- |
- Kuwa wa kwanza kutoa maoni!
- ukubwa wa font punguza ukubwa wa font zidisha ukubwa wa font
بسم الله الرحمن الرحيم
Uislamu uko Mbali na Mazungumzo ya Dini Mseto
(Imetafsiriwa)
Habari:
Mnamo tarehe 5 Julai 2025, jumba jipya la ibada katika Kanisa la Arise and Shine Tanzania lililopo Kawe, viungani mwa jiji la Dar es Salaam lilizinduliwa.
Kanisa hilo linaongozwa na Mwinjilisti na anayejiita ‘mtume’ Boniface Mwamposa ambaye mahubiri yake mwaka 2020 yalileta msiba wa vifo vya waumini zaidi ya 20 kutokana na mkanyagano waliokuwa wakikimbia kupakwa mafuta yenye baraka.
Maoni:
Sherehe za uzinduzi huo zilitumika kuimarisha maadili ya kidemokrasia na kisekula kwa kusisitizwa na Rais Samia kuhusu umuhimu wa kudumisha mshikamano wa kitaifa na kuwataka Watanzania kulinda amani na umoja wa muda mrefu nchini wakati taifa linapojiandaa kwa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025.
Fauka ya hayo, hafla kama hiyo ilitumika kuunganisha ajenda hatari sana ya imani mseto kufikia kiwango ambacho vitendo kadhaa vinavyowakilisha kampeni hiyo ya kishetani vilitekelezwa na kusisitizwa mno.
Ilishuhudiwa wakati wa hafla hiyo kuwa baadhi ya viongozi wa Waislamu, wanasiasa wenye asili ya Kiislamu pamoja na Waislamu wa kawaida wakifanya maombi pamoja na wasiokuwa Waislamu ndani ya kanisa hilo, baadhi yao hata wakitoa kauli kinyume na mafundisho na fikra za Kiislamu.
Uzinduzi huo ulicheza dori kubwa na ulitumika sana kama jukwaa la kuhubiri na kulingania mazungumzo ya dini mseto kati ya Uislamu na Ukristo kwa jina la mshikamano wa kijamii au kidini nchini.
Baada ya kufeli kwa Wamagharibi kuwatenga Waislamu na imani (itikadi) yao kupitia wamishenari, orientalisti, kazi za kithaqafa, vyombo vya habari, udanganyifu wa kifikra na wa kisiasa, walitumia njia za mazungumzo ya dini mseto ambayo yalianzishwa rasmi mwaka 1932 na Ufaransa kupitia kutuma ujumbe wake katika Chuo Kikuu cha Azhar.
Lengo lao kuu la kampeni ya mazungumzo ya dini mseto ambayo inasukumwa na dola za kibepari ni kuzuia Uislamu kurudi katika mambo ya maisha kama mfumo mpana. Kwani Uislamu unatishia uhai wa mfumo wao na hadhara yao ya kibepari na kuangamiza maslahi na ushawishi wao.
Kupitia mazungumzo ya dini mseto, mabepari wa Magharibi wanafanya kazi ya kuondoa thaqafa ya Kiislamu katika akili za Waislamu. Wanalenga kufikia hilo kwa kuhujumu imani ya Waislamu kwa thaqafa yao, machimbuko na kanuni zake.
Pia, kampeni hiyo ilimaanisha kuzimua na kudhoofisha mafundisho ya Kiislamu ya nguvu zake za kimaumbile katika kupingana na fahamu za hadhara zisizo za Kiislamu. Bila kutaja njama ya kimagharibi ya kuuvua sifa zake muhimu zaidi zinazoutofautisha na dini nyenginezo, nazo ni za kijamii, kiuchumi na muhimu zaidi nyanja ya kisiasa ambayo kwayo Khilafah ndiyo dola yake.
Waislamu nchini Tanzania na kwengineko wanapaswa kuwa waangalifu na ajenda hii ovu ya kimataifa inayoendelea ya mazungumzo baina ya dini mseto, kwa upande wa fikra na vitendo.
Ijapokuwa Uislamu unaruhusu ushirikiano wa kisheria na wasiokuwa Waislamu, lakini hiyo haipanuki hadi kwenye mshikamano wa kidini, na unakataza kabisa ushiriki wowote katika matendo yoyote ya ibada ya dini nyengine. Dini pekee ya haki ni Uislamu, ambayo Waislamu wanapaswa kujishughulisha katika dawah ili kanuni zake zote zitabikishwe chini ya dola yake ya Khilafah.
Imeandikwa kwa Ajili ya Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir na
Said Bitomwa
Mwanachama wa Afisi ya Habari ya Hizb ut Tahrir Tanzania