Imetafsiriwa)
Swali:
Matukio yanatokea kwa kasi kubwa kaskazini mashariki mwa Syria, na Vikosi vya Kidemokrasia vya Syria (SDF) vinapoteza udhibiti wa maeneo hayo kwa kasi kubwa, huku serikali ya Syria ikiyachukua. Yote haya yalitokeaje? Hili linapaswa kuelewekaje ikizingatiwa kwamba serikali na SDF ni vibaraka wa Amerika? Na licha ya idhini ya Marekani kwa serikali ya Syria kuwa wazi kama mwanga wa mchana katika kuteka maeneo hayo, utawala wa Trump unapanga nini nchini Syria au viunga vyake?
Jibu:
Ili jibu la maswali ya hapo juu liwe wazi, tunawasilisha mambo yafuatayo:
Kwanza: Hatua za usaidizi wa Amerika kwa SDF nchini Syria
1. Vikosi vya Kidemokrasia vya Syria (SDF au QASAD) ni muungano mpana ulioanzishwa Oktoba 2015 kwa lengo la kupambana na shirika la Dola ya Kiislamu (ISIS/ISIL/DAESH). Vinajumuisha wapiganaji wa Kikurdi, Waarabu, Wasyria, Waarmenia, na Waturuki. Sehemu kubwa zaidi ya SDF ni Vitengo vya Ulinzi wa Watu (YPG) na Vitengo vya Ulinzi wa Wanawake (YPJ), ambavyo vina jukumu la usalama na ulinzi wa ardhi za majimbo yenye kujitawala wenyewe yaliyotangazwa huko Rojava. (Wikipedia). Amerika iliongeza uungaji mkono wake kwa Vikosi vya Kidemokrasia vya Syria tangu kuanzishwa kwao mwaka wa 2015 na tangu uingiliaji kati wa Marekani nchini Syria mwaka wa 2014, ambao ulitangulia uingiliaji kati wa Urusi. Vikosi vya Marekani viliipa SDF ulinzi wa angani na kuwapa usaidizi wa kifedha na silaha. Kujitolea kwa Amerika kwao kulifikia hatua ambayo iliwaua mamia ya vikosi vya Wagner vya Urusi vilivyokuwa vikijaribu kuvuka Furat kuelekea mashariki mnamo Februari 2018. Amerika ilipinga taarifa na juhudi zote za Uturuki zilizolenga kudhoofisha SDF.
Hivyo, uungaji mkono wa Marekani kwa SDF uliendelea tangu kuanzishwa kwake, ukitoa ulinzi wa anga za kijeshi pamoja na ulinzi wa kisiasa, pamoja na usaidizi wa kifedha na silaha, na kuwezesha udhibiti wake juu ya ardhi yenye rutuba karibu na Furat, viwanja vya mafuta na gesi, na vituo vya umeme. Amerika pia ilipinga upinzani wa Uturuki kwa sera hii ya Marekani kaskazini mashariki mwa Syria. Yote haya yalikuwa sehemu ya maandalizi ya Amerika ya zana za kupigana na Uislamu iwapo Khilafah ya Kiislamu (Khilafah) itazinduliwa kutoka Damasko.
2. Leo, Trump ameona kwamba serikali ya Ahmed al-Sharaa ina uwezo zaidi wa kufikia maslahi ya Amerika katika eneo hili, jambo la kwanza miongoni mwa mambo mawili: kuweka mfumo wa utawala katika Uislamu mbali na Syria, na kujisalimisha kwa matakwa ya umbile la Kiyahudi nchini Syria na Palestina, ili umbile hili lisipingwe hata linaposhambulia mchana na usiku! Kwa hivyo, misimamo ya Trump, ikifuatiwa na ile ya mawaziri wake, kuhusu mwisho wa dori ya SDF na serikali ya Syria inayochukua nafasi yake katika kutumikia maslahi ya Amerika katika eneo hilo, imedhihirika. Hili halifichiki tena, bali limetangazwa waziwazi mchana na usiku na mjumbe wa Marekani nchini Syria, Tom Barrack, wakati wa ziara zake, na pia katika kauli za marais wa Uturuki na Syria.
a. Tom Barrack alisema: “Dori ya Vikosi vya Kidemokrasia vya Syria (SDF) kama “kikosi kikuu cha kupambana na ISIS ardhini” “imekwisha muda wake kwa kiasi kikubwa” kwani serikali ya Syria iko tayari kuchukua majukumu ya usalama,” (Al-Jazeera Net, 21/1/2026). Katika taarifa nyengine kwenye jukwaa la X, Barrack alisema: “Hali ya Syria “kimsingi” imebadilika, huku Damascus ikijiunga na Muungano wa Kimataifa wa Kuishinda ISIS kama mwanachama wake wa 90 mwishoni mwa 2025. Syria sasa “iko tayari na iko katika nafasi ya kuchukua majukumu ya usalama” ikiwa ni pamoja na udhibiti wa vituo na kambi za uzuizi za ISIL (ISIS), (Aljazeera; BBC, 20/1/2026).
Pia alisema katika chapisho refu kwenye ukurasa wake wa X, lililotafsiriwa na Ubalozi wa Marekani nchini Syria:
“Leo, hali imebadilika kimsingi. Syria sasa ina serikali kuu inayotambulika ambayo imejiunga na Muungano wa Kimataifa wa Kuishinda ISIS (kama mwanachama wake wa 90 mwishoni mwa 2025), ikiashiria mwelekeo wa magharibi na ushirikiano na Marekani katika kupambana na ugaidi. Hii inabadilisha mantiki ya ushirikiano wa Marekani na SDF: madhumuni ya asili ya SDF kama kikosi kikuu cha kupambana na ISIS ardhini yamekwisha muda wake kwa kiasi kikubwa, kwani Damascus sasa iko tayari na iko katika nafasi ya kuchukua majukumu ya usalama, ikiwa ni pamoja na udhibiti wa vituo na kambi za uzuizi za ISIS.” (X; CNN Arabic, 21/1/2026).
b. Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdoğan alisema mnamo Jumatano kwamba vikosi vya Wakurdi kaskazini mwa Syria lazima viweke chini silaha zao na kuvunja mara moja safu zao ili kufikia suluhisho bila umwagaji damu zaidi, baada ya Damascus kuwapa makataa ya siku nne ya kuwasilisha mpango wa kuijumuisha al-Hasakah katika jimbo kuu. (Al-Jazeera Net, 21/1/2026).
c. Afisi ya rais wa Syria ilitangaza katika taarifa mnamo Jumatatu kwamba rais wa mpito wa Syria Ahmed al-Sharaa alifanya mazungumzo ya simu na Rais wa Marekani Donald Trump. Kulingana na taarifa iliyochapishwa na Shirika la Habari la Kiarabu la Syria (SANA), “...marais hao wawili walisisitiza umuhimu wa kuhifadhi umoja wa eneo la Syria na uhuru wake, na kuunga mkono juhudi zote zinazolenga kufikia utulivu. Pande zote mbili zilisisitiza hitaji la kuhakikisha haki na ulinzi wa Wakurdi ndani ya muundo wa dola ya Syria.” (SANA; CNN Arabic, 19/1/2026).
Pili: Kutokana na haya yote, inadhihirika kwamba Amerika inampa Rais wa Syria Ahmed al-Sharaa ruhusa ya kukomesha SDF. Amerika leo haifichi nia yake, wala haitumii juhudi zozote kutumia lugha ya kidiplomasia. Inatangaza waziwazi kwamba SDF, kama chombo cha Marekani cha kupambana na “ugaidi,” imekwisha, na kwamba Amerika sasa inataka kutegemea chombo kikubwa zaidi, yaani serikali ya Ahmed al-Sharaa. Zote ni zana za Marekani, na Amerika hubadilisha zana zake inapendavyo.
Yote haya, pamoja na yanayojiri uwanjani, yanaelekeza mambo mengi, ikiwa ni pamoja na yafuatayo:
1. Suala la kumbadilisha kibaraka mmoja kwa mwengine: Wakati wa mapinduzi ya ash-Sham, ambayo yaliichosha Amerika na kusababisha nywele za Obama kuwa na mvi, Amerika iliendelea kutafuta kibaraka mwenye nguvu anayeweza kutawala ili kuchukua nafasi ya kibaraka wake Bashar, ambaye Syria ilikuwa imeasi dhidi yake. Tulisema katika Jibu la Swali la tarehe 26/7/2025 kwamba hii inafafanua kwamba mpango wa Marekani nchini Syria “unajengwa juu ya msingi mkuu: kubadilisha kibaraka mmoja kwa mwengine. Kwa kusudi hilo, Uturuki ilipewa idhini ya kuvunja utawala wa Bashar na kujenga mpya mtiifu kwake.”
Uturuki na huduma zake za ujasusi ilichukua misheni hii ya Marekani na kumuandaa Ahmed al-Sharaa, ambaye hapo awali alijulikana kama al-Julani. Miezi kadhaa kabla ya mwisho wa utawala wa Biden, Amerika iliruhusu Uturuki kuongoza operesheni ya kuikabidhi Syria kwa kibaraka mpya wa Marekani, Ahmed al-Sharaa. Uturuki, kwa niaba ya Amerika, iliwasiliana na Iran na Urusi na kuzima vikosi vyao nchini Syria. Amerika ilimwomba Bashar al-Assad kuikabidhi nchi hiyo, na hivyo ikawa. Kibaraka mpya aliwekwa badali ya yule wa zamani, na Uturuki ilibaki kuwa njia kuu ya mawasiliano ya Amerika naye.
2. Amerika ilianza kudai kwamba kibaraka wake mpya anatekeleza “vitendo vilivyokatazwa” zaidi, na akaanza kuthibitisha utiifu wake chini ya shinikizo la Uturuki. Aliitelekeza rayah (bendera) iliyokuwa na “Tawhid” na akaibadilisha kwa bendera ya kisekula, akatoa msamaha kwa mabaki ya Bashar, huku akiendelea kuwafunga Mashababu vijana wa Khilafah ambao wanafanya kazi ya kutangaza bishara njema ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) baada ya utawala huu dhalimu ambao tunaishi chini yake:
«...ثُمَّ تَكُونُ مُلْكاً جَبْرِيَّةً فَتَكُونُ مَا شَاءَ اللهُ أَنْ تَكُونَ، ثُمَّ يَرْفَعُهَا إِذَا شَاءَ أَنْ يَرْفَعَهَا، ثُمَّ تَكُونُ خِلَافَةً عَلَى مِنْهَاجِ النُّبُوَّةِ. ثُمَّ سَكَتَ»
“...Kisha kutakuwa na ufalme wa kidhalimu, na utabaki kwa muda wote ambao Mwenyezi Mungu anataka ubaki. Kisha atauondoa atakapotaka kuuondoa. Kisha itakuwepo Khilafah kwa njia ya Utume.” Kisha akakaa kimya.
Alipunguza mgao wa somo la Qur’an mashuleni, na Trump akataka asijibu mashambulizi ya mara kwa mara na makali ya umbile la Kiyahudi, ambayo hata yalifika Damascus yenyewe. Kisha Trump akata ajadiliane na umbile la Kiyahudi, na mazungumzo yalifanyika yakiongozwa na waziri wake wa mambo ya nje al-Shaybani bila aibu au uchamungu—si mbele ya Mwenyezi Mungu na Mtume wake wala mbele ya waumini, hasa watu wa Gaza. Matakwa ya serikali ya Ahmed al-Sharaa kutoka kwa umbile la Kiyahudi wakati wa mazungumzo haya yalikuwa madogo sana kiasi kwamba mhalifu Bashar alikuwa amejadiliana zaidi yake katika mazungumzo ya 2008 yaliyofadhiliwa na Uturuki kabla ya mapinduzi ya ash-Sham kuanza. Kwa kukubali “vitendo hivi vyote vilivyokatazwa,” Amerika ilifungua njia ya moja kwa moja ya kisiasa pamoja naye, pamoja na njia za ujasusi na njia za Uturuki. Njia ya kwanza ya kisiasa ilikuwa mkutano kati ya kibaraka wa Amerika Bin Salman (MBS) na al-Sharaa jijini Riyadh mnamo 14/5/2025. Njia hizi kisha zikapanuka, na al-Sharaa akapokea sifa kutoka kwa rais wa Amerika, ambaye baadaye alimpokea katika Ikulu ya White House mnamo 11/11/2025, ingawa kupitia mlango wa nyuma na bila sherehe rasmi. Trump alisema jioni hiyo kwamba “anakubaliana” na Rais wa Syria Ahmed al-Sharaa na akathibitisha kwamba Washington itafanya kila iwezalo kuifanya Syria ifanikiwe. (RT, 11/11/2025).
3. Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki Hakan Fidan alijadili katika Ikulu ya White House njia za kutatua matatizo yaliyopo nchini Syria sambamba na ziara ya Rais wa Syria Ahmed al-Sharaa jijini Washington na mkutano wake na Rais Trump. Fidan alitangaza kwamba majadiliano yalifanyika katika Ikulu ya White House na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Rubio, Mjumbe Maalum wa Rais wa Marekani Witkoff, Mjumbe wa Marekani nchini Syria Thomas Barrack, na Waziri wa Mambo ya Nje wa Syria As’ad al-Shaybani. Makamu wa Rais wa Marekani J.D. Vance baadaye alijiunga na mkutano huo. Washiriki walijadili njia zinazowezekana za kutoka katika matatizo ya sasa nchini Syria. (RT, 11/11/2025).
4. Katika kipindi hiki, Amerika ilikuwa ikiondoa vikwazo dhidi ya Syria hatua kwa hatua ili kuhakikisha katika kila hatua kwamba al-Sharaa anajidhihirisha kuwa kibaraka mtiifu wa Marekani. Kwa hivyo, Syria ilijiunga na muungano wa kimataifa kupambana na ISIS. Ubalozi wa Marekani jijini Damascus ulitangaza mnamo 11/11/2025 kwamba Syria ilikuwa imejiunga na muungano wa kimataifa kupambana na ISIS, na kuwa rasmi mwanachama wa 90. (Anadolu, 12/11/2025). Kisha Amerika iliondoa vikwazo dhidi ya Syria wakati Rais Donald Trump aliposaini kufutwa kwa Sheria ya Kaisari iliyowekwa nchini Syria tangu 2019. (Al-Jazeera, 19/12/2025).
Tatu: Wakati wa matukio ya sasa, vikosi vya SDF vilikuwa vikiondoka kutoka maeneo hayo, na kulingana na taarifa za kamanda wao Mazloum Abdi, kujiondoa huku kutoka magharibi mwa Furat kuelekea mashariki mwake kulitokana na ushauri wa “marafiki na wapatanishi” (tovuti ya Kurdistan 24, 16/1/2026). Na hakika Amerika inaongoza marafiki na wapatanishi hawa, ambao walikuwa wakishinikiza utekelezaji wa makubaliano ya SDF na serikali ya Syria mnamo 10/3/2025:
(“Rais wa Syria Ahmed al-Sharaa na kamanda wa Vikosi vya Kidemokrasia vya Syria Mazloum Abdi walitia saini mnamo Jumatatu makubaliano yanayoelezea ujumuishaji wa taasisi zote za kiraia na kijeshi zinazohusiana na utawala huru wa Kikurdi ndani ya muundo wa dola ya Syria, kwa mujibu wa kile afisi ya rais ulichotangaza...” (Al-Arabiya, 10/3/2025)).
Kisha serikali ya Syria ilitia saini makubaliano ya pili na SDF, ambapo SDF inajiondoa na kukabidhi “mara moja” majimbo ya Deir ez-Zor na Raqqa. Mjumbe wa Marekani aliyakaribisha na kuyaona kuwa ni hatua muhimu ya mabadiliko, na kwamba Amerika inataka Syria iliyoungana: (Mjumbe wa Marekani jijini Damascus, Tom Barrack, aliona kwamba makubaliano ambayo kusainiwa kwake kulitangazwa na Rais wa Syria Ahmad al-Shara’ pamoja na kamanda wa Vikosi vya Kidemokrasia vya Syria Mazloum Abdi ni “hatua muhimu ya mabadiliko”. Barrack alisema katika chapisho kwenye jukwaa la X: “Makubaliano haya na kusitisha mapigano yanawakilisha hatua muhimu ya mabadiliko, ambapo wapinzani wa zamani wanakumbatia ushirikiano juu ya mgawanyiko,” Barrack alisifu makubaliano hayo, akisema yatasababisha “mazungumzo mapya na ushirikiano kuelekea Syria iliyoungana” (X: Runinga ya Al-Arabi, 18/1/2026).
Nne: Mirengo yenye msimamo mkali ndani ya SDF—hasa wale wanaoshirikiana na Chama cha Wafanyikazi cha Kurdistan (PKK)—walikuwa wakichelewesha utekelezaji kwa matumaini kwamba mwanya unaweza kuwafungukia katika sera ya Marekani. Walisisitiza kwamba ujumuishaji wa SDF katika jeshi uwe kama kambi moja badala ya kama watu binafsi. Al-Arabiya iliripoti mnamo 17/1/2026, ikinukuu mkutano wa Erbil, kwamba Kamanda wa SDF Mazloum Abdi alijaribu kuwashawishi Wamarekani kuruhusu ujumuishaji kama vitengo vitatu ndani ya jeshi la Syria. Hata hivyo, mwanya huu haukufunguka katika msimamo wa Marekani, si katika mkutano wa Erbil wala kabla yake. Serikali ya al-Sharaa kisha ilianza mashambulizi—yaani, kutekeleza makubaliano kwa nguvu—kuanzia kutoka vitongoji vya mji wa Aleppo. Kwa hivyo, SDF ililazimika kusaini makubaliano ya pili na serikali ambayo chini yake ingekabidhi “mara moja” majimbo ya Deir ez-Zor na Raqqa. Amerika iliidhinisha makubaliano haya. Kama tulivyosema hapo awali, SDF ilijaribu kuchelewesha utekelezaji kwa kila makubaliano, lakini kuingilia kati kwa makabila ya Kiarabu na mashambulizi yao dhidi ya SDF hakukuacha nafasi ya hilo, ingawa rais wa Syria alitoa wito kwa makabila hayo kutulia. Al-Sharaa alisema: “Tunashauri makabila yetu ya Kiarabu kutulia na kuruhusu nafasi ya utekelezaji wa masharti ya makubaliano.” Wanamgambo wa Kiarabu wamejiunga na jeshi katika mapigano yake na Vikosi vya Kidemokrasia vya Syria tangu Jumamosi (CNN Arabic, 19/1/2026).
Tano: Hivyo, matukio yaliongezeka kwa kasi:
1- Serikali ya Syria ilitangaza kwamba mchakato wa kuwajumuisha wapiganaji wa SDF ungefanywa kwa mtu mmoja mmoja na si kama kambi au kama vitengo vya kijeshi ndani ya jeshi na wizara ya mambo ya ndani. Serikali pia ilitangaza hakikisho kuhusu haki za “kitamaduni” za idadi ya watu na utoaji wa uraia. Kisha ikaanza kuchukua udhibiti wa maeneo katika majimbo ya Raqqa na Deir ez-Zor, ikaingia katika jimbo la al-Hasakah, na kupanua udhibiti wake juu yake, na kuiacha SDF bila nafasi ya mazungumzo isipokuwa kuhusu al-Hasakah. Wizara ya Ulinzi ya Syria ilitangaza mnamo Jumatatu jioni kusitisha mapigano kati ya vikosi vya Syria na SDF kuanzia saa 8 mchana (karibu saa moja kutoka wakati huo) kwa muda wa siku nne. Hii ilikuja kufuatia tangazo la afisi ya rais wa Syria la kufikia makubaliano ya pamoja kati ya serikali na SDF kuhusu masuala yanayohusiana na mustakabali wa jimbo la al-Hasakah (Al Jazeera Net, 20/1/2026). Mkataba huu uliipa SDF idadi ndogo tu ya hatua za kutuliza: Shirika la Habari la Kiarabu la Syria (SANA) liliripoti mnamo Jumanne, likinukuu afisi ya rais wa Syria, kwamba kamanda wa Vikosi vya Kidemokrasia vya Syria, Mazloum Abdi, angemteua mgombea kutoka SDF kwa wadhifa wa naibu waziri wa ulinzi, pamoja na kupendekeza mgombea wa wadhifa wa gavana wa al-Hasakah, majina ya uwakilishi bungeni, na orodha ya watu binafsi kwa ajili ya ajira ndani ya taasisi za serikali ya Syria (CNN Arabic, 20/1/2026). Afisi ya rais ilisema kwamba, iwapo makubaliano yatafanyika, “Vikosi vya Syria havitaingia katikati mwa miji ya al-Hasakah na al-Qamishli na vitabaki viungani mwao, huku ratiba na maelezo yanayohusiana na ujumuishaji wa amani wa jimbo la al-Hasakah, ikiwa ni pamoja na mji wa al-Qamishli, yakijadiliwa baadaye.” (BBC, 20/1/2026). Pande hizo mbili pia zilikubaliana kwamba vikosi vya serikali ya Syria havitaingia katika vijiji vya Kikurdi, huku usalama wao ukifanywa na vikosi vya usalama vya ndani kutoka kwa watu wa eneo hilo. (CNN Arabic, 20/1/2026).
2- Baada ya Amerika kuamua kuwahamisha wafungwa wa ISIS kutoka magereza ambayo yalikuwa chini ya udhibiti wa SDF hadi Iraq, SDF iliomba kutoka Amerika kuongezwa muda wa mwisho hadi kukamilika kwa uhamisho wa wafungwa, na hivi ndivyo ilivyotokea. Wizara ya Ulinzi ya Syria ilitangaza kuongezwa muda wa makataa wa kusitisha mapigano na Vikosi vya Kidemokrasia vya Syria (SDF) kwa siku 15 ili kuunga mkono operesheni ya Marekani ya kuwahamisha wafungwa wa ISIS/ISIL kutoka magerezani. Wizara ya Ulinzi ilifafanua katika akaunti yake kwenye jukwaa la X kwamba muda huo utaanza usiku wa leo saa kumi na moja saa za ndani, na kwamba hii inaunga mkono kuwaondoa wafungwa wa ISIS/ISIL katika magereza ya SDF na kuwahamisha hadi Iraq (Al Jazeera, 24/1/2026). Kwa hivyo, mchakato wa kufunga ukurasa wa SDF na ukurasa wa kamanda wake, kibaraka mdogo wa Amerika Mazloum Abdi, unaendelea baada ya kukamilisha kazi ya Marekani, na Amerika ikamaliza huduma zake kwa badali ya “mshahara mdogo wa kustaafu,” yaani uteuzi wa wafanyikazi hapa na pale – jambo ambalo linaweza kuwa la muda. Kwani anayesimamia matukio katika eneo hilo ni Amerika, na ikiwa maslahi yake yanahitaji mabadiliko ya misimamo, inawaamuru vibaraka wake miongoni mwa watawala kuyatekeleza bila kope zao kupepesa au hisia yoyote ya aibu kuwagusa. [أَلَا سَاءَ مَا يَحْكُمُونَ] “Tazama uovu wa wanavyohukumu!” [Al-Nahl:59]
Sita: Inauma kwamba Syria imekuwa mtiifu kikamilifu kwa Amerika baada ya kafara zote zilizotolewa na watu wake kubadilisha utawala na kusimamisha utawala wa Uislamu mahali pake. Amerika hununua utiifu duni ili kupata kiti kibovu ambacho mkaazi wake anaitumikia Amerika ili abaki ameketi na kudhibiti eneo lote la Syria. Anaachana na utukelezaji wa Uislamu na jihad kukomboa ardhi inayokaliwa kimabavu, anaiondoa Syria kutoka kwenye mstari wa mapambano na adui—jambo ambalo hata mhalifu mtoro Bashar al-Assad hakusubutu kufanya—na anasahau au kujifanya kusahau kwamba kujitupa mikononi mwa Amerika hakutahifadhi wadhifa wake endapo Amerika itapata kibaraka mwenye uwezo zaidi. Katika wale yaliokuwa kabla yake kuna mafunzo ya kutosha. Je, watawala, wasaidizi wao, na wapambe wao, vibaraka wa Amerika, hawatazingatia jinsi Amerika inavyowaangusha vibaraka wake, kujitosheleza na huduma zao, na kuwatelekeza baada ya ndoto zao kuzama, ikiwatupa bila majuto na bila kutoa chozi hata moja kwa ajili yao, baada ya kueneza ufisadi kote nchini kwa ajili ya kuitumikia Amerika—ila tu kisha kuwatupa kando ya barabara mara tu itakapomalizana na huduma zao kwa kupendelea kibaraka mpya mwenye uwezo zaidi wa kuitumikia kuliko yule aliyemtangulia? Na kweli kuhusu watawala hawa vibaraka ni kauli ya Mwenyezi Mungu Aliyetukuka:
[فَأَذَاقَهُمُ اللَّهُ الْخِزْيَ فِي الْحَيَاةِ الدُّنْيَا وَلَعَذَابُ الْآخِرَةِ أَكْبَرُ لَوْ كَانُوا يَعْلَمُونَ]
“Basi Mwenyezi Mungu akawaonjesha hizaya katika uhai wa duniani. Na bila ya shaka adhabu ya Akhera ni kubwa zaidi; laiti wangeli jua!” [Surah Az-Zumar 39:26].
8 Sha’ban 1447 H
27/1/2026 M