- |
- Kuwa wa kwanza kutoa maoni!
- ukubwa wa font punguza ukubwa wa font zidisha ukubwa wa font
بسم الله الرحمن الرحيم
Yaonekana Mazuri, lakini Ndani Hamna Kitu!
(Imetafsiriwa)
Habari:
Rais Erdoğan, katika hotuba yake baada ya mkutano wa baraza la mawaziri, pia aligusia mwelekeo wa Uturuki wa sera ya kigeni, akisema: “Uturuki imeipa dunia funzo katika haki za binadamu kupitia juhudi zake zinazolenga amani na haki katika maeneo yaliyolowa damu na machozi—Gaza, Syria, Somalia, na Libya.” Alisisitiza kwamba taifa hilo limeunganishwa kwa fungamano lisilotikisika, pasi na tofauti kati ya Mturuki, Mkurdi, Muarabu, Alevi, au Caucassian. (Mashirika, 15.12.2025)
Maoni:
Inasemekana kwamba wasomi walipowaona watu ambao tabia zao hazikufikia maana ya majina yao—ambao walitenda kinyume chake—waliwashauri wabadilishe majina yao au wabadilishe akhlaki zao. Labda leo, huu ni msemo ambao aghlabu unahitaji kuhutubiwa wale wanaotutawala. Kwa sababu kwa karne moja, Ummah umedanganywa na watawala wake na kwa bahati mbaya umesalitiwa. Ufahamu wa kuelekeza umma kwa maneno yenye kutuliza hisia na watawala wanaoona siasa kama sanaa ya kubaki madarakani sasa umekuwa wa kawaida. Kutoynganisha kati ya maneno na matendo yao kumekuwa kawaida. Kama tafakari ya fikra hii, watawala—ambao hawaachi fursa yoyote—wanajaza ufahamu wa umma kwa jumbe wanazotaka kuwasilisha. Hotuba ya hivi karibuni ya Rais Erdoğan iko katika mkondo huu pia: “Uturuki imeupa ulimwengu funzo katika haki za binadamu kupitia juhudi zake zinazolenga amani na haki katika maeneo yaliyolowa damu na machozi—Gaza, Syria, Somalia, na Libya.”
Maneno kama amani, haki, uadilifu, haki za binadamu, na “kutoa funzo” yanaweza kusikika kikamilifu na ya kupendeza masikioni, lakini kila mtu anajua kiwango ambacho yanatekelezwa katika sera za kigeni. Tazama: kwa miaka miwili, mauaji ya kinyama na mauaji ya halaiki zaidi katika historia ya binadamu yamefanywa Gaza, na bado yanaendelea. Nchi ambazo, chini ya jina la “amani,” huvaa barakoa ya “mdhamini” hubaki kimya na kutotoa jibu licha ya ukiukaji na mauaji ya halaiki. Ingawa ni sehemu ndogo tu ya misaada inayopaswa kuingia Gaza huifikia, wale wanaotutawala hubaki watulivu kana kwamba hakuna kinachotokea—lakini wanazungumzia amani na usawa! Maadamu mnaendelea na mahusiano na kulitambua Umbile la Kiyahudi na kuyaelekea mauaji haya na ukatili wa kimfumo wa njaa sio kwa majeshi bali kwa sanamu ya siasa halisi, mnajidanganya wenyewe. Ingawa katika nchi ulizoorodhesha sio tu kwamba machozi yanamwagika lakini damu inatiririka kwa mito kuzama ardhini, wewe unashiriki katika muundo mpya wa kisiasa katika maeneo haya pamoja na mshirika wa kimkakati, Marekani—bila shaka, muundo mpya uliofanywa kwa kuzingatia maslahi ya Marekani, kwa badali ya kile kinachoitwa “uhalali” uliopewa...
Lakini Marekani—ambayo inalipa Umbile la Kiyahudi usaidizi mkubwa zaidi katika silaha, pesa, ujasusi, vyombo vya habari, na siasa—inaunga mkono uvamizi wa Gaza na ardhi za Palestina. Ingawa wanatekeleza vitendo hivi, na wewe unadumisha uhusiano wa kisiasa, kijeshi, na kiuchumi nao, ni aina gani ya “funzo katika ubinadamu” unalotoa?
Wakati Umbile la Kiyahudi halifuati hata makubaliano yanayoitwa ya kusitisha mapigano, linaua Waislamu wengi kila siku, linageuza Ukingo wa Magharibi kuwa gereza la wazi, na linapanua uvamizi siku baada ya siku—kwa kukaa kimya dhidi ya uhalifu huu—unawezaje kuchangia kuzuia machozi ya mtu yeyote?
Nchini Syria, kuanzia kwenye mpaka wetu, chini ya mipango ya Marekani iliyoundwa kutoka masafa ya maelfu ya kilomita ili kuunda upya eneo hilo, umechukua jukumu la “kutoa nidhamu” kwa mfumo na kada inayotawala—kwanza kabisa utawala wa Syria—ili kuoanishwa katika Magharibi. Ungewezaje kuanzisha haki yoyote katika hali kama hiyo?
Kwa kuwa ndani ya mashirika kama NATO na Umoja wa Mataifa yanayofanya haya yote na zaidi, na kwa kutenda kama setilaiti sambamba na siasa za Marekani, kuna “funzo” lolote linatolewaje kwa ulimwengu? Tunashangaa kweli. Maneno haya mazuri yanaweza kuwa kama nyumba inayoonekana nzuri kutoka nje na ya kupendeza—lakini kwa sababu hakuna matendo yanayofanywa, ndani yake kumeharibika na patupu.
Dua yetu kwa Mola wetu Mlezi ni kwamba atupe sisi makhalifa ambao matendo yao yana nguvu kuliko maneno yao; ambao huchukua kama msingi wao sio mipaka iliyochorwa na makafiri bali mipaka iliyochorwa na Mwenyezi Mungu (swt); na ambao hupa kipaumbele si siasa halisi bali maslahi ya Umma.
Imeandikwa kwa Ajili ya Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir na
Ahmet SAPA



