Jumatatu, 09 Rabi' al-awwal 1442 | 2020/10/26
Saa hii ni: (M.M.T)
Menu
Main menu
Main menu

بسم الله الرحمن الرحيم

Nani Atakayesimama Dhidi ya Mauaji ya Halaiki ya Waislamu Eneo la Turkestan Mashariki?

Mnamo tarehe 27 Agosti, shirika la habari la ‘Buzzfeed News’ lilichapisha taarifa zilizotokana na uchunguzi ulioegemea maelfu ya picha za satelaiti katika eneo la ‘Xinjiang’ inayofichua “miundo mbinu mikubwa na inayoendelea ya uwekaji kizuizini na kushikiliwa kwa muda mrefu” kwa jamii za Uyghur, Kazakh na Waislamu wengine inayotekelezwa na utawala wa kidhalimu wa China. Unaonyesha namna “China inavyojenga kwa siri idadi kubwa ya magereza makubwa na makambi ya kuwafunga watu katika miaka 3 iliyopita, kwa uwazi kabisa ikikuuza kampeni yake dhidi ya Waislamu wachache.” Nyingi ya kambi hizi mpya za kuwazuilia watu ni zenye uwezo wa kuwaweka mamia ya maelfu ya watu, kama eneo jipya lililojengwa katika wilaya ya Shufu. Uchunguzi wa Buzzfeed umeonyesha zaidi ya majengo 260 yaliojengwa tokea 2017 yenye kubeba sifa maalum za eneo lililoimarishwa la kuwaweka watu kizuizini, kama kuwa na kuta nene, minara ya walinzi, senyenge na vitu vyengine vinavyofanana na majengo ya magereza yenye ulinzi mkali katika sehemu nyengine za Uchina. Imeelezwa kuwa kuna angalau kambi moja ya aina hii katika kila wilaya ya ‘Xinjiang’ na kuwa baadhi ya maeneo yanakusanya vituo vingi kwa pamoja. Hii inaonyesha uwezo wa utawala na nia ya kuwaweka kizuizini mamia ya maelfu zaidi ya Waislamu katika eneo hilo.

Ujenzi wa mfumo huu mkubwa wa kuwaweka gerezani Waislamu katika Turkestan Mashariki, inaoaminika kuwa na zaidi ya Waislamu milioni moja, unaendelea hadi hivi leo. Huu ndio uzuiaji wa kiwango cha juu zaidi wa jamii ya wachache ya kidini tokea Vita vya Pili vya Dunia. Matokeo haya ya uchunguzi hata hivyo, yanafichua namna kampeni ya Uchina ya kuwaweka ndani idadi kubwa ya Wauyghur na Waislamu wengine katika eneo ni mkubwa zaidi ya ulivyokuwa ukijulikana. Waislamu huweza kuwekwa gerezani kwa jambo la msingi kama kusoma Quran, kufundisha Uislamu, kuwa na ndevu, kuvaa niqab, kutekeleza ibada ya swala na ibada nyenginezo, upakuaji wa Whatsapp ambayo imepigwa marufuku nchini China, kuchunga mshikamano na familia ilioko nje ya nchi, na kuangalia mitandao ya nje. Mahojiano ya waliowahi kuwekwa kizuizini katika kambi hizi wanaelezea mateso yanayofanyika kikawaida, udhalilifu, kuwekwa na njaa, kujazwa kwa wingi kupita kiasi kwa makusudi ndani ya vyumba vya gereza, wafungwa kutengwa na wengine, hali mbaya ya uchafu, uzuiaji wa mimba wa lazima, kufanyishwa kazi kwa nguvu na aina nyengine za unyanyasaji zinazoamriwa kwa wanaowekwa ndani. Baadhi ya wafungwa wa mwanzoni wameelezea pia juu ya ubakaji wa makundi na – “kelele zikienea kila kona ndani ya jengo”. Hii ikiwa ni pamoja na upewaji kasumba wa kila siku wa propaganda za kikomunisti kwa wafungwa. Licha ya kambi hizi za wafungwa ambazo utawala wa China kwa stihzai huziita ‘vituo vya mafunzo ya kiufundi’, idadi ya jamii ya wafungwa ya Xinjiang imekuwa ikiongezeka kwa kasi katika miaka ya karibuni kwa mujibu wa uchambuzi wa gazeti la New York Times juu ya takwimu za serikali ya China. Katika mwaka 2017, eneo hilo lilikuwa na asilimia 21 ya watu wote waliowekwa kizuizini katika China, licha ya kuwa wao ni asilimia 2 tu ya idadi jumla ya watu wote katika nchi, ni ongezeko la mara 8 kutoka mwaka wa nyuma yake.

Yote haya bila shaka ikiwa ni pamoja na mfumo mpana wa ufuatiliaji unaoendelea, sera za ukandamizaji za kuwabebesha fikra ngeni, utasa wa kulazimisha, uondoaji wa watoto kupelekwa nyumba za mayatima za serikali, na sera nyengine za kikandamizaji ambazo Muislamu wa Turkestan Mashariki  amekuwa na anaendelea kukumbwa na utawala wa kishenzi wa China chini ya kivuli cha uongo cha kupambana na ugaidi na hatua za kuzuia ugaidi. Hata hivyo, kwa hakika ni kuwa, lengo lake ni kuondosha athari zote za utambulisho wa Kiislamu wa eneo la Waislamu na kuwatia kasumba ya imani ya kikafiri ya kikomunisti. Hii ni kwa sababu ya kuwafanya wawe watumwa watiifu na vibaraka wa Chama cha Kikomunisti, na kuwa raia waaminifu na watulivu wa dola. Hii upande mmoja inasukumwa na ajenda ya utawala wa China kulinda Mpango wake wa mradi wa trilioni za dolari kuunganisha maeneo katika nchi mbali mbali duniani(Belt and Road Initiative) (BRI), ambao unapitia jimbo la Xinjiang, wenye lengo la kufikia masoko katika Asia ya Kati na Ulaya.

Hali mbaya ya kuvunja moyo na ya kutisha ya Waislamu wa Uyghur na maeneo mengine ya Turkestan Mashariki ni ya kusikitisha sana. Lakini kinachovunja moyo zaidi na ambacho ni cha kushangaza kabisa ni ile kuwa hakuna nchi yoyote ulimwenguni hivi leo iliyo tayari kusimama, au kuchukua hatua yoyote ya maana kumaliza urundikaji huu wa raia wasio na hatia wa kiwango kikubwa, ambao ni marudio ya kambi za mateso za Wanazi wa Kijerumani. Kuna ukosefu mkubwa wa kimaadili katika dunia hii iliotawaliwa na urasilimali, ambapo serikali ziko tayari kushuhudia mauwaji ya watu wengi, mateso ya watu wengi, kurundikwa gerezani kwa watu wengi wasio na hatia, na ukandamizaji wa watu wote, lakini hakuna chochote kumaliza uovu huu dhidi ya wanaadamu kwa kuhofia kupoteza maslahi ya kiuchumi. Kawaida hii ya serikali za Kirasilimali ya kuziweka ‘haki za binaadamu’ rehani, imefupishwa na kukiri kusiko na mvuto kwa Raisi wa Amerika, Donald Trump katika mahojiano na Axios Juni mwaka huu, ambapo aliepuka kuiadhibu China kwa vikwazo dhidi ya uwekwaji wa Uyghur katika makambi ili kulinda mazungumzo ya biashara pamoja na China. Alieleza, “Sisi tulikuwa katikati ya mkataba mkubwa wa biashara.”

Tawala katika ardhi za Waislamu vivyo hivyo zimewauza Waislamu wa Uyghur na hata kusaidia China katika uangamizaji wa kikabila na kampeni ya mauwaji ya kimbari dhidi ya ndugu zao Waislamu katika Turkestan Mashariki kwa ajili ya kupata vitega uchumi vya mabilioni ya dolari kutoka China. Mnamo Julai 2020, Kauli ya pamoja iliosukumwa na Saudi Arabia, Imarati, Bahrain na Ufalme wa Oman, miongoni mwa nyengine ilitolewa ambapo ilieleza kuwa haki za binaadamu za “watu wa makabila yote” wanaoishi maeneo ya magharibi ya mbali ya China zimehifadhiwa kikamilifu.” Mnamo mwezi Februari, 2019 wakati wa ziara ya kibiashara nchini China, shirika la habari la serikali la Xinhua, liliripoti kuwa Mwana Mfalme Muhammad bin Salman alimwambia Raisi wa China Xi Jinping, “Tunaheshimu na kuunga mkono haki ya China kuchukua  hatua za kupambana na ugaidi na misimamo mikali kuhifadhi usalama wa taifa.” Ilikuwa ni ziara ambapo Saudi Arabia na China zilitia saini mikataba 35 ya ushirikiano wa kiuchumi wenye thamani ya $28 bilioni, kwa mujibu wa shirika la habari la serikali la Saudia SPA.

Hapana shaka, kuwa katika miaka ya karibuni, uchumi wa nchi za Ghuba zinazotegemea mafuta umekuwa ukishuka na unaendelea kutegemea fedha na biashara kwa Uchina.  Kwa mujibu wa Taasisi ya Ufuatiliaji wa takwimu za Vitega Uchumi vya China Duniani, (China Global Investment Tracker), Uchina imewekeza zaidi ya dolari bilioni 50 katika nchi za Baraza la Ushirikiano la nchi za Ghuba (GCC) baina ya 2016 na 2020. Mfano mwengine wa utegemezi ni kuwa asilimia 80 ya mafuta ambayo Oman inayauza nje yanasafirishwa China.

Hivyo, mgeuko wa ghafla wa sera za Shirika la Ushirikiano wa nchi za Kiislamu (OIC) (unaokusanya nchi 57) katika mtiririko wa jumbe za tweets Disemba 2018 ambapo imetaja “taarifa za kuchukiza” za ukandamizaji Waislamu wa China, haistaajabishi. Imegeuza msimamo wake wa awali kwa kutoa taarifa ikisema kuwa “kupongeza jitihada za Jamhuri ya Watu wa China katika kuwashughulikia raia wake Waislamu ikiangazia mbele katika ushirikiano zaidi baina ya OIC na Jamhuri ya Watu wa China.” Astaghfirullah! Nchi nyingi wanachama wa OIC ni wafaidika wa biashara za China au fedha, au zipo karibu na miradi ya miundombinu ya kuleta faida inayohusisha BRI ya Uchina. Kwa hivyo haishangazi kuwa serikali hizi zilizo na msukumo wa kimagharibi, zikiwa na misingi na sera zao za kirasilimali, hawaoni aibu kwa kuwaweka ndugu zao na dada zao Waislamu wa Uyghur kuwa ni wahanga kwa ajili ya wengine kwa kubadilishana na maslahi ya kiuchumi. Wameuza nafsi zao kwa ajili ya dolari.

Serikali ya Pakistan pia nayo imefuata mkumbo katika kuwatelekeza Waislamu wa Turkestan Mashariki. Katika Jukwaa la Uchumi la Dunia lililofanyika Davos Januari mwaka huu, Waziri Mkuu wa Pakistan, Imran Khan, aliungama alipoulizwa na wanahabari, kuwa alikataa kulaumu matendo ya Uchina dhidi ya Waislamu wa Uyghur kutokana na mahusiano maalum ya uchumi na Uchina. Alieleza kuwa China “imetusaidia tulipokuwa katika kiwango cha chini.” Imran Khan kwa fedheha alikwepa maswali kutoka kwa wanahabari katika mkutano wa mwanzoni juu ya kuwekwa ndani kwa idadi kubwa ya Waislamu, akitamka bila aibu kuwa “haelewi kwa kina” kuhusu taarifa hizo, licha ya kuwa hali mbaya ya Wauyghur imekuwa ikigonga vichwa vya habari na kuwa ni suala la mjadala ulioenea katika vyombo vya habari vya kijamii wakati huo, wakati pia akielezea kuwa, “Uchina imekuwa ni pumzi yetu ya hewa safi.”

Pamoja na hayo, uongozi wa Pakistan, kwa aibu umeipongeza China katika Baraza la UN la Haki za Binaadamu kwa “kuwahudumia raia wake Waislamu” wakati pia ikijisafisha na jukumu katika kusimama dhidi ya mauwaji ya kimbari ya Waislamu wa Uyghur kwa kuliweka kuwa ni ‘suala la ndani’.

Waziri wa kigeni wa Pakistan amefikia hata kuvishutumu kwa kuvidhalilisha vyombo vya habari kwa “kujaribu kulikuuza” suala la Xinjiang. Labda ni muhimu kudokeza kuwa Pakistan ni moja ya mpokeaji mkubwa wa mikopo ya China na miradi ya miundombinu.

Ukanda wa Uchumi wa Uchina na Pakistan kwa mfano, ambao ni mkusanyiko wa miradi ya miundombinu iliyo katika ujenzi kote Pakistan ikiwa ni sehemu ya vitega uchumi vya China BRI vimethaminiwa kufikiwa dolari bilioni 62 katika mwaka 2017. Ni wazi kuwa Uchina imemnyamazisha Imran Khan na serikali yake! Kwa hakika, mwezi huu wa Agosti, vyanzo mbali mbali vya habari vimeripoti kuwa utawala wa Pakistan umewasilisha tathmini ya ripoti ya ndani kwa ujumbe wa China katika Islamabad iliofanywa kwa ajili ya kupima na kudhibiti maoni ya umma na harakati zinazofanywa kama majibu kwa uovu wa China dhidi ya Waislamu wa Uyghur. Lengo kuu la uchunguzi wa ndani wa Pakistan lilikuwa ni kudhibiti na kuzuia dhihirisho baya kwa wananchi na hamasa zinazohusiana na suala hilo, hasa kutoka katika makundi ya kidini katika jamii, ambayo yanaweza kuleta madhara kwa mahusiano baina ya nchi hizi mbili.

Uongozi wa Uturuki pia, japokuwa umepongezwa na baadhi kwa kukemea makambi ya kuwarundika Waislamu wa China, haijafanya chochote cha maana kumaliza uwekwaji huu magerezani wa watu wengi na mateso ya Waislamu katika Turkestan Mashariki. Suala la kuwa vitega uchumi vya Uchina katika Uturuki ilikuwa kiasi cha dolari bilioni 3 kufikia mwaka 2019, kukiwa na zaidi ya makampuni alfu moja yanayofanya kazi nchini humo, na kwamba vitega uchumi vitafikia dolari bilioni 6 mwaka 2021 kwa mujibu wa balozi wa China nchini Uturuki, yamkini imekuwa ni sehemu yenye uzito katika upendeleo wa Erdogan wa kusita kwa muitikio wake juu ya mauwaji ya halaiki dhidi ya Wauyghur kwa kuishia kutamka tu mdomoni badala ya kufanya juhudi za maana kumaliza uovu huu wa kihaini dhidi ya ndugu zake Waislamu wa kiume na kike.

Kwa sababu hiyo hivi leo, hakuna dola wala serikali, wala kiongozi aliye na utashi wa kisiasa, utambuzi wa kimaadili, au ubavu wa kusimama kwa dhati kuwahami Waislamu wa Turkestan Mashariki, na hakika kwa kila mtu anayedhulumiwa. Hakuna dola inayotoa jibu kwa maovu yalio machungu zaidi dhidi ya wanaadamu – ima yawe ni mauwaji ya zaidi ya Waislamu milioni moja nchini Syria, au mauwaji ya kimbari ya watu wa Rohingya, Myanmar, au mauwaji ya watoto wa Kiislamu katika Jamhuri ya Afrika ya Kati au urundikaji wa zaidi ya Waislamu milioni moja wa Xinjiang wasio na hatia! Na haitopatikana wakati siasa za dunia hii zikiwa zimetawaliwa na mifumo ya kirasilimali na tawala zenye kujali maslahi yao binafsi. Kwani tunaishi katika dunia ambapo thamani ya maisha ya mwanaadamu hupimwa kwa mujibu wa kiwango cha faida inayoweza kuizalisha!

Hivyo, wale wanaodhulumiwa hupuuzwa, wanaachwa hawajiwezi na katika hali ya kukata tamaa, na kuwachwa katika matashi ya watesaji wao. Hii ndio hali ambayo kwa kweli haiwezi kuachwa kuendelea! Kutegemea Umoja wa Mataifa au serikali yoyote ya kimagharibi kuja kusaidia ndugu zetu wa Kiislamu wa kike na wa kiume ni ujinga kamwe! Hautoi chochote isipokuwa matumaini ya uongo na kurefusha maafa na shida! Kwa hakika, kila Muislamu anapaswa kutambua kuwa hakuna dola hivi leo ambayo itakuja kuwaokoa pindi wakiwa wahanga wa mateso au mauwaji.

Baada ya kutambua haya, hivyo hatujawa na udharura wa kuwa na dola, mfumo na uongozi ambao kwa dhati kabisa unajali walimwengu na utasimama kwa ajili ya maslahi ya Waislamu? Je, kuna mfumo mwengine wowote unaotoa haya, mbali na ule ulioteremshwa na Muumba wa Walimwengu, Mwenyezi Mungu (swt), Mjuzi, Mwenye Hekima? Basi kwa hakika, kama tunataka kwa dhati kumaliza maafa haya yenye kuogofya kwa Ummah wetu katika Turkestan Mashariki, Syria, Palestina, Kashmir, Afrika ya Kati, Myanmar na kwengine kokote, ni lazima tulenge mazingatio yetu yote na kutoa bidii zetu zote katika kusimamisha Mfumo wa Kiislamu – Khilafah kwa njia ya Utume, ambayo Mtume (saw) ameielezea kuwa ni ngao na mlinzi wa Waumini.

Chini ya mfumo huu, mtawala Khalifah Al Muttasim alipeleka jeshi zima kumuokoa mwanamke mmoja Muislamu aliyetekwa na Warumi. Bado hivi leo, kuna zaidi ya Waislamu milioni moja wasio na hatia wanadhoofika katika magereza ya madikteta, lakini hakuna kiongozi anayechukua hatua! Chini ya Khilafah, Khalifah wa Kiuthmani Bayezid II alipeleka manuwari zake kuwaokoa Mayahudi wa Ulaya 150,000 waliokuwa wakiteswa na watawala wa Kikristo wa Uhispania wakati wa Mateso ya Kihispania (Spanish Inquisition) na wakaletwa ndani ya dola ya Khilafah, kwa kuwa hii ndio hali ya msimamo wa kweli kwa wanaoteswa, bila ya kuzingatia dini zao, kabila au taifa! Ni Khilafah pekee ndio yenye utashi wa kisiasa wa kusimama dhidi ya dola yoyote inayowatesa Waislamu, na ambayo haitoweza kununuliwa na mvuto wa mali! Bali itatumia kila nguvu iliyo nayo katika uwezo wake kutia hofu katika nyoyo za maadui wa Uislamu, na kumkomboa kila Muislamu anayeteswa kutokana na makucha ya watesaji. Hivyo, tunamlingania kila Muislamu mwenye ikhlasi kuitikia amri za Mola wake:

(وَإِنِ اسْتَنصَرُوكُمْ فِي الدِّينِ فَعَلَيْكُمُ النَّصْرُ)

“Na wakiomba msaada katika dini basi ni juu yenu kuwasaidia” [8:72] kwa kubeba da’wah kwa haraka kusimamisha Mfumo wa Mwenyezi Mungu (swt), Khilafah – kwani bila hiyo, mateso, mauwaji na dhiki kwa Ummah wetu, na bila shaka kwa wanaadamu, yataendelea kwa nguvu zote!

Imeandikwa kwa Ajili ya Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir na

Dkt. Nazreen Nawaz

Mkurugenzi wa Kitengo cha Wanawake katika Afisi Kuu ya Habari ya Hizb Ut Tahrir

Imebadilishwa mara ya mwisho mnamoAlhamisi, 17 Septemba 2020 17:17

Andika maoni

Hakikisha umejaza (*) habari zinazohitajika palipoashiriwa. Kodi za HTML haziruhusiwi.

rudi juu

Vifungu vya Tovuti

Viunganishi

Magharibi

Ardhi za Waislamu

Ardhi za Waislamu