Logo
Chapisha ukurasa huu

بسم الله الرحمن الرحيم

Kuna Kamba ya Uokozi kwa Sudan – Ichukueni!

(Imetafsiriwa)

Kwa zaidi ya miaka mia moja, ulimwengu umefanywa kuamini kuwa vita katika Ardhi za Waislamu, hususan nchi za Kiafrika, vinatokana na wao kutoendelea kifikra, kisiasa na kiuchumi. Zimewasilishwa kwa ulimwengu kuwa haziwezi kusimamia uwepo wao bila kile kinachoitwa msaada na uingiliaji kutoka kwa Magharibi.

Kwa hakika, uongo huo ulikuja kuwa kweli baada ya nchi za Magharibi kuanza kuzikoloni nchi za Kiafrika, ambapo walinyang’anya ardhi hizi utajiri wao, wakawanyang’anya ubinadamu wao, na sio tu kuwazuia fursa zote za maendeleo ya kweli bali hata kurudisha hali zao za maisha nyuma katika zama za kabla ya kalenda ya sasa. Waliua makabila na ustaarabu mzima, wakawafanya watumwa waliosalia, wakabeba maelfu ya watu wake hadi kwenye mabara ya mbali, na hata wakawaweka kwa akili ya maonyesho katika mbuga zao za wanyama, wakitumia maisha yao, heshima, tamaduni na sio rasilimali zao tu. Miaka mia chache baadaye, wakati utumwa ulipokuwa ghali sana kilinganishwa na uanzishaji wa viwanda, waliyapa maeneo haya uhuru bandia na mamlaka ya kujitawala yasiyokuwepo ndani ya mipaka bandia waliyochora yakiwa na mtawala na kuyavisha hadhi ya dola za kitaifa. Na ili kuhakikisha ufanisi wenye faida kwa “aina mpya ya viwanda” hivi, walitengeneza mtandao wa usalama wa sheria za kimataifa, makubaliano, mifumo ya ufadhili nk., ili wakati wowote umiliki wa viwanda hivyo unapoelekea kuhamisha mikono, au faida mpya zikipatikana, mkoloni na “Bwana Magharibi” wasio waaminifu huchukua tu mjeledi wake kuwadhibiti farasi wake. Mjeledi huo wenye nguvu umekuwa na bado ungali ni mifumo yao tawala fisidifu  ya utawala iliyolazimishwa, iliyotungwa na watawala vibaraka wao walio rahisi kuchukua nafasi, wakatili, wasio na roho, ambao hamu yao ndogo kabisa ni mafanikio na maendeleo ya watu wao wenyewe. Mkono wao mrefu juu ya vibaraka hao ulikuwa ni balozi zao, na mashirika ya kibinadamu, na yale yanayofanana na hayo, yaliyo tayari kuchochea uasi, mapinduzi na hata mauaji ya halaiki, yenye kuchochea ukabila, ubaguzi wa rangi, madhehebu – chochote na wakati wowote maslahi ya Magharibi yanaona kuwa inafaa. Haya yote na huku wakiulevya ulimwengu mzima – kumbuka, sio tu makoloni – kwa dawa ya usingizi na kupagawisha, iitwayo “demokrasia na usekula”.

Magharibi ya kibepari haijawahi kukumbuka thamani ya mwanadamu, kwa maana faida ya kifedha ndio nzuri zaidi katika mfumo wao. Kwa hivyo, ukoloni ndio njia ambayo mfumo wa kibepari unahakikisha uwepo wake, unajilinda na kujieneza kwa wengine. Kwa hivyo, kulazimisha udhibiti wa kijeshi, kisiasa, kiuchumi, kifikra na kithaqafa juu ya watu wengine ni muhimu ili kufikia malengo na matamanio yake. Jambo la msingi la miongo kadhaa ya ushawishi wa kikoloni ni kwamba kila moja ya serikali zao vibaraka katika ardhi zetu ziliingiza nchi zao katika taabu nyingine na machungu zaidi kwa ajili ya ushindani wa ulafi uliojaa matamanio ya siasa za Magharibi. Tumeshuhudia hilo tena na tena nchini Rwanda, Tunisia, Misri, Libya, Pakistan, Bangladesh, Uturuki, na nchi nyingine nyingi za Kiislamu. Na Sudan sio tofauti na hizo. Orodha ya kufeli kukubwa, kiuchumi, kielimu, kithaqafa na mengine mengi ya kimfumo ya tawala mtawalia za kisekula na kidemokrasia zinaweza kuendelezwa kwa kurasa nyingi.

Kwa hivyo, vita vya Sudan na ratiba nzima ya maafa ya kisiasa na kiuchumi ni matokeo ya ukoloni huu, ambapo mkoloni wa awali Uingereza ana zana zake ndani ya miundo ya kisiasa na pia katika harakati za silaha, kama vile mkoloni Marekani anazo zana zake ndani ya Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF) na wengineo. Kwa hivyo, vita hivi vinachochewa na ushindani wa udhibiti kwa wakoloni wawili nchini, kila mmoja akitaka kumfukuza mwenzake.

Tukizingatia Sudan leo, tunaona jinsi Jenerali Abdel Fattah al-Burhan, na Mohamed Hamdan Dagalo (“Hemedti”) wamepofushwa katika utiifu wao kwa nchi za Magharibi. Kiasi kwamba hawajali utakatifu wa damu ya Muislamu. Badala yake, wanashindana wao kwa wao kwa ukatili na udhalimu katika vita hivi vya kipuuzi, wakihamisha zaidi ya watu milioni 12 katika ardhi yao wenyewe, wakiwasukuma kwenye njaa na kiu, wakitumia mateso, mauaji, na hata ukatili wa kingono dhidi ya wanawake na wasichana.

Hivyo, ni nani atakayemaliza vita hivi vya wababe na kuokoa nchi hiyo na watu wake?

Ni lazima tukumbuke kwamba sisi ni Waislamu, na kwamba Mwenyezi Mungu (swt) ndiye mwenye uwezo mkubwa zaidi juu ya ulimwengu huu. Hivyo basi, hatua ya kwanza ni kumtegemea Mwenyezi Mungu tu na sio wakoloni hata kidogo, kwani Mwenyezi Mungu (swt) asema:

[وَلَن يَجْعَلَ اللَّهُ لِلْكَافِرِينَ عَلَى الْمُؤْمِنِينَ سَبِيلًا]

“wala Mwenyezi Mungu hatawapa makafiri njia ya kuwashinda Waumini.” [An-Nisa:141].

Kwa hiyo, suluhisho na tiba ya migogoro yote ya Sudan na ulimwengu mzima wa Kiislamu ni imani tukufu ya Uislamu, ambayo inatoka katika nyoyo za Waislamu. Uislamu ni itikadi na mfumo kamili wa maisha, Dini, na hiyo ndiyo inayounda dola iliyo huru na inayojitawala kikweli, na sio kiwanda cha utumwa kilichojengwa ndani ya mipaka ya Sykes-Picot ya wakoloni.

Wakoloni walichochea migawanyiko ya kimaeneo na kikabila, ugonjwa ambao unaweza kuponywa tu kupitia Uislamu na si vyenginevyo. Katika historia, Uislamu umekuwa ndio nguvu pekee iliyoweza kuwaunganisha watu mbalimbali kuwa Umma mmoja.

[وَأَلَّفَ بَيْنَ قُلُوبِهِمْ لَوْ أَنْفَقْتَ مَا فِي الْأَرْضِ جَمِيعاً مَا أَلَّفْتَ بَيْنَ قُلُوبِهِمْ وَلَكِنَّ اللَّهَ أَلَّفَ بَيْنَهُمْ إِنَّهُ عَزِيزٌ حَكِيمٌ]

“Na akaziunga nyoyo zao. Na lau wewe ungeli toa vyote viliomo duniani usingeli weza kuziunga nyoyo zao, lakini Mwenyezi Mungu ndiye aliye waunganisha. Hakika Yeye ndiye Mtukufu Mwenye nguvu na Mwenye hikima.” [Al-Anfal: 63].

Hii ni kwa sababu Uislamu si dini tu, bali ni Aqidah yenye mfumo mpana, kamili, usio na dosari, mfumo kamilifu wa maisha na sheria – hukmu za Sharia.

[الْيَوْمَ أَكْمَلْتُ لَكُمْ دِينَكُمْ وَأَتْمَمْتُ عَلَيْكُمْ نِعْمَتِي وَرَضِيتُ لَكُمُ الْإِسْلَامَ دِيناً]

“Leo nimekukamiliishieni Dini yenu, na nimekutimizieni neema yangu, na nimekupendeleeni UISLAMU uwe ndiyo Dini.” [Al-Ma’ida:3].

Mamlaka ya kutawala watu si ya wahalifu wakubwa, wauaji, na wamwagaji damu, ambao lengo lao kuu ni kupata manufaa ya kidunia kwa ajili ya kuwaridhisha mabwana zao wakoloni. Utawala chini ya Uislamu ni kwa ajili ya watu wema, waadilifu na wasafi tu wanaolinda na kuhifadhi maisha, mali, na heshima ya Waislamu na wasio Waislamu chini ya ulinzi wao kwa sababu wanafahamu kwamba utawala ni jukumu na amana, na kwamba Shariah inawataka wawe na uwezo wa kutekeleza majukumu ya utawala, na kwa sababu wanafuata tu amri za Mwenyezi Mungu (swt), na sio matamanio ya mabepari chini ya mifumo ya kisekula ya kidemokrasia, wanaomfunga Mola wa Walimwengu katika vitendo vya ibada:

[إنِ الْحُكْمُ إِلَّا لِلَّهِ يَقُصُّ الْحَقَّ وَهُوَ خَيْرُ الْفَاصِلِينَ]

“Hapana hukumu ila ya Mwenyezi Mungu. Yeye anasimulia yaliyo kweli; naye ni Mbora wa kuhukumu kuliko wote.” [Al-An’am:57]. Na kauli yake:

[إِنِ الْحُكْمُ إِلَّا لِلَّهِ أَمَرَ أَلَّا تَعْبُدُوا إِلَّا إِيَّاهُ ذَلِكَ الدِّينُ الْقَيِّمُ وَلَكِنَّ أَكْثَرَ النَّاسِ لَا يَعْلَمُونَ]

“Hapana hukumu ila ya Mwenyezi Mungu tu. Yeye ameamrisha msimuabudu yeyote isipo kuwa Yeye tu. Hiyo ndiyo Dini Iliyo Nyooka. Lakini watu wengi hawajui.” [Yusuf:40].

Uislamu utamaliza vita vyote vya utaifa, ukabila, na umadhehebu vilivyo chochewa na wakoloni kwa malengo yao ya ukoloni ya kinyonyaji, kwa sababu Waislamu ni Umma mmoja, mwili mmoja! Vita vyote vilivyopo katika ardhi zetu hususan Sudan ni kwa ajili ya manufaa ya kafiri Magharibi, licha ya onyo la Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw), lililopokewa na Al-Ahnaf bin Qays, ambaye amesema: فَإِنِّي سَمِعْتُ رَسُولَ اللهِ ﷺ يَقُولُ: «إذَا الْتَقَى الْمُسْلِمَانِ بِسَيْفَيْهِمَا فَالْقَاتِلُ وَالْمَقْتُولُ فِي النَّارِ» قُلْتُ: يَا رَسُولَ اللهِ، هَذَا الْقَاتِلُ، فَمَا بَالُ الْمَقْتُولِ؟ قَالَ: «إِنَّهُ كَانَ حَرِيصاً عَلَى قَتْلِ صَاحِبِهِ»؟! “Nimemsikia Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) akisema: “Wanapopigana Waislamu wawili kwa panga zao, muuwaji na mwenye kuuwawa wote wawili wako Motoni.” Nikasema, ‘Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) ni sawa kwa muuaji lakini vipi kuhusu yule aliyeuawa?’ Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) akajibu: “Hakika alikuwa na nia ya kumuua mwenzake.” [Bukhari].

Kwa kumalizia, kuhuisha maisha kamili ya Kiislamu, kama inavyoonyeshwa katika njia ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw), na kama ilivyothibitishwa katika historia yote ya Kiislamu, ndiyo kamba pekee ya uokozi kwa Sudan na ulimwengu mzima wa Kiislamu. Ni Khilafah Rashida ya Pili tu kwa Njia ya Utume pekee ndiyo itakayovunja minyororo yote ya ukoloni wa Magharibi na kung'oa zana zake kutoka kwa ulimwengu wa Kiislamu. Kuutabikisha Uislamu na kuueneza kwa ulimwengu, ni kamba ya uokozi ambayo Hizb ut Tahrir inakupeni bila ya kudai malipo yoyote. Mtapata masuluhisho yote ya migogoro na matatizo yote yaliyotokea kama matokeo ya miongo kadhaa ya kuishi chini ya udhibiti wa hadhara ya Magharibi katika ramani ya Dola ya Khilafah iliyotayarishwa na Hizb ut Tahrir.

Basi, chukueni kamba hii ya uokozi kwani inatoka kwa Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wa walimwengu wote:

[يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اسْتَجِيبُوا لِلَّهِ وَلِلرَّسُولِ إِذَا دَعَاكُمْ لِمَا يُحْيِيكُمْ وَاعْلَمُوا أَنَّ اللَّهَ يَحُولُ بَيْنَ الْمَرْءِ وَقَلْبِهِ وَأَنَّهُ إِلَيْهِ تُحْشَرُونَ]

“Enyi mlio amini! Muitikieni Mwenyezi Mungu na Mtume anapo kuitieni jambo la kukupeni uzima wa milele. Na jueni kuwa Mwenyezi Mungu huingia kati ya mtu na moyo wake, na kwamba hakika kwake Yeye tu mtakusanywa.” [Al-Anfal: 24].

#أزمة_السودان

#SudanCrisis

Imeandikwa kwa Ajili ya Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir na
Zehra Malik

Template Design © Joomla Templates | GavickPro. All rights reserved.