Jumatano, 09 Rabi' al-awwal 1444 | 2022/10/05
Saa hii ni: (M.M.T)
Menu
Main menu
Main menu

بسم الله الرحمن الرحيم

 Jibu la swali

Hukmu ya Baba Anaye Muozesha Binti Yake Pasi na Ridhaa Yake

Kwa: ‏‎Nazik Al-Malaika

(Imetafsiriwa)

Swali:                                    

Nina swali na nataraji kuwa swali langu litajibiwa kwa haraka.

Je, inaruhusiwa ndoa kufanyika bila ya msichana kutoa ridhaa kwa mume?

Ni njia ipi ya kutatua tatizo hili endapo ndoa itafungwa ilhali bado haijakamilika? Sio kwa sababu nimelazimishwa kutia saini, bali kwa sababu wameniambia kuwa mchumba au bwana harusi yuko mlangoni na nikamkubalia, lakini kwa kuhisi kuwa chini ya shinikizo na kulazimishwa kukubali pasi na kuzungumzishwa.

Jibu:

Wa Alaikum Assalam wa Rahmatullahi wa Barakatuh,

Kuhusiana na kadhia hii, tumetaja katika kitabu, Nidhamu ya Kijamii katika Uislamu, mlango wa Ndoa, Hadith ya Mtume (saw) juu ya mada hii:

“Abdullah bin Burayda (ra) amesimulia kutoka kwa babake kuwa

«جاءتْ فتاةٌ إلى رسولِ اللهِ صلى الله عليه وسلم فقالتْ: إن أبي زَوَّجَني ابنَ أَخيهِ لِيَرْفَعَ بي خَسيسَتَهُ. قال فَجَعَلَ الأمرَ إليها فقالتْ قد أَجَزْتُ ما صَنَعَ أبي، ولكنْ أردْتُ أن أُعْلِمَ النساءَ أنْ ليسَ إلى الآباءِ مِنَ الأمْرِ شيءٌ»

“Msichana mmoja alikuja kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) akasema: “Hakika babangu ameniozesha kwa mtoto wa kaka yake ili kunyanyua hadhi yake ya chini.” Hivyo Mtume (saw) akampa haki ya kuvunja ndoa hiyo. Akasema: “Nimekubali yale aliyoyafanya babangu, lakini nilitaka kuwajulisha wanawake (wengine) kuwa kina baba hawana mamlaka ya kuwaozesha binti zao pasi na ridhaa zao.”, imesimuliwa na Ibn Majah.” Mwisho,

Inasemwa katika “Mesbah al-Zujajah fi Zawaid ibn Majah” na mwandishi wake Abu al-Abbas Shihabuddin al-Busairi al-Kannani al-Shafi’i (aliyekufa: 840 H): 

“Abdullah bin Burayda (ra) anasimulia kutoka kwa babake kuwa msichana mmoja mdogo alikuja kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) na kusema: “Babangu ameniozesha mpwa wake ili kunyanyua hadhi yake ya chini. Yeye akasema: «فَجعل الْأَمر إِلَيْهَا فَقَالَت قد أجزت مَا صنع أبي وَلَكِن أردْت أَن تعلم النِّسَاء أَنه لَيْسَ للآباء من الْأَمر شَيْء» “Mtume (saw) akampa haki ya kuvunja ndoa hiyo. Akajibu: “Nimekubali yale aliyoyafanya babangu, lakini nilitaka kuwajulisha wanawake (wengine) kuwa kina baba hawana mamlaka ya kuwaozesha binti zao pasi na ridhaa zao.” Na akasema riwaya hii ni sahih na wapokezi wake ni waaminifu”

Kutokana na hayo, babake ni lazima apate ridhaa yake, na afisa mfungaji ndoa hiyo ni lazima ahakikishe hilo, ili ombi (Ijab) na kukubali (Qubul) yafanyike kwa ridhaa na chaguo.

Tumefafanua waziwazi hili katika Nidhamu ya Kijamii katika mlango huo uliotajwa juu wa Ndoa, ambao unasema:

“Pindi mwanamke anapoposwa, yeye pekee ndiye aliye na haki ya kuikubali ndoa hiyo au kuikataa. Hakuna yeyote katika mawalii wake (Awliya) au yeyote mwengine aliye na haki ya kumuozesha pasi na idhini yake au kumzuia kuolewa. Imeripotiwa kutoka kwa Ibn 'Abbas kuwa alisema kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) amesema: «الثَّيِّبُ أحقُّ بِنَفْسِها مِنْ وَلِيِّها،  والبِكْرُ  تُسْتأْذنُ في نَفْسِها وإِذنُها صُماتُها»  “Mke mkuu ana haki zaidi katika nafsi yake kuliko walii wake, na mwari huulizwa idhini yake. Idhini yake (mwari) ni kunyamaza kwake”. Abu Hurayrah (ra) pia amesimuliwa kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) amesema: «لا تُنْكَحُ الأَيِّمُ حتى تُسْتَأْمَرَ، ولا البِكْرُ حتى تُسْتَأْذَنَ. قالوا: يا رسولَ اللهِ، وكيفَ إذْنُها؟ قال: أن تَسْكُتَ» “Mke mkuu hapaswi kuozeshwa mpaka baada ya kushauriana naye; na mwari hapaswi kuozeshwa mpaka baada ya kuulizwa idhini yake”. (Watu) wakasema, “Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, Vipi tutajua idhini yake”? Yeye (saw) akasema: “Kunyamaza kwake [huashiria idhini yake].” [Imepokewa na Bukhari na Muslim] Ibn 'Abbas amesimulia kuwa

«أن جاريةً بكْراً أَتَتْ رسولَ اللهِ صلى الله عليه وسلم فَذَكَرَتْ أَن أَباها زَوَّجَها وهِيَ كارِهَةٌ، فَخَيَّرها النبيُّ صلى الله عليه وسلم»

“Mwari mmoja bikra alikuja kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) akataja kuwa babake alimuozesha dhidi ya matakwa yake. Hivyo Mtume (saw) akampa khiyari ya kuvunja ndoa hiyo.” [Imesimuliwa na Abu Dawood] Khansa bint Khizam al-Ansariya (ra) amesimulia kuwa

«أن أباها زَوَّجها وهِيَ ثَيِّبٌ فَكَرِهَتْ ذلك فأَتَتْ رسولَ اللهِ صلى الله عليه وسلم فَرَدَّ نِكاحَها»

“Babake alimuozesha na hali ya kuwa yeye ni mke mkuu basi akachukia hilo. Akaja kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) na (Mtume) akaivunja ndoa yake.” [Imesimuliwa na Bukhari] Hadith hizi zaonyesha waziwazi kuwa endapo mwanamke hatatoa idhini kwa ndoa yake basi ndoa hiyo haijatimia. Endapo ataikataa ndoa hiyo au ataozeshwa kwa nguvu mkataba huo utakuwa ni batil, isipokuwa ikiwa atarudi na kutoa ridhaa kwake.”

Unaona dalili ya wazi juu ya kadhia hii kama tulivyo taja juu, na twairudia: “Hadith hizi zaonyesha waziwazi kuwa endapo mwanamke hatatoa idhini kwa ndoa yake basi ndoa hiyo haijatimia. Endapo ataikataa ndoa hiyo au ataozeshwa kwa nguvu mkataba huo utakuwa ni batil, isipokuwa ikiwa atarudi na kutoa ridhaa kwake.”

Natarajia kuwa hili litatosheleza, na Mwenyezi Mungu Mtukufu ni Mjuzi zaidi na Yeye ni Mwingi wa hekima.

Ndugu yenu,

Ata Bin Khalil Abu Al-Rashtah

14 Jumada II 1441 H

Jumamosi, 08/02/2020 M

Linki ya jibu hili imetoka kwa ukurasa wa Amiri wa Facebook

Imebadilishwa mara ya mwisho mnamoJumanne, 24 Machi 2020 21:37

Andika maoni

Hakikisha umejaza (*) habari zinazohitajika palipoashiriwa. Kodi za HTML haziruhusiwi.

rudi juu

Vifungu vya Tovuti

Viunganishi

Magharibi

Ardhi za Waislamu

Ardhi za Waislamu