- |
- Kuwa wa kwanza kutoa maoni!
- ukubwa wa font punguza ukubwa wa font zidisha ukubwa wa font
بسم الله الرحمن الرحيم
Jibu la Swali
Matukio Mjini Al-Suwayda
(Imetafsiriwa)
Swali:
Axios iliripoti kwamba mkutano wa ngazi ya juu ulifanyika jijini Paris kati ya Waziri wa Mambo ya Kimikakati wa ‘Israel’ Ron Dermer na Waziri wa Mambo ya Nje Asaad Al-Shibani, uliopatanishwa na mjumbe maalum wa Marekani nchini Syria, Thomas Barak, mnamo 25/7/2025. Siku chache zilizopita tangu tarehe 12/7/2025 zimeshuhudia kuongezeka kwa machafuko katika Jimbo la Al-Suwayda [Sweida] kusini mwa Syria, ambalo wengi wa wakaazi wake ni Druze. Umbile la Kiyahudi limetangaza kuingilia kati masuala yao sambamba na kuendeleza uvamizi na mashambulizi yake nchini Syria. Lilishambulia pambizoni mwa kasri la rais, na kuishambulia Wizara ya Ulinzi na Majeshi jijini Damascus.
Kwa hiyo swali ni: Je, ni upi uhalisia wa yanayojiri mjini Al-Suwayda? Je, umbile la Kiyahudi linapanga nini kwa eneo la Suwayda na kusini mwa Syria kwa jumla, na je, Amerika inaunga mkono mipango yake? Na kuna uhusiano gani kati ya haya yote na mazungumzo ya uhalalishaji mahusiano kati ya serikali ya Syria na umbile la Kiyahudi, haswa mikutano iliyotokea nchini Azerbaijan? Na mikutano iliyokusudiwa jijini Paris? Mwenyezi Mungu awalipe mema.
Jibu:
Ili kufafanua majibu ya maswali ya hapo juu, tunahakiki mambo yafuatayo:
1- Kwa upande wa Druze, idadi yao nchini Syria inakadiriwa kuwa karibu 700,000, wanaoishi katika maeneo ya kusini mwa Syria, haswa katika Mkoa wa Al-Suwayda. Baadhi yao wanaishi Lebanon, wanaokadiriwa kuwa karibu 250,000, na sehemu nyengine, inayokadiriwa kuwa karibu 140,000, wanaishi kaskazini mwa Palestina na Milima ya Golan. Umbile la Kiyahudi limetoa uraia wake kwa wale wanaoishi katika maeneo yanayokaliwa, na baadhi yao wamejiunga na safu zake za jeshi. Hivyo, umbile la Kiyahudi linawatumia kama kisingizio cha kuingilia Syria. Limewachochea tangu mwisho wa Februari iliyopita huko Jaramana na Sahnaya karibu na mji mkuu, Damascus... na katika matukio ya hivi majuzi mjini Al-Suwayda yaliyozuka tangu tarehe 12 Julai 2025, umbile la Kiyahudi lilitangaza wazi kwamba linawaunga mkono Druze na linafanya kazi ya kuwatumia vibaya. Wanamgambo wa Druze walifanya vitendo vya unyanyasaji dhidi ya Waislamu Mabedui wanaoishi katika Jimbo la Al-Suwayda, na kuua mamia yao. Waziri Mkuu wa umbile la Kiyahudi, Netanyahu, alitangaza katika hotuba iliyotangazwa na televisheni ya Kiyahudi na vyombo vyengine vya habari mnamo tarehe 17/7/2025: “Tumeweka sera ya wazi, ya kuondoa nguvu za kijeshi eneo la kusini mwa Damascus, kutoka Milima ya Golan hadi milima ya Druze, ni mstari mmoja [mwekundu]. Mstari wa pili [ni] kulinda ... Druze katika mlima wa Druze.” Waziri wa vita wa umbile la Kiyahudi, Yisrael Katz, alituma vitisho kwa Syria kupitia jukwaa la X mnamo tarehe 16 Julai 2025, akisema, “Ishara kwa Damascus zimekwisha; sasa yanakuja mapigo uchungu. Jeshi litaendelea kufanya kazi kwa nguvu mjini Al-Suwayda kuharibu vikosi vilivyoshambulia Druze hadi kujiondoa kabisa.” Msemaji wa jeshi la Kiyahudi alisema kwenye jukwaa la X: “Jeshi linaendelea kushambulia maeneo ya kijeshi ya utawala wa Syria. Muda mfupi uliopita, lilishambulia makao makuu ya Jeshi la Syria katika eneo la Damascus.” Siku hiyo hiyo, Redio ya Jeshi la umbile la Kiyahudi ilitangaza: “Ilishambulia karibu shabaha 160 nchini Syria tangu jana usiku, nyingi zikiwa Al-Suwayda dhidi ya vikosi vya usalama vya Syria na Mabedui, na zengine katika mji mkuu Damascus.” Mashambulizi yalitangazwa kwenye kasri la rais, Wizara ya Ulinzi, na Jeshi jijini Damascus.
2- Kwa hivyo, umbile la Kiyahudi linatangaza wazi wazi malengo na sera yake na kwamba linawatumia Druze kutekeleza sera hii kuelekea Syria, kufanya mambo yao kuwa hamu kwake na sio kwa serikali ya Syria, kana kwamba linachonga eneo hili nje ya Syria na kuwa ndilo linalolidhibiti. Halikusimamisha mashambulizi yake nchini Syria wakati wa utawala wa Bashar Al-Assad, lakini halikuwa limewatumia Druze kama kisingizio cha hilo; bali, lilitumia uwepo wa Iran na wafuasi wake kama kisingizio. Lilishambulia vituo vingi vya kijeshi vya utawala na pia wa Iran, ambayo ilikuwa ikiunga mkono serikali na wanamgambo wake, na lilipua kwa mabomu ubalozi wake jijini Damascus na kuua viongozi wengi wa kijeshi wa Iran. Siku ambayo Bashar Al-Assad alikimbia mnamo tarehe 8/12/2024, umbile la Kiyahudi lilianzisha mashambulizi makali kwa siku kadhaa mfululizo na kushambulia mamia ya maeneo ya kijeshi ya Syria. Wakati halikupata jibu wala upinzani, lilizidi kuwa na tamaa kubwa na kuendelea na uvamizi wake hadi lilipovamia maeneo mapya ya Syria, likifika takriban kilomita 25 kutoka mji mkuu Damascus na kukalia kwa mabavu Mlima Hermon. Lilikiuka makubaliano ya 1974 ya kujiondoa na kusitisha mapigano. Umbile la Kiyahudi linataka kupata eneo la kusini mwa Syria kama eneo salama lisilo na nguvu za kijeshi, kwa kucheza kadi ya walio wachache, haswa Druze.
3- Kufuatia matukio hayo, Rais wa Syria Ahmad Al-Sharaa alitoa hotuba iliyotangazwa na televisheni ya Syria na idhaa nyenginezo za Kiarabu asubuhi ya tarehe 17/7/2025, ambapo alisema: (“Tulikuwa kati ya chaguo la vita na Israel au kuruhusu wazee wa Druze kufikia makubaliano, kwa hiyo tulichagua kulinda nchi.” Alisema: “Israel ilitaka kuhujumu usitishaji vita ‘mjini Al-Suwayda’ lau si kwa upatanishi wa Amerika, Waarabu na Waturuki.”) Alitoa hotuba ya pili mnamo tarehe 19/7/2025, kama ilivyoripotiwa na Shirika la Habari la Syria na kutangazwa na vituo vya televisheni, ambapo alisema: (“Nchi ya Syria iliweza kutuliza hali licha ya ugumu wa hali hiyo, lakini uingiliaji wa Israel uliiingiza nchi katika hatua ya hatari ambayo inatishia utulivu wake kutokana na mashambulizi ya wazi ya kusini na taasisi za serikali jijini Damascus. Natija ya matukio haya, upatanishi wa Amerika na Waarabu ulijaribu kutuliza hali.”) Anategemea uingiliaji kati wa nchi nyenginezo, ya kwanza kabisa miongoni mwao Amerika, ambayo inafadhili na kuunga mkono umbile la Kiyahudi, ili kuwapa udhibiti juu yake!
4- Kisha matukio yakazidi, na uhusiano kati ya Mayahudi na Hikmat al-Hijri ukaanza kudhihirika zaidi, huku akikaza mshiko wake kwenye sehemu ya ndani ya Al-Suwayda. Chini ya kauli mbiu kama vile “kuunganisha safu ndani ya dhehebu na kuzifariji familia za mashahidi,” alianza kuondoa sauti zisizomuunga mkono, kama zile za Jarbou, Al-Bala’ous, na Al-Hanawi. Na wakati kundi la Hikmat al-Hijri ndilo kubwa zaidi katika Al-Suwayda na linatawala makundi mengine, sauti za wapinzani kama Al-Jarbou’ na Al-Bala’ous zimekuwa za uoga katika wito wao wa kubaki ndani ya dola ya Syria, bila uzito halisi uwanjani. Ni Hikmat al-Hijri ambaye anazusha makabiliano na kughairi makubaliano yaliyofanywa na Damascus, na lake sasa linatawala Al-Suwayda. Anatoa kauli kwa jina la uongozi wa kiroho wa dhehebu la Druze, bila kujali mamlaka ya Al-Jarbou’ na Al-Hanawi. Ni wazi kwamba anawasiliana moja kwa moja na umbile la Kiyahudi, kwani alikuwa ametuma wageni kadhaa wa Druze kwenye umbile hilo. Hikmat al-Hijri alitoa taarifa kwa jina la uongozi wa kiroho wa Druze akisema: (“Tunaomba ulimwengu huru na mamlaka yote yenye ushawishi ndani yake, na tunaelekeza wito wetu kwa Mheshimiwa Rais (wa Amerika) Donald Trump, na Waziri Mkuu (wa Israel) Benjamin Netanyahu, na Mrithi wa Kifalme (wa Saudia) Mwanamfalme Mohammed bin Salman, na Mtukufu Mfalme Abdullah II, na kwa kila mtu aliye na sauti na ushawishi duniani kote ... Iokoeni Al-Suwayda.” (Shirika la Anadolu, 17/7/2025). Umbile la Kiyahudi lilifungua milango yake ya mpaka na Druze ndani ya umbile hilo ili kujiunga na mapigano ndani ya Syria. RT iliripoti mnamo tarehe 19/7/2025 kwamba watu wapatao 2,000 kutoka dhehebu la Druze, wakiwemo wanajeshi wanaohudumu katika jeshi la Kiyahudi, walitangaza nia yao ya kujiunga na vita nchini Syria katika siku moja tu.
5- Inafaa kuashiria kuwa serikali ya Damascus imejifanya kuwa kiungo dhaifu zaidi katika mlolongo wa matukio yanayoizunguka Al-Suwayda na kusini mwa Syria. Mbali na kuridhika na udhaifu wake mbele ya mashambulizi yote ya kijeshi yaliyofanywa na umbile la Kiyahudi dhidi yake na mashambulizi ya vikosi vyake yaliyofika kusini mwa Syria kwa mauaji na kukamata watu kana kwamba hakukuwa na serikali hata kidogo kutokuwepo kwa majibu ya serikali kunatokana na ushauri wa Erdogan, ambaye alitangaza kuunga mkono ombi la rais wa Marekani la Damascus kujiunga na Mkataba wa Abraham 26/7/20). Erdogan aliwezesha mawasiliano kati ya serikali ya Shar’a na umbile la Kiyahudi nchini Azerbaijan. Hivyo, serikali ya Ahmad Al-Shar’a ikawa tete sana katika mgogoro wa Al-Suwayda. Iliingilia kati ili kusitisha mapigano katika eneo hilo na ikaondoka kwa unyonge chini ya shambulizi la bomu la umbile la Kiyahudi, ambalo lililenga Wanajeshi Wakuu na kukaribia kufika kasri la rais. Kisha upatanishi wa Marekani na wale walioitwa Waarabu na Uturuki waliingilia kati kurudisha vikosi vya usalama lakini safari hii kutoka kwa Wizara ya Mambo ya Ndani, sio jeshi, na kwa silaha nyepesi. Baadaye ilidhihirika kuwa majeshi haya ya serikali hayakuwahi kuingia Al-Suwayda hata kidogo; bali dhamira yao ilikuwa ni kuzuia makabila ya Waarabu wasiendelee na mashambulizi yao dhidi ya Al-Suwayda. Yaani walisimama viungani mwa mkoa huo pasi na kuingia humo. Kwa hakika, umbile la Kiyahudi lilikuwa limetaka hivyo, kwamba wazuie makabila yasiwashambulie Al-Suwayda. Katika kila makubaliano, muasi Hikmat al-Hijri ndiye anayeyavunja na kudai masharti mapya, na kuilazimisha serikali kuandaa makubaliano mengine mapya, na ya hivi karibuni yakiwa ya nne ndani ya wiki moja. Serikali ya Ahmad Al-Sharaa, kwa njia ya mazungumzo, iliwaondoa wapiganaji wa kikabila kutoka ndani ya Al-Suwayda bila ya kuingia humo na kisha kuanza kuyaondoa makabila yaliyokuwa yakiishi Al-Suwayda. Iliondoa na kuhamisha mamia ya familia za Kiislamu kutoka Al-Suwayda hadi kwenye makaazi huko Daraa. Hiki ni kitu ambacho Hikmat al-Hijri pia anafanya. “Mapigano yalianza tena siku ya Ijumaa baada ya kundi lenye mafungamano na Hikmat al-Hijri, mmoja wa viongozi wa Druze, kuwafukuza kwa nguvu baadhi ya watu wa kabila Kibedui la Sunni na kufanya ukiukaji dhidi yao.” (Shirika la Anadolu, 21/7/2025). Kwa hivyo, serikali mpya ya Syria imethibitisha kivitendo kwamba inakubali kutawala Syria kulingana na kile Amerika inachoamuru, huku njia yake ilkiwa imechorwa na balozi wa Amerika nchini Uturuki na mjumbe wake nchini Syria, Tom Barak!
6- Baada ya kutafakari matukio nchini Syria, inabainika kuwa Marekani inayasimamia kwa mujibu wa mpango ambao haukuanza leo, ingawa uliongezeka baada ya kuwasili kwa Trump.
(Rais wa Marekani Donald Trump alitoa wito kwa Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu wakati wa mkutano wao katika Ikulu ya White House, “suluhisha matatizo yake" pamoja na Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan “na chukua hatua kwa busara.” Trump alisema katika maoni yake kwa waandishi wa habari wakati wa mkutano wake na Netanyahu: “Nina uhusiano mkubwa na mtu anayeitwa Erdogan. Ninampenda, na ananipenda na hicho ndicho kinachovikasirisha vyombo vya habari.” Alieleza kuwa alimwambia Netanyahu “anampenda Erdogan,” na ikiwa ana matatizo naye, anapaswa kuyatatua, akisisitiza: “Waisraeli wanapaswa kuchukua hatua kwa busara kutatua masuala yoyote na Uturuki.” (Al Jazeera, 8/4/2025) “Kisha (Trump alikutana mnamo Jumatano jijini Riyadh na rasi wa mpito wa Syria Ahmad Al-Sharaa katika mkutano wa kwanza wa kipekee katika kipindi cha miaka 25, siku moja baada ya kutangaza uamuzi wake wa kuondoa vikwazo kwa Damascus hatua iliyokaribishwa na Syria kama “nukta muhimu ya mabadiliko.” Msemaji mmoja wa Ikulu ya White House alisema kuwa Trump alimtaka rais wa Syria kutia saini Mkataba wa Abraham na 'Israel' (France 24, 14/5/2025).
Kupitia mkutano huu na kuondolewa kwa vikwazo dhidi ya Syria, na ombi lake kwamba Netanyahu aratibu shughuli zake nchini Syria na Uturuki, Rais Trump na utawala wake wanafanya kazi ya kuitawala Syria.
7- Kwa hivyo, ni wazi kwamba mpango wa Marekani nchini Syria umejengwa juu ya msingi wa fikra ya: kumbadilisha kibaraka mmoja kwa mwengine. Kwa ajili hiyo, Uturuki ilipewa idhini kuusambaratisha utawala wa Bashar na kujenga utawala mpya mtiifu kwake. Licha ya kauli zote za utiifu kutoka kwa rais mpya wa Syria, Ahmad Al-Sharaa, zikionyesha kukubali kwake kuchukua nafasi hii—kama vile kuachana na hukmu ya Uislamu, kuachana na kuwashtaki wafuasi wa Bashar, na kubadilisha hayo kwa maridhiano ya kitaifa, hata alifikia hatua ya kufungua mazungumzo na umbile la Kiyahudi nyuma ya pazia. Kisha nchini Azerbaijan mnamo 12/7/2025, wazi wazi juu ya pazia, na baadaye katika mikutano ya Paris: Axios iliripoti kwamba mkutano wa ngazi ya juu ulifanyika jijini Paris kati ya Waziri wa Mambo ya Kimikakati wa ‘Israel’ Ron Dermer na Waziri wa Mambo ya Nje wa Syria Assad Al-Sheibani, aliyepatanishwa na mjumbe maalum wa Marekani nchini Syria Tom Barrak. Mazungumzo haya yaliyochukua takriban masaa manne, ni ya kwanza ya aina yake kati ya nchi hizo mbili katika kipindi cha miaka 25. Ililenga katika kupunguza mvutano kusini mwa Syria, kuweka usalama, na kusitishwa kwa mapigano. Shirika la Uangalizi wa Haki za Kibinadamu la Syria lilifichua kwamba makubaliano yalifikiwa kati ya Syria na "Israel," yaliyopatanishwa na Marekani, yenye vifungu saba vikuu vinavyohusiana na usitishaji vita kusini, hasa katika Al-Suwayda, ambayo imeshuhudia ongezeko kubwa tangu Julai 12. Kulingana na Shirika hilo, makubaliano hayo yanabainisha kuhamishwa kwa faili lote la Al-Suwayda kwa utawala wa Marekani. Makubaliano hayo pia yanaainisha kuunda mabaraza ya mitaa kutoka kwa wakaazi wa Al-Suwayda kutoa huduma, kuunda kamati ya kunakili ukiukaji ambayo inaripoti moja kwa moja upande wa Amerika, kupokonya silaha mikoa ya Daraa na Quneitra, na kuunda kamati za usalama za mitaa huko bila kuruhusu umiliki wa silaha nzito. (Axios / Ain Libya, 25/7/2025). Haya yote yanathibitisha kwamba Marekani inataka eneo la kusini mwa Syria liwe eneo la usalama (buffer) kwa umbile la Kiyahudi, na kwamba imeridhika na uvamizi wake wa mara kwa mara ili kuulazimisha utawala huo kukubali hali hii kwa ajili ya kuhalalisha mahusiano. Mikutano ya Azerbaijan na Paris ni hatua mtawalia kwenye njia hii. Kwa mujibu wa uvujaji wa habari, jambo muhimu zaidi linalojadiliwa ni: kuanzisha eneo la usalama kusini mwa Syria kwa manufaa ya umbile la Kiyahudi, sawa na lile la Sinai kati ya Misri na umbile la Kiyahudi chini ya mkataba wa amani uliotiwa saini na utawala wa Misri mwaka 1979, ambao bado unawazuia watu wa Misri kusonga kuwanusuru ndugu zao huko Gaza, ambao wanakabiliwa na mauaji ya halaiki.
8- Hatimaye, inatia uchungu kwa hakika kwamba Syria Ash-Sham aliyoisema Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) katika Hadith yake tukufu iliyopokelewa na al-Tabarani... kutoka kwa Salamah bin Nufayl ambaye amesema: Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) amesema: «عُقْرُ دَارِ الإِسْلامِ بِالشَّامِ» “Kitovu cha Uislamu kitakuwa Ash-Sham” hivi sasa imekuwa chini ya serikali inayotawala mbali na Uislamu, na mtawala wake anajitupa katika utiifu kwa Marekani na kujisalimisha kwa umbile la Kiyahudi bila ya kupigana nalo, lakini badala yake anataka kutia saini makubaliano ya amani nalo na kufanya yale yanayolifurahisha umbile hili na mtetezi wake, Marekani.
Aliwaacha hata wanachama wa Hizb ut Tahrir wale wanaolingania Khilafah Rashida gerezani na hakuwaachilia huru, ili kuiridhisha Marekani na Mayahudi ambao ni maadui wa Khilafah na watu wake, akijidanganya kwamba kuwaridhisha maadui wa Mwenyezi Mungu kutahifadhi utawala wake! Amesahau au anajifanya kusahau kauli ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) iliyopokelewa na Ibn Hibban katika Sahih yake kutoka kwa Urwah, kutoka kwa Aisha (ra), amesema: Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) amesema:
«مَنِ الْتَمَسَ رِضَا اللهِ بِسَخَطِ النَّاسِ رَضِيَ اللهُ عَنْهُ، وَأَرْضَى النَّاسَ عَنْهُ، وَمَنِ الْتَمَسَ رِضَا النَّاسِ بِسَخَطِ اللهِ سَخَطَ اللهُ عَلَيْهِ، وَأَسْخَطَ عَلَيْهِ النَّاسَ»
“Mwenye kutaka radhi za Mwenyezi Mungu kwa gharama ya ghadhabu za watu, basi Mwenyezi Mungu atakuwa radhi naye na kuwaridhisha watu, na anayetaka radhi za watu kwa ghadhabu ya Mwenyezi Mungu, basi Mwenyezi Mungu atamghadhibikia na atawafanya watu wamghadhibikie.” Vile vile imepokewa na al-Tirmidhi katika Sunan yake kwa maneno haya: «مَنْ الْتَمَسَ رِضَا اللهِ بِسَخَطِ النَّاسِ كَفَاهُ اللهُ مُؤْنَةَ النَّاسِ وَمَنْ الْتَمَسَ رِضَا النَّاسِ بِسَخَطِ اللهِ وَكَلَهُ اللهُ إِلَى النَّاسِ» “Mwenye kutaka radhi za Mwenyezi Mungu na hali watu wanachukizwa, Mwenyezi Mungu humtosheleza kwa watu, na anayetaka radhi za watu na hali Mwenyezi Mungu anachukizwa, Mwenyezi Mungu atamkabidhi kwa watu.”
Vyovyote iwavyo, tunahakikishiwa kwamba Khilafah itaregea baada ya utawala huu dhalimu tunaoishi ndani yake: Ahmad amesimulia katika Musnad yake kutoka kwa Hudhayfah ambaye amesema: Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) amesema:
«... ثُمَّ تَكُونُ مُلْكاً جَبْرِيَّةً فَتَكُونُ مَا شَاءَ اللهُ أَنْ تَكُونَ، ثُمَّ يَرْفَعُهَا إِذَا شَاءَ أَنْ يَرْفَعَهَا، ثُمَّ تَكُونُ خِلَافَةً عَلَى مِنْهَاجِ النُّبُوَّةِ. ثُمَّ سَكَتَ»
“Kisha utakuwepo ufalme wa kiimla, na utabakia kadri Mwenyezi Mungu atakavyo, kisha atauondoa apendapo kuuondoa, kisha itakuwepo Khilafah kwa njia ya Utume.” Kisha akanyamaza. Imeripotiwa pia na al-Tayalisi katika Musnad yake. Wakati huo, Uislamu na Waislamu watakuwa na izza, na ukafiri na makafiri watadhalilika. Na wape bashara njema Waumini:
[وَأُخْرَى تُحِبُّونَهَا نَصْرٌ مِنَ اللهِ وَفَتْحٌ قَرِيبٌ وَبَشِّرِ الْمُؤْمِنِينَ]
“Na kinginecho mkipendacho, nacho ni nusura itokayo kwa Mwenyezi Mungu, na ushindi ulio karibu! Na wabashirieni Waumini!” [Surah As-Saff:13].
1 Safar 1447 H
26/7/2025 M