Alhamisi, 09 Shawwal 1445 | 2024/04/18
Saa hii ni: (M.M.T)
Menu
Main menu
Main menu

بسم الله الرحمن الرحيم

 Silsila ya Maswali Yaliyowasilishwa kwa

Amiri wa Hizb ut Tahrir

Sheikh Ata Bin Khalil Abu Al-Rashtah Katika Ukurasa Wake wa Facebook wa “Kifiqh”

Jibu La Swali:

Maana ya Hadithi:

«وَتَفْتَرِقُ أُمَّتِي عَلَى ثَلَاثٍ وَسَبْعِينَ فِرْقَةً»

“Ummah wangu utagawanyika makundi sabiini na tatu.”

Kwa: Abdullah Omar

(Imetafsiriwa)

Swali:

Assalamu Alaykum Wa Rahmatullah Wa Barakatuhu

Mimi ni Abdullah kutoka Afghanistan, Mwenyezi Mungu akulinde Sheikh wetu,

Mjumbe wa Mwenyezi Mungu (saw) amesema:

« ستنقسم أمتي إلى ثلاثة وسبعين فرقة وكلها في النار ما عدا واحدا »

"Umma wangu utagawanyika makundi sabini na tatu na yote yataingia motoni isipokuwa kundi moja tu."

Natumai utaielezea Hadithi hii.

Jibu:

Wa Alaikum Assalam Wa Rahmatullah Wa Barakatuhu,

Kwanza: Hadithi unayoiulizia haisimuliwi katika muundo uliowasilishwa katika swali lako, na tulikuwa tumeiweka wazi hadithi hii katika Jibu la Swali lililochapishwa mnamo 24 Rabii 'ul-Akhir 1439 H sawia na 11/01/2018 M, katika mapokezi kadhaa, ambayo mengine ni pamoja na nyongeza tofauti, na tulihitimisha mwishoni mwa jibu kuwa: (hadithi inayohusu mgawanyiko wa Ummah katika madhehebu 73 bila nyongeza yoyote ni hadithi sahihi… na kwamba hio ni riwaya ya kwanza:

"كلها في النار إلا واحدة" "Yote yataingia motoni isipokuwa kundi moja tu " imezingatiwa na wengi kuwa ni hasan… ama kuhusu riwaya ya pili:

"كلها في الجنة إلا واحدة" "Yote yataingia Peponi isipokuwa moja tu," wengi wameichukulia ni dhaifu, na wachache tu wameiona kuwa ni sahih au hasan; kwa hivyo, naona ya kuwa yenye uzito zaidi ni rai ya kuwa nyongeza katika mapokezi:

"كلها في النار إلا واحدة" "Yote yataingia motoni isipokuwa moja" inakubaliwa, ama kwa ile inayoelezea:

"كلها في الجنة إلا واحدة" "Yote yataingia Peponi isipokuwa moja," haikubaliki, hii ni kwa kuregelea yale tuliyotoa katika masimulizi yanayojumuisha nyongeza zote mbili...) Na kulingana na yale tuliyoyataja katika jibu la swali lililotajwa hapo juu. Kati ya masimulizi yanayoweza kutegemewa na kutiliwa maanani ni masimulizi yafuatayo:

- Tirmidhi ameripoti katika Sunan yake kwamba Abu Hurayrah (ra) amesimulia: Mtume (saw) amesema:

« تَفَرَّقَتْ الْيَهُودُ عَلَى إِحْدَى وَسَبْعِينَ أَوْ اثْنَتَيْنِ وَسَبْعِينَ فِرْقَةً وَالنَّصَارَى مِثْلَ ذَلِكَ وَتَفْتَرِقُ أُمَّتِي عَلَى ثَلَاثٍ وَسَبْعِينَ فِرْقَةً »

“Mayahudi waligawanyika katika makundi sabini na moja au sabini na mbili; na Wakristo waligawanyika mfano wa hivyo; na Ummah wangu utagawanyika katika makundi sabini na tatu.”

Na katika mlango huo huo, Sa’ad na Abdullah ibn Amr na ‘Awf ibn Malik walisema: Abu Issa alisema: Hadith ya Abu Hurayrah ni Hasan Sahih. Katika riwaya nyingine ya Tirmidhi kwamba Abdullah ibn Amr amesema: Mtume (saw) amesema:

«... وَإِنَّ بَنِي إِسْرَائِيلَ تَفَرَّقَتْ عَلَى ثِنْتَيْنِ وَسَبْعِينَ مِلَّةً وَتَفْتَرِقُ أُمَّتِي عَلَى ثَلَاثٍ وَسَبْعِينَ مِلَّةً كُلُّهُمْ فِي النَّارِ إِلَّا مِلَّةً وَاحِدَةً قَالُوا وَمَنْ هِيَ يَا رَسُولَ اللَّهِ قَالَ مَا أَنَا عَلَيْهِ وَأَصْحَابِي»

"...Bani Isra'il waligawanyika katika mila (makundi) 72, lakini watu wangu watagawanyika katika mila (makundi) 73, yote yataingia motoni isipokuwa moja tu." Alipoulizwa ni lipi ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, alijibu, "Ni lile ambalo mimi na Masahaba wangu tupo." Abu Issa amesema kuwa Hadith hii ni Hasan Gharib…

- Al-Hakim katika Al-Mustadrak ameripoti katika sahih mbili kwamba Abu `Amir Abdullah bin Luhay amesema;

حَجَجْنَا مَعَ مُعَاوِيَةَ بْنِ أَبِي سُفْيَانَ... ثُمَّ قَامَ حِينَ صَلَّى الظُّهْرَ بِمَكَّةَ، فَقَالَ: قَالَ النَّبِيُّ ﷺ: «إِنَّ أَهْلَ الْكِتَابِ تَفَرَّقُوا فِي دِينِهِمْ عَلَى اثْنَتَيْنِ وَسَبْعِينَ مِلَّةً، وَتَفْتَرِقُ هَذِهِ الْأُمَّةُ عَلَى ثَلَاثٍ وَسَبْعِينَ كُلُّهَا فِي النَّارِ إِلَّا وَاحِدَةً وَهِيَ الْجَمَاعَةُ...»

"Tulifanya Hija na Mu`awiyah bin Abi Sufyan. Tulipofika Makkah, alisimama baada ya kuswali Dhuhr na akasema; 'Mjumbe wa Mwenyezi Mungu (saw) amesema: "Hakika watu wa Kitabu wamegawanyika katika dini yao makundi (millah) sabiini na mbili, na Umma huu utagawanyika makundi sabiini na tatu yote yataenda Motoni isipokuwa moja nalo ni jamaa (kundi kubwa lao)...” Al-Hakim amesema: sanad hii ya wapokezi ni uthibitisho katika kuainisha hadith hii kuwa ni Sahih... na Al-Dhahabi amekubaliana naye.

‘Ahl ul-Kitab waligawanyika katika makundi (mila) sabiini na mbili. Ummah huu utagawanyika katika makundi (mila) sabiini na tatu, yote yataingia Motoni isipokuwa moja, ambalo ni Jama`ah (kundi kubwa lao). Baadhi katika Umma wangu utaongozwa na matamanio, kama yule aliye ambukizwa na kichaa cha mbwa; hakuna mshipa au kiungo kitakacho okolewa kutokana na tamaa hizi.’

- Abu Dawud katika Sunan yake, na Ibn Majah pia waliripoti riwaya kama hiyo.

Pili: maana tunayoiona ina nguvu zaidi katika Hadith hii ni kama ifuatavyo:

1. Vikundi na migawanyiko ya kiistilahi imetumika sana katika Sharia katika mantiki ya mgongano katika Aqidah na katika chimbuko la Dini, na mgongano katika ushahidi wa hakika na wa wazi:   

- Mwenyezi Mungu (swt) asema:

(وَلَا تَكُونُوا كَالَّذِينَ تَفَرَّقُوا وَاخْتَلَفُوا مِنْ بَعْدِ مَا جَاءَهُمُ الْبَيِّنَاتُ وَأُولَئِكَ لَهُمْ عَذَابٌ عَظِيمٌ)

"Wala msiwe kama wale waliofarikiana na kukhitilafiana baada ya kuwafikia hoja zilizo wazi. Na hao ndio watakaokuwa na adhabu kubwa.” [Aali-Imran: 105].

- Mwenyezi Mungu (swt) asema: 

(وَمَا تَفَرَّقَ الَّذِينَ أُوتُوا الْكِتَابَ إِلَّا مِنْ بَعْدِ مَا جَاءَتْهُمُ الْبَيِّنَةُ)  “Wala hawakufarikiana waliopewa Kitabu ila baada ya kuwajia hiyo bayana.” [Al-Bayyina: 4].

- Mwenyezi Mungu (swt) anasema:

(إِنَّ الدِّينَ عِنْدَ اللَّهِ الْإِسْلَامُ وَمَا اخْتَلَفَ الَّذِينَ أُوتُوا الْكِتَابَ إِلَّا مِنْ بَعْدِ مَا جَاءَهُمُ الْعِلْمُ بَغْياً بَيْنَهُمْ وَمَنْ يَكْفُرْ بِآيَاتِ اللَّهِ فَإِنَّ اللَّهَ سَرِيعُ الْحِسَابِ)

“Bila ya shaka Dini mbele ya Mwenyezi Mungu ni Uislamu. Na waliopewa Kitabu hawakukhitilafiana ila baada ya kuwajia ujuzi, kwa sababu ya uhasidi uliokuwa baina yao. Na anayezikataa ishara za Mwenyezi Mungu basi hakika Mwenyezi Mungu ni mwepesi wa kuhisabu.” [Aali-Imran:19]

- Mwenyezi Mungu (swt) asema:

(إِنَّ الَّذِينَ فَرَّقُوا دِينَهُمْ وَكَانُوا شِيَعاً لَسْتَ مِنْهُمْ فِي شَيْءٍ إِنَّمَا أَمْرُهُمْ إِلَى اللَّهِ ثُمَّ يُنَبِّئُهُمْ بِمَا كَانُوا يَفْعَلُونَ)

“Hakika walioigawa Dini yao na wakawa makundi makundi, huna uhusiano nao wowote. Bila ya shaka shauri yao iko kwa Mwenyezi Mungu; kisha atawaambia yale waliokuwa wakiyatenda.” [Al-An'am: 159]

2. "Kundi" hapa katika hadith hizi inamaanisha watu wa dini ya Uislamu, na maandishi ya kisharia yamewekwa wazi ambayo yanafafanua maana hii, pamoja na Hadith zilizowafikiwa. Abdullah ibn Mas'oud amesema: Mjumbe wa Mwenyezi Mungu (saw ) amesema:

«لَا يَحِلُّ دَمُ امْرِئٍ مُسْلِمٍ يَشْهَدُ أَنْ لَا إِلَهَ إِلَّا اللَّهُ وَأَنِّي رَسُولُ اللَّهِ إِلَّا بِإِحْدَى ثَلَاثٍ الثَّيِّبُ الزَّانِي وَالنَّفْسُ بِالنَّفْسِ وَالتَّارِكُ لِدِينِهِ الْمُفَارِقُ لِلْجَمَاعَةِ»

"Si halali kumwaga damu ya Muislamu anaye shuhudia kuwa hapa mola wa kuabudiwa kwa haki ila Mwenyezi Mungu na kwamba mimi (Muhammad) ni Mtume wa Mwenyezi Mungu, isipokuwa katika hali tatu: mzinifu aliyeowa, nafsi kwa nafsi, na yule aliyeiacha dini yake na kujitenga na jamaa.”

Hii ni riwaya ya Muslim. Katika hadith hii adhimu, Mtume (saw) alielezea kuwa kujitenga na kundi ni sawa na kutoka katika Dini na kuitupa kwa sababu alimchukulia yule anayeitupa Dini yake kuwa yupo tofauti na kundi, kwa hivyo kinachofunzwa hapa ni kwamba neno kundi kwa maana hii ni kutoamini na ni sawa na kuacha Dini na Imani (itikadi)…

- Imetajwa katika Fath Al-Bari, Sherhe ya Sahih Al-Bukhari ya Ibn Hajar, yafuatayo:

[…kauli yake ‘yule anayeitelekeza Dini yake, akaachana na kundi kama ilivyo kuja katika kauli ya Abu Dhar kwa Akashmihani na waliobaki, na ‘yule anayejiweka mbali na Dini (Mareq)’, lakini katika mapokezi ya Nasafi, Sarkhasi na Almustmli: 'kuikataa Dini yake' Al-Taybi amesema: yule anayeikataa Dini yake ndiye anayeitelekeza; imechukuliwa kutokana na neno "kuiasi" ambalo linamaanisha "kuacha/kutelekeza". Katika masimulizi ya Muslim: "na yule anayejitenga na dini yake na kuachana na kundi," na katika mapokezi ya Al-Thawri: "na yule anayeacha dini yake na kujitenga na kundi." ... na kinachomaanishwa kwa neno 'kundi' ni wafuasi wa Uislamu, yaani amejitenga nao au kuwaacha, ikimaanisha ni muasi, kwani uasi ni sifa ya yule aliyeondoka au kujitenga... Al-Baydawi alisema: yule anayeiacha Dini yake ni mwenye sifa dhahiri ya "Mareq" yaani yule aliyejitenga na kundi la Waislamu na kuacha safu zao…] MWISHO.

3. Kauli yake (saw) katika hadith tofauti: «وَتَفْتَرِقُ أُمَّتِي» “Ummah wangu utagawanyika,” «وَتَفْتَرِقُ هَذِهِ الْأُمَّةُ» “Ummah huu utagawanyika,” «وَإِنَّ هَذِهِ الْمِلَّةَ سَتَفْتَرِقُ» “Mila (imani) hii itagawanyika” zote ziko wazi kuwa Ummah au mila hapa inamaanisha Umma wa Uislamu unaoamini dini ya Uislamu, kama Mtume (saw) alivyo ongezea katika moja ya mapokezi ya neno Ummah kwake mwenyewe «أُمَّتِي» “Ummah wangu,” «هَذِهِ الْأُمَّةُ» “Ummah huu,” na «وهَذِهِ الْمِلَّةَ» "Mila hii” kwa hivyo ni wazi kwamba Hadith inazungumzia Ummah mmoja na mila moja, Ummah wa Kiislamu…

4. Kama inavyojulikana, baadhi ya ikhtilafu katika Uislamu ni zenye kulaumiwa na nyengine ni zenye kusifiwa. Ama kwa ikhtilafu zenye kusifiwa, ni ikhtilafu katika maswala ya Ijtihad kutokana na kutofautiana katika ufahamu wa maandiko, kwa kupata kwake ujira mara mbili yule aliyepatia (katika hukmu), na kulipwa mara moja kwa yule aliyekosea (katika hukmu) kama ilivyotajwa katika Hadithi iliyosimuliwa na Bukhari katika Sahih yake, kwamba Amr ibn Al-Aas alimsikia Mjumbe wa Mwenyezi Mungu (saw) akisema:

«إِذَا حَكَمَ الْحَاكِمُ فَاجْتَهَدَ ثُمَّ أَصَابَ فَلَهُ أَجْرَانِ وَإِذَا حَكَمَ فَاجْتَهَدَ ثُمَّ أَخْطَأَ فَلَهُ أَجْرٌ »

“Pindi hakimu anapohukumu akajitahidi na akapatia atapata ujira mara mbili. Anapohukumu akajitahidi kadri ya uwezo wake na kukosea atapata ujira mara moja.” Ama ikhtilafu yenye kulaumiwa, inajumuisha ikhtilafu katika Aqidah, dalili na hukmu za kukatikiwa, ni aina ya ikhtilafu inayomfanya mtu auasi Uislamu, aina nyingine ya ikhtilafu hii ni ile inayotokana na matakwa na matamanio kama ikhtilafu kati ya watu wa uzushi (bid'ah), wale ambao hawaamini katika uzushi wao, na pia ni pamoja na kutokubaliana juu ya imamu na utiifu kwake, na pia aina nyengine ya ikhtilafu zenye kulaumiwa ni ambazo muhusika hatoki nje ya Uislamu…

Tatu: Kulingana na uchunguzi uliotajwa hapo juu na kwa kuuzingatia, tunaweza kuelewa Hadith tukufu juu ya mgawanyiko wa Mayahudi na Wakristo na mgawanyiko wa Umma wa Uislamu ... na maelezo yake ni kama ifuatavyo:

1. Mwenyezi Mungu (swt) alimtuma Musa (AS) na dini ya ukweli kwa Bani Israil, wale waliomwamini na wakawa pamoja naye kwenye 'Aqidah ya ukweli na Tawhid wamekuwa ni watu wa imani moja (millah).. hata hivyo, baadhi ya vikundi vya watu walijitenga na imani hii kila muda ulivyosonga, wakitofautiana nayo katika Dini «إِنَّ أَهْلَ الْكِتَابِ تَفَرَّقُوا فِي دِينِهِمْ عَلَى اثْنَتَيْنِ وَسَبْعِينَ مِلَّةً» "Hakika watu wa kitabu wamegawanyika katika Dini yao makundi (milla/itikadi) sabiini na mbili," wakitengana na imani yake, ushahidi na dini wazi ya Musa (AS), wakiiwacha Dini yake na kuwa makafiri. Makundi hayo yalioacha Dini ya Musa yakawa makundi tofauti na yenye maoni tofauti katika uasili wa Dini (aqidah) «إِنَّ أَهْلَ الْكِتَابِ تَفَرَّقُوا فِي دِينِهِمْ عَلَى اثْنَتَيْنِ وَسَبْعِينَ مِلَّةً» "Hakika watu wa kitabu wamegawanyika katika Dini yao makundi sabiini na mbili," wamefikia milla sabiini au sabiini na moja, ambayo yote ni makundi yasioamini ya watu wa motoni, ama kwa kundi lililobakia kwenye Dini ya Musa (AS), yaani imani ya Musa (AS), ambalo ni kundi la 71 au la 72, ni kundi lililo juu ya ukweli na ni katika watu wa Jannah, na ni kundi lililookoka (Firqat al-Najiyah) kutoka kwa wafuasi wa Nabii wa Mwenyezi Mungu, Musa (AS)…       

 2. Pia, Mwenyezi Mungu (swt) alimtuma Issa (AS) na dini ya kweli kwa Bani Israil, wale waliomwamini na kukusanyika pamoja naye kwenye Aqidah ya kweli na Tawhid wakawa ni watu wa imani moja (millah).. lakini, makundi ya watu waliojitenga na imani hii kidogo kidogo, wakitafautiana nayo katika Dini, wakitengana na imani yake, ushahidi na Dini ya wazi ya Issa (AS), wakaiacha Dini yake na kuwa makafiri. Makundi hayo yaliyoiacha Dini ya Issa (AS) na kuwa makundi tofauti yenye maoni tofauti katika asili ya Dini (aqidah) yamefikia makundi sabiini na moja, yote ni makundi ya watu wasioamini ya watu wa motoni, ama kwa dhehebu lililobakia juu ya Dini ya Issa (AS), yaani imani ya Issa (AS), ambalo ni kundi la 72, liko juu ya haki na ni katika watu wa Jannah, na limekuwa ni kundi lililookoka (Firqat al-Najiyah) kutoka kwa wafuasi wa Nabii wa Mwenyezi Mungu Issa (AS)…

3. Baadaye Mwenyezi Mungu (swt) alimtuma Nabii wake Muhammad (saw) kwa Dini ya haki na 'Aqidah ya Tawhid, Waislamu walimuamini na wakaungana juu ya 'Aqidah ambayo Mtume (saw) na masahaba wake watukufu waliiamini, na kwa umoja huu, wakawa Umma wa Kiislamu na imani ya Uislamu na Jama’ah (kundi)… lakini makundi yalikengeuka (na yataendelea kukengeuka) kutoka kwa Dini ya Muhammad (saw), na yamejitenga (na yatajitenga) na kile ambacho Mtume (saw) na masahaba zake na Waislamu wengine wameamini katika 'Aqidah ya Uislamu na Nusus za wazi na dalili za Uislamu ... kwa hivyo, kila moja ya madhehebu hayo yaliojitenga na Uislamu limekuwa kundi na imani inayotafautiana na imani ya Uislamu, kwa sababu waliamini imani ambazo ni kinyume na za Uislamu… makundi hayo ambayo wafuasi wao walikuwa Waislamu kisha walijitenga na Uislamu yamefikia au yatafikia makundi/imani 72, na yote ni makundi ya ukafiri na ni ya watu wa motoni... kundi/imani(millah) ya 73, kundi mama, ambalo ni kundi (jama'ah) na dhehebu la Uislamu ambalo linaamini kile ambacho Mtume (saw) na masahaba watukufu waliamini, wakishikamana na Nususi za wazi na dalili za Uislamu, ni Umma wa Uislamu ambao unamuamini Mwenyezi Mungu (swt), Malaika Wake, Vitabu Vyake, Mitume Wake, Siku ya Mwisho na Qadhaa Wal-Qadar – kizuri chake na kibaya chake ni kutoka kwa Mwenyezi Mungu (swt)… ni Ummah wa Uislamu kwa jumla, kundi lililookoka (al-Firqat al-Najiyah) na ni katika watu wa Jannah, kundi na aqida iliyounganishwa juu ya yale ambayo Mtume (saw) na masahaba wake wameibeba, nalo ni (kundi) Jama'ah.

Nne: Kulingana na ufafanuzi huu wa maana ya hadith na uhalisia wake, tunaweza kuhitimisha kwa yafuatayo:

1. Kundi lililookolewa (al-Firqa al-Najiyah) ni Ummah wa Kiislamu kwa maana yake ya jumla, nao ndio uliokusanyika juu ya 'Aqidah ya Uislamu na uwazi wa Dini na dalili zake, bila kujali tofauti kati ya rai zao, fikra, na madhehebu juu ya masuala yote ya matawi ya imani na matakwa ya Shari'ah... nk, na sababu ya kudumu kwake na kuwa kundi la watu wa Jannah ni imani yao katika 'Aqidah ya Uislamu, uhakika wake na ushahidi wake... Na hivyo hivyo:

a) Ahlul-Sunnah wal Jama'ah miongoni mwa watu wa kauli (kalam), kama Ash'ari, Maturidiyya, na mapote yote mengine ya kifikra, pamoja na wale wanaoitwa "Salafi", watu wa hadith, na waandishi wengine wa makala na makundi ya fikra za Kiislamu… wote ni katika Al-Firqa Al-Najiyah kwa neema ya Mwenyezi Mungu (swt) kwa sababu wao ni wafuasi wa Muhammad (saw), waumini wa 'Aqidah ya Uislamu, uhakika wake na ushahidi wake ... na tofauti kati yao haziwatoi katika kundi la Uislamu.

b) Na madhehebu tofauti ya kifiqhi ya Hanafi, Maliki, Shafi'i, Hanbali na madhehebu mengine ya kifiqhi, na wafuasi wa mujtahidina anuwai ... wote hao ni miongoni mwa watu wa kundi lililookolewa, kwa mapenzi ya Mwenyezi Mungu (swt), kwa sababu wao ni wafuasi wa Muhammad (saw), waumini wa 'Aqidah ya Uislamu, uhakika wake na dalili... na tofauti kati yao haiwatoi katika kundi la Uislamu.

c) Na makundi ya Kiislamu na harakati za Kiislamu zinazofanya kazi katika medani za zama zetu, kama Hizb ut Tahrir, Ikhwan al-Muslimina, Kundi la Tabligh, makundi ya jihad, makundi ya Salafi, na mengineo… yote ni kutoka kwa watu wa kundi lililookolewa, kwa mapenzi ya Mwenyezi Mungu (swt), kwa sababu wao ni wafuasi wa Muhammad (saw), waumini wa 'Aqidah ya Uislamu, uhakika wake na dalili... na tofauti kati yao haiwatoi katika kundi la Uislamu.             

Kwa hivyo, sio sahihi kwa kundi lolote la Ummah Kiislamu kudai, kwa msingi wa hadith hii tukufu, kwamba ndilo kundi lililookolewa na dhehebu lililookolewa kwa sababu hii itamaanisha kuwa inawaondoa Waislamu wasiokubaliana nayo kutoka kwenye duara la Uislamu na kuingia ndani ya duara la wasioamini, na hii sio sawa katika hali yoyote, kwa sababu Waislamu wote ambao wanaamini 'Aqidah ya Uislamu, wanaozingatia uhakika na ushahidi wake ni katika kundi lililookolewa, kwa matakwa ya Mwenyezi Mungu (swt).

4. Mapote yaliyoacha kundi la Uislamu na wakawa makafiri na hivyo kustahili kuwa makundi ya watu wa Motoni, ni makundi yaliyokiuka Dini na kuachana na imani (Aqidah) ya Waislamu na kuvuka mipaka ya Uislamu na uhakika wake na dalili, kwa hivyo wamemshirikisha Mwenyezi Mungu (swt) na vitu vyengine au wakamfuata mtume baada ya Muhammad (saw) au kukataa Sunna ya Mtume wa Mwenyezi Mungu au mfano wake... kama Ma-Druze, wa-Nusayri, ma-Bahai, ma-Qadiani na makundi mengine ya kikafiri nje ya Uislamu... na wenziwao kutoka kwa Mayahudi waliokengeuka kutoka dini ya Musa, amani iwe juu yake, watu waliomfanya 'Uzeyr, amani iwe juu yake, mwana wa Mungu, na miongoni mwa wafuasi wa Issa, amani iwe juu yake, waliomfanya kuwa mwana wa Mungu ... kwa hivyo watu hao walibadilika katika imani zao dhidi ya imani na dini ya Manabii hawa wawili mashuhuri, kwa hivyo wakawa makafiri.

Natumai kuwa maana ya hadith imekuwa wazi kwa ufafanuzi huu, na Mwenyezi Mungu (swt) ni ndiye Mjuzi zaidi na Mwingi wa Hekima.

Ndugu Yenu,

Ata Bin Khalil Abu Al-Rashta

16 Jumada al-Akhira 1442 H

29/01/2021 M

Link ya jibu hili kutoka ukurasa wa Amiri wa Facebook.

Andika maoni

Hakikisha umejaza (*) habari zinazohitajika palipoashiriwa. Kodi za HTML haziruhusiwi.

rudi juu

Vifungu vya Tovuti

Viunganishi

Magharibi

Ardhi za Waislamu

Ardhi za Waislamu