Afisi ya Habari
Wilayah Sudan
| H. 7 Rabi' II 1448 | Na: HTS 1448 / 40 |
| M. Jumamosi, 19 Septemba 2026 |
Taarifa ya Msemaji Rasmi wa Hizb ut Tahrir katika Wilaya ya Sudan kwenye Mkutano na Waandishi wa Habari yenye Kichwa:
Utawala Usio Halali na Sera Zilizofeli... Matokeo Yake: Njaa na Dhiki
(Imetafsiriwa)
Alhamdulillah Rabbil Alamin (Sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu, Mola wa walimwengu wote), na rehma na amani zimshukie yule aliyeletwa kuwa rehma kwa walimwengu—bwana wetu, mtume wetu, na kielelezo chetu—Muhammad bin Abdullah; rehma na baraka za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, familia yake, na maswahaba zake, pamoja na wale wote wanaofuata mwongozo wake na kufuata njia yake hadi Siku ya Kiyama.
Ndugu watukufu—waliopo hapa ukumbini na wale wanaofuatilia kupitia matangazo ya moja kwa moja—Assalamu Alaikum wa Rahmatullah wa Barakatahu.
Migogoro inazidi kurundikana: bei za juu mno zinatikisa masoko, na sarafu ya ndani inaporomoka dhidi ya sarafu za kigeni. Wakati huo huo, serikali yenyewe inasababisha mateso—kwa kuweka kodi nzito kwa wafanyibiashara na wengineo, kupandisha ushuru wa forodha kwa bidhaa zinazoingizwa nchini, na kuwasumbua wachuuzi ili kukusanya matozo—hadi pale maisha yalipogeuka kuwa mateso yasiyovumilika na hali kufikia ukingoni. Shughuli za kiuchumi zimesimama, lakini serikali inajifanya inajitahidi kushughulikia masuala hayo, ikielezea hali halisi kana kwamba haikuhusika hata kidogo katika kuisababisha. Waziri wa Fedha, Gibril Ibrahim, anawaambia waandishi wa habari kuwa kushuka kwa kasi kwa thamani ya pauni dhidi ya sarafu za kigeni kunatokana na mahitaji makubwa ya fedha za kigeni na kutokuwepo kwa uwiano ambapo bidhaa zinazoingizwa nchini ni nyingi kuliko zinazouzwa nje; anakiri kuwa kushuka huku kwa thamani ya sarafu kumeathiri moja kwa moja maisha ya watu, hasa wale wenye kipato kidogo. Kisha, Wizara ya Nishati na Petroli inapuuza hali halisi ambayo hata kipofu angeweza kuiona, ikisisitiza kuwa mafuta yanapatikana na kukataa kuwa foleni za magari katika vituo vya mafuta zinasababishwa na uhaba! Hata hivyo, kila mtu anashuhudia magari yakipanga foleni katika vituo vya mafuta kwa siku nyingi mfululizo; katika baadhi ya majimbo, wamiliki wa magari hulazimika hata kulala katika vituo hivyo.
Aidha, serikali ilipandisha kiwango cha kubadilisha fedha kwa ajili ya forodha mara nne mwaka huu—mara ya mwisho ikiwa tarehe 12 Septemba 2026—ikikirekebisha kutoka pauni 3,960 hadi 4,346. Kupanda huku kunaongeza shinikizo kwenye gharama za bidhaa zinazoingizwa nchini, na hivyo kupandisha bei moja kwa moja na kuwafanya watu walio katika mazingira magumu zaidi kubeba mzigo huo mzito.
Mwanzoni mwa mgogoro huu, vyombo vya habari vilivyolipwa vilijaribu kuonyesha kuwa ulafi wa wafanyibiashara ndio chanzo kikuu; hata hivyo, baadaye masoko yalianzisha migomo kupinga kodi hizo za juu mno—jambo lililoonyesha kuwa ulafi wa kweli ulikuwa upande wa serikali. Jumatano iliyopita, shughuli za masoko jijini Khartoum zilisimama kabisa kutokana na kushuka kwa thamani ya sarafu ya ndani kwa kiwango ambacho hakijawahi kushuhudiwa. Wafanyibiashara walilazimika kusitisha mauzo kwa kuhofia kutoweza kununua bidhaa mpya za kuuza; kiwango cha ubadilishaji fedha dhidi ya dolari ya Marekani kilipanda hadi pauni 8,800 za Sudan—kutoka pauni 7,200 mwanzoni mwa wiki—jambo lililosababisha kupanda kwa bei za bidhaa, hasa zile muhimu kama vile unga, sukari, na mafuta ya kupikia. Kwa mfano, ndani ya muda usiozidi mwezi mmoja, bei ya kilo moja ya sukari ilipanda kutoka pauni 5,000 hadi 10,000, unga kutoka 3,000 hadi 5,000, na mchele kutoka 8,000 hadi 14,000—huku bidhaa zengine zikishuhudia ongezeko kama hilo.
Wafanyibiashara katika Soko la Atbara katika Jimbo la Mto Nile walisimamisha shughuli zao kabisa mnamo tarehe 6 na 7 Septemba ili kupinga kodi na matozo makubwa waliowekewa na mamlaka za serikali. Wafanyibiashara wa Shendi walichukua hatua kama hiyo mnamo tarehe 9 Septemba, na migomo pamoja na kufungwa kwa masoko kulishuhudiwa pia katika majimbo ya Al-Qadharif na Sennar. Hali hiyo ya kufungwa kwa masoko ilienea hadi El Obeid katika jimbo la Kordofan Kaskazini; wakati huo huo, wafanyibiashara wa Kosti, Rabak, na Al-Duwaym (katika jimbo la White Nile) waligoma na kufunga maduka yao kupinga kodi na matozo yaliyowekwa na mamlaka za eneo hilo. Katika hali inayozidi kuwakandamiza maskini, mamlaka za manispaa katika miji mbalimbali zinaendesha kampeni ambazo kimsingi zinadaiwa kufanywa kwa ajili ya "kupanga mambo vizuri." Hata hivyo, lengo halisi ni kukusanya mapato au kusafisha eneo husika ili kuliuza kwa wanunuzi wenye uwezo mkubwa wa kifedha. Hili ndilo hasa lililotokea kwa soko la wanawake katika mji wa Kassala, mashariki mwa Sudan. Wiki iliyopita, mamlaka za eneo hilo zilibomoa soko hilo—lililojulikana kama "Souq al-Niswan"—ambalo lilikuwepo kwa miongo kadhaa; kuna uvumi kwamba eneo hilo limeuzwa kwa upande ambao haujatajwa.
Katika mazingira haya ya migogoro na majanga, programu za mabenki—hasa programu ya Bankak—zimekuwa zikifeli mara kwa mara, na kusababisha shughuli za ununuzi na uuzaji kusimama kabisa. Hali hii ilitokana na ukweli kwamba zaidi ya asilimia 90 ya fedha za wananchi ziliwekwa benki kwa lazima wakati wa mchakato wa kubadilisha sarafu. Hali ngumu wanayokabiliana nayo watu katika mazingira haya inafanana na ile ya yule paka aliyefungiwa na mwanamke ambaye hakumlisha wala kumruhusu kutafuta chakula ardhini—kitendo kilichomfanya mwanamke huyo kuhukumiwa kuingia Motoni, kulingana na Mtume (saw). Je, itakuwaje basi kwa wale wanaosababisha watu kufa kwa njaa?
Uhalisia huu mchungu unathibitisha ufisadi wa serikali hii katika utendaji wake na kutokuwa halali kwake kwa mujibu wa Sharia; kwani imejengwa juu ya mfumo wa kibepari, ambao huzalisha umaskini na kuua maskini. Hali hii chungu haitaondoka kwetu isipokuwa kwa kuregea kwenye mfumo uliowekwa na Mola wa Walimwengu—Khilafah Rashida kwa njia ya Utume—ambao hulinda mambo yetu na kutuhakikishia maisha ya heshima katika kumtii Mwenyezi Mungu.
Suluhisho msingi la mgogoro wa kiuchumi nchini Sudan—na kwa hakika, duniani kote—linategemea mambo yafuatayo:
Kwanza: Kusimamishwa kwa mfumo wa kiuchumi unaozingatia itikadi sahihi na wenye suluhisho la haki—jambo ambalo linaweza tu kutoka kwa Mtaalamu Mjuzi wa yote. Kwa hivyo, ni muhimu kutekeleza mfumo wa kiuchumi wa Kiislamu, ambao unahakikisha kukidhi kikamilifu mahitaji yote ya msingi—kama vile chakula, mavazi, na makazi—kwa kila mtu mmoja mmoja miongoni mwa raia. Mtume (saw) asema:
«مَنْ أَصْبَحَ مِنْكُمْ آمِناً فِي سِرْبِهِ، مُعَافًى فِي جَسَدِهِ، عِنْدَهُ قُوتُ يَوْمِهِ، فَكَأَنَّمَا حِيزَتْ لَهُ الدُّنْيَا»
“Yeyote miongoni mwenu anayeamka akiwa na usalama wa familia na afya njema, na akiwa na riziki ya siku yake, basi ni kama vile amemiliki dunia nzima.” na kuwawezesha kukidhi mahitaji yao ya ziada kwa kiwango kikubwa iwezekanavyo; Aidha, kupitia hukmu za Sharia, mfumo huu unakataza kuhodhi mali ili kuhakikisha haizunguki mikononi mwa matajiri pekee
﴿كَيْ لَا يَكُونَ دُولَةً بَيْنَ الْأَغْنِيَاءِ مِنْكُمْ﴾
"Ili isije ikawa mali inayozunguka miongoni mwa matajiri wenu pekee". Mbali na kuharamisha ukiritimba, kodi zisizo za moja kwa moja, na matozo mbalimbali—ili zisije zikasababisha kupanda kwa bei za bidhaa na huduma—Mtume (saw) asema:
«مَنْ دَخَلَ فِي شَيْءٍ مِنْ أَسْعَارِ الْمُسْلِمِينَ لِيُغَلِّيَهُ عَلَيْهِمْ كَانَ حَقّاً عَلَى اللَّهِ أَنْ يُقْعِدَهُ بِعُظْمٍ مِنَ النَّارِ يَوْمَ الْقِيَامَةِ»
"Yeyote anayeingilia bei za Waislamu kwa lengo la kuzipandisha, ni haki juu ya Mwenyezi Mungu kumkalisha juu ya kiti kikubwa cha Moto Siku ya Kiyama."
Pili: Sarafu inapaswa kuwa na dhamana ya dhahabu—kutokana na thamani yake ya asili—huku biashara zote za kimataifa (uagizaji na usafirishaji wa bidhaa) zikifanyika kwa msingi huo. Mbali na usalama na uthabiti wake, hukmu nyingi za Kiislamu zinajengwa juu yake, kama vile zile zinazohusu fidia ya damu (diyah), kiwango cha thamani kinachostahilisha kukatwa mkono wa mwizi, "Zaka" ya mali ya kifedha, na nyinginezo. Sudan ni nchi yenye utajiri wa dhahabu, jambo linalomaanisha kuwa haina haja ya mikopo yenye riba au aina nyinginezo za ukopaji wa namna hiyo.
Tatu: Kukata kabisa mafungamano na Mfuko wa Fedha wa Kimataifa (IMF), Benki ya Dunia, na taasisi nyingine za kifedha zinazotoa mikopo ya riba, na kutekeleza hukmu za Uislamu zinazohusiana na upataji, ukuzaji, na matumizi ya mali.
Nne: Serikali hairuhusiwi kupeana mali ya umma—kama vile dhahabu, mafuta ya petroli, na madini ambayo hayamaliziki—iwe kwa njia ya mauzo, zawadi, au njia nyinginezo. Badala yake, jukumu lake ni kuisimamia kwa manufaa ya Ummah mzima, kwani mali hizi ni mali za Ummah na lazima zitumike kwa ustawi wake.
Kwa ufupi, ni hukmu hizi—pamoja na sheria nyinginezo za Kiislamu—ndizo zinazohakikisha maisha yenye heshima kwa watu. Kwa hivyo, hakuna njia ya kuepuka hali hii ya kusikitisha kwa yeyote kati yetu isipokuwa kwa juhudi za dhati pamoja na wanachama wanyoofu wa Ummah—wale wanaojitahidi kuuregesha kama Khilafah Rashida kwa njia ya Utume, ambapo tunaweza kumridhisha Mola wetu (swt) na kuishi chini ya kivuli chake kwa heshima na utukufu.
Wassalamu alaikum wa Rahmatullah wa Barakatahu
Ibrahim Othman (Abu Khalil)
Msemaji Rasmi wa Hizb ut Tahrir
katika Wilayah Sudan
| Hizb-ut Tahrir: Afisi ya Habari Wilayah Sudan |
Address & Website Tel: 0912240143- 0912377707 http://www.hizb-sudan.org/ |
E-Mail: Spokman_sd@dbzmail.com |