Jumanne, 07 Rabi' al-awwal 1446 | 2024/09/10
Saa hii ni: (M.M.T)
Menu
Main menu
Main menu

بسم الله الرحمن الرحيم

 Silsila ya Majibu ya Mwanachuoni Mkubwa Ata Bin Khalil Abu Al-Rashtah Amiri wa Hizb ut Tahrir "Juu ya Maswali ya Wanaozuru Ukurasa Wake wa Facebook wa "Kifiqhi"

Jibu la Swali

Chanjo Dhidi ya Maradhi ya Korona.

Kwa: Ummu Bilal

(Imetafsiriwa)

Swali:

Assalamu Alaikum wa Rahmatullahi wa Barakatuh

Mwenyezi Mungu akubariki ewe Amiri wetu, na awape ushindi, na awatilie nguvu kwa ufunguzi wa wazi na Khilafah kwa njia ya Utume nyoyo za waumini ziweze kupoa.

Swali langu ni kuhusiana na chanjo mpya ambazo serikali zimeanza kuwapa raia wao dhidi ya ugonjwa wa korona... twawaona watu wengi wana hofu ya kupewa hizi chanjo, kutokana na watu wengi kueneza maneno mengi kupitia mitandao ya kijamii kuhusu hatari ya hizi chanjo. Na kwamba eti ni njama za kiulimwengu wa mabepari dhidi ya mataifa... twajua kwamba, uponyaji upo mikononi mwa Mwenyezi Mungu, na kwamba kila kitu kina mda wake ulioandikwa, na sisi kama wabebaji wa ulinganizi twaulizwa kuhusu uhakika wa chanjo hizi. Na je, ni wajib kisheria kuchukua chanjo katika hali hii ya kuenea kwa hili janga?

Mwenyezi Mungu awabariki.

Jibu:

Wa Alaikum Salam wa Rahmatullahi wa Barakatuh.

Kama unavyojua tulishawahi kutoa majibu kuhusiana na maswali yanayohusu kujitibu. Na tukasema kwenye hayo majibu kwamba:

- Dawa ikiwa ndani yake kuna madhara basi ni haramu. Kutokana na hadith isemayo:

«لا ضرر ولا ضرار»

 “Hakuna kujidhuru, wala kuwadhuru wengine”

- Ama dawa ikiwa haina madhara lakini ndani yake kuna vitu vya haramu au najisi basi hukmu yake itakuwa ni Makruh. Yaani: sio haramu, bali yaruhusiwa kuitumia ila ni Makruh ikiwa mgonjwa hatopata dawa nyengine iliyo Mubaah.

Nitanukuu kutoka kwenye hayo majibu sehemu zinazohusiana na swali lako:

[ kwanza: Jibu la Swali 26/1/2011 M kuhusu “kunufaika na kilicho haramu na najisi na kujitibu nacho” ndani yake kulikuwa na haya:

(... 3- suala la kujitibu linavuliwa kutoka kwenye uharamu. Hivyo, si haramu kujitibu kwa kilicho najisi na haramu.

- Ama dalili ya kuwa kujitibu na kilicho haramu sio haramu, ni hadith ya Muslim kutoka kwa Anas (r.a):

«رَخَّصَ رَسُولُ اللَّهِ ﷺأَوْ رُخِّصَ لِلزُّبَيْرِ بْنِ الْعَوَّامِ وَعَبْدِ الرَّحْمَنِ بْنِ عَوْفٍ فِي لُبْسِ الْحَرِيرِ لِحِكَّةٍ كَانَتْ بِهِمَا»

 “Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) alimruhusu Zubair ibn Awwaam na Abdurahman bin Awf kuvaa hariri kwa sababu ya ugonjwa wa kujikuna waliokuwa nao”. Wanaume kuvaa hariri ni haram lakini waliruhusiwa kwa matibabu...

- Ama dalili ya kwamba kujitibu kwa kilicho najisi sio haramu, ni kwa hadith ya Bukhari kutoka kwa Anas (r.a):

«أَنَّ نَاساً اجْتَوَوْا فِي الْمَدِينَةِ فَأَمَرَهُمْ النَّبِيُّ ﷺ أَنْ يَلْحَقُوا بِرَاعِيهِ يَعْنِي الْإِبِلَ فَيَشْرَبُوا مِنْ أَلْبَانِهَا وَأَبْوَالِهَا فَلَحِقُوا بِرَاعِيهِ فَشَرِبُوا مِنْ أَلْبَانِهَا وَأَبْوَالِهَا...».

“Kwamba kuna watu waliugua (kutokana na hali ya anga ya madina) Mtume (saw) akawaamrisha waende kukutana na mchungaji wake wa ngamia na wanywe maziwa yake na mikojo yake. wakakutana naye na wakanywa maziwa ya ngamia na mikojo yake....”. Maana ya neno “ijtawaw”: vyakula vya madina havikukubaliana nao kwa hiyo wakawa wagonjwa”. Na Mtume (saw) akawaruhusu kujitibu kwa “mikojo” nayo ni najisi...] mwisho wa nukuu.

Pili: imekuja katika jibu suali 19/9/2013 M:

[ ... na jibu ni kwamba, kutumia kilevi kwenye dawa, na vilevile dawa zinazotiwa pombe... hukmu yake ni: kufaa pamoja na karaha. Na dalili ya hilo:

Amepokea ibn Maajah kupitia njia ya Twariq bin Suwaid Al-Hadhrami akisema:

«قُلْتُ يَا رَسُولَ اللَّهِ إِنَّ بِأَرْضِنَا أَعْنَاباً نَعْتَصِرُهَا فَنَشْرَبُ مِنْهَا قَالَ لَا فَرَاجَعْتُهُ قُلْتُ إِنَّا نَسْتَشْفِي بِهِ لِلْمَرِيضِ قَالَ إِنَّ ذَلِكَ لَيْسَ بِشِفَاءٍ وَلَكِنَّهُ دَاءٌ»

“Nilisema ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, katika ardhi zetu kuna mizabibu, tunaikamua na kunywa (na kulewa). akasema: hapana. Nikasisitiza na kusema: hakika sisi pia twawatibu nayo wagonjwa. akasema: kwa hakika, hiyo sio tiba bali ni ugonjwa”. Hili ni katazo la kutotumia najisi au kilicho haramu “pombe” kujitibu. Lakini Mtume (saw) aliruhusu kujitibu kwa najisi “mikojo ya ngamia”. Amepokea Bukhari kutoka kwa anas (r.a):

«أَنَّ نَاساً مِنْ عُرَيْنَةَ اجْتَوَوْا الْمَدِينَةَ فَرَخَّصَ لَهُمْ رَسُولُ اللَّهِ ﷺ أَنْ يَأْتُوا إِبِلَ الصَّدَقَةِ فَيَشْرَبُوا مِنْ أَلْبَانِهَا وَأَبْوَالِهَا...»

“Kwamba, watu kutoka katika kabila la Uraina waliugua kutokana na hali ya anga ya Madina, Mtume (saw) akawaruhusu waende palipo ngamia wa zaka na wanywe maziwa na mikojo yake....” neno “ijtawaw” yaani: hali ya hewa ya madina haikulingana nao, wakaugua. Mtume (saw) akawaruhusu wajitibu kwa mikojo ya ngamia, nayo ni najisi.

Pia Mtume (saw) aliruhusu kujitibu kwa kilicho haramu “kuvaa hariri”. Amepokea Tirmidhi na Ahmad - na matamshi ni ya Tirmidhi - kwa njia ya Anas:

«أَنَّ عَبْدَ الرَّحْمَنِ بْنَ عَوْفٍ وَالزُّبَيْرَ بْنَ الْعَوَّامِ شَكَيَا الْقَمْلَ إِلَى النَّبِيِّ ﷺ فِي غَزَاةٍ لَهُمَا، فَرَخَّصَ لَهُمَا فِي قُمُصِ الْحَرِيرِ. قَالَ: وَرَأَيْتُهُ عَلَيْهِمَا»

“Kwamba, Abdurahman bin Awf na Zubair ibn Awwaam walimshitakia Mtume (saw) kusumbuliwa na chawa walipokua katika vita, basi Mtume (saw) akawaruhusu kuvaa nguo za hariri. Asema (mpokezi): na niliwaona wakizivaa”. Hadith hizi mbili ni vidokezi kwamba lile katazo katika hadith ya ibn Maajah halikuwa katazo la kukata, yaani: kujitibu kwa najisi na kilicho haramu ni Makruh.]

Tatu: jibu la suali 18/11/2013 M kuhusu chanjo na hukmu yake... na ndani yake kulikuja:

[ Chanjo ni dawa, na kujitibu ni Mandub (jambo linalopendekezwa) wala si faradhi. Na dalili ya hilo:

1. Amepokea Bukhari kwa njia ya Abu Huraira akisema: amesema Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw):

«ما أنزل الله داء إلا أنزل له شفاء»

“Mwenyezi Mungu hateremshi maradhi isipokuwa huteremshi na tiba yake”

Na Muslim amepokea kutoka kwa Jaabir bin Abdillah, kutoka kwa Mtume (saw) kuwa amesema:

«لكل داء دواء فإذا أصيب دواء الداء برأ بإذن الله عز وجل»

“Kila ugonjwa una dawa yake. Kwa hiyo, ikipatikana dawa ya ugonjwa basi utapoa kwa idhni ya Mwenyezi Mungu Azza wa Jalla”

Na amepokea Ahmad katika Musnad yake kutoka kwa Abdullah bin Mas`ud:

«ما أنزل الله داء إلا قد أنزل له شفاء، علمه من علمه وجهله من جهل»

“Mwenyezi Mungu hajateremsha maradhi isipokuwa kwa hakika ameteremsha na tiba yake. Huijua wanaoijua, na wasioijua hawaijui”

Ndani ya hadith hizi kuna muongozo wa kwamba, kila ugonjwa una dawa yake ya kuiponya. Ili hilo liwe msukumo wa kwenda mbio kupata tiba itakayopelekea ponyo kwa idhini ya Mwenyezi Mungu (swt). Na huo ni muongozo wala sio kulazimisha.

2. Amepokea Ahmad kutoka kwa Anas akisema: hakika Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) amesema:

«إِنَّ اللَّهَ حَيْثُ خَلَقَ الدَّاءَ، خَلَقَ الدَّوَاءَ، فَتَدَاوَوْا»

“Hakika Mwenyezi Mungu pindi alipoumba maradhi pia aliumba na dawa, kwa hiyo jitibuni”

Na amepokea Abu Dawud  kutoka kwa Usama bin Sharik akisema:

أَتَيْتُ النَّبِيَّ ﷺ وَأَصْحَابَهُ كَأَنَّمَا عَلَى رُءُوسِهِمُ الطَّيْرُ، فَسَلَّمْتُ ثُمَّ قَعَدْتُ، فَجَاءَ الْأَعْرَابُ مِنْ هَا هُنَا وَهَا هُنَا، فَقَالُوا: يَا رَسُولَ اللَّهِ، أَنَتَدَاوَى؟ فَقَالَ: «تَدَاوَوْا فَإِنَّ اللَّهَ عَزَّ وَجَلَّ لَمْ يَضَعْ دَاءً إِلَّا وَضَعَ لَهُ دَوَاءً، غَيْرَ دَاءٍ وَاحِدٍ الْهَرَمُ» أي "إلا الموت".

“Nilimuendea Mtume (saw) hali ya kuwa maswahaba wake (wametulia) kana kwamba kuna ndege juu ya vichwa vyao. nikasalimia, kisha nikakaa. Wakaja mabedui kutoka huku na kule, wakasema:  Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu je tujitibu? Akasema: “Jitibuni, kwani Mwenyezi Mungu Azza wa Jalla haweki maradhi isipokuwa huyawekea na tiba pia, ila tu ugonjwa mmoja 'Al-Haram' (kifo)”. Yaani isipokuwa kifo.

Katika hadith ya kwanza kuna amri ya kujitibu, na katika hadith hii kuna jibu kwa mabedui kuwa wajitibu, na ni kuwazungumzia waja wajitibu, kwani Mwenyezi Mungu haweki maradhi isipokuwa huyawekea na tiba pia. Bila shaka, mazungumzo katika hizo hadith mbili yamekuja kwa tamshi la amri, na amri hujulisha kutakwa jambo fulani moja kwa moja wala haijulishi ulazima wa jambo isipokuwa ikiwa ni amri ya kukata. na “kukata” kunahitajia Qarina (kidokezi) inayojulisha. Na katika hadith hizi mbili hakuna Qarina yoyote inayojulisha ulazima. Ukiongezea kwamba, kuna hadith zimekuja kujulisha kuwa yaruhusiwa kuacha kujitibu, ambapo zinaondoa katika hadith hizi ujulishaji wa ulazima. Amepokea Muslim kutoka kwa Imran bin Huswain kwamba Mtume (saw) amesema:

«يَدْخُلُ الْجَنَّةَ مِنْ أُمَّتِي سَبْعُونَ أَلْفًا بِغَيْرِ حِسَابٍ»، قَالُوا: وَمَنْ هُمْ يَا رَسُولَ اللهِ؟ قَالَ: «هُمُ الَّذِينَ لَا يَكْتَوُونَ وَلَا يَسْتَرْقُونَ، وَعَلَى رَبِّهِمْ يَتَوَكَّلُونَ»

“Wataingia Peponi katika Ummah wangu watu elfu sabiini bila ya hisabu. Wakauliza: ni kina nani hao ewe Mtumbe wa Mwenyezi Mungu? Akajibu: ni wale wasiojichoma moto (kama tiba), na hawajisomei ruqya, na wanamtegemea Mola wao tu”.

Ruqya na kujichoma ni aina za kujitibu.

Amepokea Bukhari kutoka kwa ibn Abbas akisema:

...هَذِهِ المَرْأَةُ السَّوْدَاءُ، أَتَتِ النَّبِيَّ ﷺ فَقَالَتْ: إِنِّي أُصْرَعُ، وَإِنِّي أَتَكَشَّفُ، فَادْعُ اللَّهَ لِي، قَالَ: «إِنْ شِئْتِ صَبَرْتِ وَلَكِ الجَنَّةُ، وَإِنْ شِئْتِ دَعَوْتُ اللَّهَ أَنْ يُعَافِيَكِ» فَقَالَتْ: أَصْبِرُ، فَقَالَتْ: إِنِّي أَتَكَشَّفُ، فَادْعُ اللَّهَ لِي أَنْ لاَ أَتَكَشَّفَ، «فَدَعَا لَهَا...»

“... huyu mwanamke mweusi alimjia Mtume (saw) akamwambia: mimi huwa naanguka (kwa ugonjwa wa kifafa) halafu nafunuka nguo, niombee kwa Mwenyezi Mungu! Akasema: “Kama utataka vumilia, na Pepo itakuwa yako. Na kama utataka nitakuombea Mwenyezi Mungu akuponye”. Akasema: nitavumilia, akasema tena: mimi huwa nafunuka nguo, basi niombee Mwenyezi Mungu nisifunuke. Mtume akamuombea”.

Hadithi  hizi mbili nazo zajulisha kuwa yaruhusiwa kuacha kujitibu.

Yote hayo yanajulisha kuwa amri iliyo katika neno “jitibuni” sio amri ya lazima. Kwa hiyo, agizo hapa ima ni agizo la Mubaah (rukhsa) ama ni la kupendekeza. Na kuwa Mtume (saw) amesisitiza sana kujitibu, hivyo amri iliyokuja katika hizo hadith itakuwa ni amri ya kupendekeza.

 Kwa hiyo, hukmu ya chanjo itakuwa ni jambo lilopendekezwa, kwa sababu, chanjo ni matibabu, na matibabu yamependekezwa. Ila ikithibitika kwamba aina fulani ya chanjo ina madhara - kama vile iwe ina vitu vibaya au vyenye madhara fulani... - basi hiyo chanjo katika hali hii itakuwa haramu kwa sababu ya hivyo vitu vya haramu, kulingana na msingi wa kudhuru kutokana na hadith ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) iliyopokewa na Ahmad katika Musnad yake kutoka kwa ibn abbas kuwa Mtume amesema:

«لَا ضَرَرَ وَلَا ضِرَارَ»

“Hakuna kujidhuru wala kuwadhuru wengine” ila tu hilo hua katika hali nadra...

Ama katika dola ya Khilafah kutakuwa na chanjo dhidi ya magonjwa yanayohitaji chanjo kama vile magonjwa ambukizi na mfano wake, na dawa itakuwa safi kutokana na uchafu wowote na Mwenyezi Mungu (swt) ndie mponyaji:

وَإِذَا مَرِضْتُ فَهُوَ يَشْفِينِ﴿

 “Na ninapo ugua ni Yeye ndiye anaye niponesha.” [Ash-Shu'ara: 80] Na inavyojulikana kisheria ni kwamba uchungaji wa afya ni miongoni mwa wajibu juu ya khalifah na ni katika uchungaji wa mambo, kwa kulifanyia kazi neno lake Mtume (saw):

«الإِمَامُ رَاعٍ وَمَسْئُولٌ عَنْ رَعِيَّتِهِ»

“kiongozi ni mchungaji naye ataulizwa kuhusu raia wake”. Imepokewa na Bukhari kutoka kwa Abdullahi bin Umar. Na hii ni dalili wazi na inayoenea, juu ya majukumu ya serikali kuhusu afya na matibabu kwa kuwa yanaingia kwenye uchungaji ambao ni wajibu juu ya serikali.

Na zipo dalili maalum kuhusiana na afya na matibabu: amepokea Muslim kutoka kwa Jabir akisema:

«بَعَثَ رَسُولُ اللهِ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ إِلَى أُبَيِّ بْنِ كَعْبٍ طَبِيبًا، فَقَطَعَ مِنْهُ عِرْقًا، ثُمَّ كَوَاهُ عَلَيْهِ»

“Mtume (saw) alimtuma tabibu kwa Ubay bin Ka'ab, akamkata mshipa kisha akamchoma kwa moto” Na amepokea Al-Hakim kwenye kitabu cha Al-Mustadrak kutoka kwa Zaid bin Aslam, kutoka kwa babake akisema:

«مَرِضْتُ فِي زَمَانِ عُمَرَ بِنَ الْخَطَّابِ مَرَضاً شَدِيداً فَدَعَا لِي عُمَرُ طَبِيباً فَحَمَانِي حَتَّى كُنْتُ أَمُصُّ النَّوَاةَ مِنْ شِدَّةِ الْحِمْيَةِ»

“Niliugua sana zama za Umar bin Khatwab, Umar akaniitia tabibu, akanipa miko hadi nikawa namumunya konde ya tende kutokana ukali wa miko”.

Mtume (saw) akiwa na sifa ya mtawala alimtuma tabibu kwa Ubay, na Umar (r.a) Khalifah Muongofu wa pili naye alimtuma tabibu kwa Aslam lli amtibu. Na hizi ni dalili mbili kwamba afya na matibabu ni miongoni mwa mahitaji msingi ya raia, ambayo ni wajibu kwa serikali kuwatimizia bure kwa wanaotaka katika raia ] mwisho wa nukuu kutoka kwenye majibu.

Kwa mukhtasari:

1. Chanjo hukmu yake ni Mandub, yaani inapendekezwa wala sio lazima.

2. Ikiwa imetengenezwa kwa vitu vyenye madhara, basi itakuwa ni haramu.

3. Ikiwa chanjo haina madhara, ila ndani yake kuna vitu vya najisi au vya haramu, basi itakuwa yaruhusiwa pamoja na kuwa Makruh, yaani haitokuwa haramu.

4. Kwa hiyo, Muislamu mgonjwa kwanza anatakiwa kutafuta dawa Mubaah (inayoruhusiwa) na kama hakuipata basi anaruhusiwa kutumia dawa ambayo ni Makruh.

5. Hivyo basi, jibu la swali lako kulingana na ilivyofafanuliwa huko juu litakuwa kama inavyofuata:

Kutumia chanjo zenye vitu vya haramu ndani yake au najisi yaruhusiwa ingawa ni Makruh, kwa sababu chanjo inaingia kwenye mlango wa kujitibu. Na kujitibu kwa kilicho haramu au najisi - kama ilivyobainishwa huko juu - yaruhusiwa ingawa ni Makruh... isipokuwa kama itabainika kuwa na madhara ndani yake basi hapo itakuwa haifai.

Na mpaka sasa sijakatikiwa kuhusu rai yoyote kuhusiana na madhara na maudhi kutokana na dawa hii. Kwa hiyo basi, hilo jambo nawaachia mashababu, kulingana na wanayohisi ni sahihi na kuwa na utulivu nalo kwa mujibu wa maelezo yaliyotajwa huko juu.

Tunamuomba Mwenyezi Mungu (swt) atuepushe sisi na Waislamu wote kutokana na kila maradhi, kwani hakika yeye ni msikivu mno na mwenye kujibu.

Wa Salaamu Alaikum wa Rahmtullahi wa Barakatuh.

Ndugu Yenu,

Ata Bin Khali Abu Rashtah

9 Jumada Al-Akhar 1442 H

 22/1/2021 M

Link ya jibu hili kutoka ukurasa wa Amiri wa Facebook.

Andika maoni

Hakikisha umejaza (*) habari zinazohitajika palipoashiriwa. Kodi za HTML haziruhusiwi.

rudi juu

Vifungu vya Tovuti

Viunganishi

Magharibi

Ardhi za Waislamu

Ardhi za Waislamu