Jumamosi, 19 Dhu al-Qi'dah 1446 | 2025/05/17
Saa hii ni: (M.M.T)
Menu
Main menu
Main menu

بسم الله الرحمن الرحيم

Jibu la Swali

Dola ya Kina (Deep State)
(Imetafsiriwa)

Swali:

Neno “dola ya kina” (deep state) limetumika sana miongoni mwa wanasiasa na katika vyombo vya habari. Hata hivyo, katika kuchunguza kauli hizi, inadhihirika kwamba ziko tofauti. Je, unaweza kufafanua zaidi uwezekano wa maana ya suala hili ili tuweze kuelewa uhalisia wa kisiasa kuhusiana na neno hili, na kutoa baadhi ya mifano kwa ufafanuzi zaidi? Naomba radhi ikiwa ombi langu la mifano hii litakukengeusha kutoka kwa kazi muhimu zaidi na yenye thamani unayofanya. Shukran.

Jibu:

Ndiyo, kuna tofauti katika kile kinachochapishwa kuhusu neno "dola ya kina." Wengine hufasiri kuwa lina maana ya matabaka yenye ushawishi nje ya serikali, yanazofanya kazi kwa siri dhidi ya utawala uliopo, kama ilivyokuwa nchini Uturuki. Wengine wanaifasiri kama nguvu yenye udhibiti ndani ya utawala; inayotawala nchi wakati wowote inapotaka. Ikiwa tatizo litatokea, hulibandika kwa mtu mwengine.

Huondoka kutoka kwa uongozi na kumleta mtu mwengine wa kulaumiwa kwa tatizo hilo, kisha inaregea tena madarakani, kama inavyotokea nchini Uingereza. Wengine wanaitafsiri kama mapambano kati ya vyama vyenye ushawishi, kama inavyofanyika hivi sasa chini ya Trump nchini Marekani. Wengine wanaitumia kama mbuzi wa kafara kwa mapungufu yao ya utawala na kufeli kwao, na hivyo kufungamanisha haya na kile wanachokiita "dola ya kina." Wengine hutumia neno hili wakati wowote wanapotaka kuwapurukusha watu na jambo fulani, wakilitaja kwa maneno yao wenyewe au kwa kutumia maneno mengine. Wengine hufasiri dola za kikoloni kuwa ndizo dola za kina katika makoloni yao. Ili kufafanua maana sahihi ya suala hili, tutahakiki mambo yafuatayo:

Kwanza: Baadhi ya ufafanuzi wa (neno) dola ya kina:

1- Kamusi ya Webster, mojawapo ya kamusi kongwe zaidi duniani, inaelezea dola ya kina (deep state) kama: "mtandao wa siri unaodaiwa kuwa wa maafisa wa serikali ambao hawakuchaguliwa na wakati mwingine mashirika ya kibinafsi yanayofanya kazi nje ya sheria kushawishi na kutunga sera ya serikali". Hii ina maana kwamba, mbali na sheria na katiba, kuna nguvu kubwa zaidi inayolitawala taifa. Nguvu hii ina ajenda yake na inaweza kudhoofisha maamuzi ya serikali iliyochaguliwa.

2- Wikipedia inasema: “Nchini Uturuki, dola ya kina (kwa Kituruki: derin devlet) ni kundi la miungano yenye ushawishi dhidi ya demokrasia ndani ya muundo wa kisiasa wa Uturuki, inayoundwa na watu wa ngazi ya juu ndani ya huduma za kijasusi (ndani na ng’ambo), jeshi la Uturuki, mashirika ya usalama, mahakama, na umafia... Ajenda ya kisiasa ya mtandao wa dola ya kina inadaiwa kuhusisha utiifu kwa utaifa, ushirika, na maslahi ya dola. Vurugu na njia zingine za shinikizo zimetumika kihistoria kwa njia ya siri ili kulidhibiti pote la kisiasa na kiuchumi, kuhakikisha kuwa maslahi mahususi yanatimizwa ndani ya muundo unaoonekana kuwa wa kidemokrasia wa mazingira ya kisiasa.”

3- Kwa kuchunguza kile wanachomaanisha watu hawa kwa neno "dola ya kina," tunagundua kwamba ina maana ya kuwepo kwa nguvu iliyofichika ndani au nje ya vyombo vya dola ambayo inadhibiti mfumo wa kisiasa, yaani, inalazimisha sera, maoni, na mwelekeo wake kwa wanasiasa waliochaguliwa kisheria ... Nguvu hii iliyofichika ni mtandao uliopangwa wa watu binafsi ambao hupenya vituo nyeti kama vile jeshi, vyombo vya usalama, na vikosi vya kisiasa, inayotenda ikiwa uhuru na serikali iliyochaguliwa... wakati mwengine istilahi tofauti zinatumiwa kukusudia mtandao huu.. kama vile “dola ya kina,” “dola sambamba,” “dola nyuma ya pazia” au “dola ndani ya dola”

4- Kuna ufafanuzi mwingine, tofauti unaotolewa na mwanasiasa aliyeshindwa serikalini au katika uchaguzi akiitumia kama kisingizio cha kushindwa kwake serikalini au katika uchaguzi. Kwa maana nyengine, ni fahamu ya upotoshaji, inayotumika kuwaondolea watawala mafisadi hatia, pindi dhulma, au uhaini vinapoenea nchini. Ni udanganyifu wa mtawala, ambaye anaweka lawama kwa watu binafsi nyuma ya pazia, ambao anawaita "dola ya kina," kisha huwapotosha watu juu ya ukweli kwamba yeye ndiye anayehusika na kwamba lazima abadilishwe.

5- Pia kuna madai kuwa dola za kikoloni ndizo dola ya kina katika koloni zao, zenye kudhibiti mifumo ya koloni zao, na kuwaweka baadhi ya watawala na kuwaondoa wengine.

Pili: Ufafanuzi Unaowezekana Zaidi:

1- Kwa kuchunguza kwa makini fasili hizi na kutafakari yaliyomo, ufafanuzi unaowezekana zaidi ni kwamba dola ya kina katika nchi inamaanisha nguvu yenye ushawishi, iwe ya kisiasa, kiuchumi, au familia za kiungwana zenye ushawishi kutoka ndani au nje ya nchi. Nguvu hii sio sehemu rasmi ya vyombo vya serikali, lakini inaathiri serikali kwa siri. Inatoa shinikizo la ufanisi na ushawishi kwa chombo rasmi cha serikali kutekeleza matakwa yake au kuyabadilisha.

2- Ama kuhusu mtawala kuwapotosha watu ili aondoe tuhuma za ufisadi kutoka kwake na kuzibandika kwenye chombo chengine anachokiita “deep state,” yaani ni mbuzi wa kafara kwa utawala wake mbovu na ufisadi, kuuita udanganyifu huu kuwa ni “deep state” sio sahihi, kwani ni hadaa inayofanywa na mtawala, sio na vyombo vyengine.

3- Ama kuhusu kuzichukulia dola za kikoloni kuwa ndio dola za kina (deep state), hili pia sio sahihi kwa sababu dola za kikoloni ndizo zinazodhibiti koloni zao na ni ngeni kwazo, na sio nguvu nyengine kutoka kwa wananchi zinazofanya kazi kwa siri, zilizofichika kutoka kwa vikosi teule vya utawala, ambapo pia ni kutokana na wananchi.

Tatu: Mifano ya dola ya kina (deep state) katika baadhi ya nchi, kwa ufafanuzi zaidi:

1- Uturuki

a- Asili ya neno "dola ya kina" ametokea Uturuki. Mwishoni mwa Dola ya Uthmani, maafisa wa Kamati ya Muungano na Maendeleo, ambao waliathiriwa na mawazo ya Kimagharibi, walifanya mapinduzi mwaka 1909, wakampindua Khalifa Abdul Hamid II na kumteua kaka yake, Muhammad Reshad, kuwa Khalifa mwenye mamlaka ya chini kuliko mamlaka yao.

* Huu uliashiria mwanzo wa kuibuka tabaka lenye nguvu zaidi kuliko Khalifa, likiathiri kunusurika au kuanguka kwake kwa namna inayoonekana, kuliko iliyo jificha. Hata hivyo, hawakupindua Khilafah na utawala wa Kiislamu. Kiuhalisia, hawakuwa, dola ndani ya dola, kwa maana ya dola ya siri, ya kina. Walionekana ndani ya dola, lakini waliidhibiti serikali.

b- Baada ya Vita vya Kwanza vya Dunia, Mustafa Kemal, ambaye alikuwa mtiifu kwa Waingereza, aliweza kunyakua madaraka na kisha akaweza kuivunja Khilafah, kuiondoa Shariah, na utabikishwaji wa sheria zake. Aliitangaza Jamhuri na kuijenga juu ya misingi ya kisekula. Alifanya mapinduzi dhidi ya utawala wa Kiislamu, na hata dhidi ya madhihirisho ya Uislamu, kama vile yale yanayojulikana kama "mapinduzi ya herufi", ambayo yalikuwa yakibadilisha herufi za lugha ya Kituruki kutoka Kiarabu hadi Kilatini. Au "mapinduzi ya mavazi ya kidini", na kuyabadilisha na mavazi ya Kimagharibi, na kadhalika. Kwa hivyo, alianzisha jeshi na vikosi vya usalama kwa mujibu wa viwango maalum vya kulinda jamhuri na usekula, na kuzuia kurudi kwa Uislamu madarakani na kusimamishwa tena kwa Khilafah. Jeshi likawa nguvu ya kudhibiti serikali, lenye kuingilia kati kila lilipoona kupotoka kutoka kwa fikra ya Ukemali (Kemalism), pamoja na kudumisha utiifu kwa Uingereza. Udhalimu wa utawala wa Kemali na msaada wa Uingereza ulizuia kuibuka kwa dola ya kina dhidi ya utawala huu.

c- Erdogan alipoingia madarakani nchini Uturuki kwa kasi ya matokeo ya sanduku la kura, na kwa uungwaji mkono wa kisiasa, kifedha na kiuchumi wa Marekani, alifahamu uwezo wa majenerali wa jeshi, walinzi wa usekula, watiifu kwa Waingereza, na kwamba wanawakilisha uti wa mgongo wa dola na wangeweza, kama wangetaka, kufanya mapinduzi dhidi yake. Kwa hiyo, alikuza maadili ya demokrasia na uhuru na kuwazingira kwa nguvu ya uhalali wa wananchi ili kuwazuia wasifanye mapinduzi dhidi yake. Amerika ilikuwa ikiwafanya Waturuki watokwe na mate kupitia mishipa yake ya kifedha na kiuchumi. Erdogan aliwaogopa wanajeshi hawa na hakuweza kuwafukuza kutokana na wingi wao na uwezo wao wa kudhibiti uti wa mgongo wa jeshi kwa miaka mingi. Walakini, haraka aliunda uhalisia mpya katika maisha ya Kituruki, jina maarufu ambalo lilikuwa "demokrasia" na mafanikio ya kiuchumi, na hii ikawa kikwazo kwa mapinduzi.

* Katika kipindi hiki, maelezo ya kuwepo kwa "dola ya kina" nchini Uturuki inayofanya kazi kwa siri ndani ya vyombo vya serikali, hasa jeshi, kuzuia, kupinga, na kujaribu kutibua maelekezo ya Waziri Mkuu aliyechaguliwa Erdogan yalikuwa maelezo sahihi. Watu hawa walikuwa ni mtandao ambao hulka zao hazikuonekana kwa wale wenye mtazamo wa juu juu ambao waliamini kuwa mambo yalikuwa yanaenda sawa na kwamba kila mtu alikuwa amejitolea kwa katiba na sheria. Mtandao huu wa Kituruki, pamoja na kuweka kiota ndani ya jeshi, mahakama, na wizara, uliunganishwa na vyama vya kisekula vilivyokuwa nje ya dola na kuwakilisha upinzani, na uliunganishwa na kitovu kilicho jijini London. Wanachama wake walikutana kwa siri, kushauriana, na kujadili masuala ya utawala wa Erdogan hadi walipoamua kufanya mapinduzi mwaka 2016, lakini hayakufaulu. Erdogan kisha akatumia hili kama hoja; kwa hiyo, aliwang’oa kutoka jeshini, pamoja na wafuasi wao kutoka katika mahakama na wizara, hadi utakaso huo ukawafikia maprofesa wa vyuo vikuu. Kwa hivyo, Erdogan alifanikiwa kung'oa dola ya kina iliyohusishwa na Waingereza ndani ya jeshi la Uturuki na ilikuwa karibu kumaliza uwepo wake. Hata hivyo, bado walikuwa na wafuasi, ingawa ni dhaifu kuliko hapo awali, ambao wanajaribu kufufua sifa ya "dola ya kina" inayoikabili serikali.

2- Marekani

a- Serikali katika Amerika imegawanyika katika ngazi mbili halisi. Ngazi ya kwanza inaonekana kuwakilisha uhalali wa watu wengi, inayofanya kazi kutekeleza matakwa ya watu waliomchagua rais huyu na wawakilishi hawa. Kwa hivyo, sura ya serikali ni ya "kidemokrasia." Hata hivyo, ngazi hii halali inaweza tu kuongoza sera za nchi kwa mujibu wa matakwa ya ngazi ya pili, ambayo ni ngazi ya ndani, isiyoonekana, na isiyochaguliwa. Hii ina maana siyo halali kwa mujibu wa mfumo wa "demokrasia". Hii ndio wanaiita "dola ya kina" (deep state). Watu binafsi katika ngazi hii, yaani, wawakilishi wa dola ya kina (deep state), wanashikilia nyadhifa nyeti ndani ya vyombo vya dola. Vyombo wanavyovidhibiti haviwezi kutenda kwa mujibu wa maagizo ya ngazi ya kwanza isipokuwa kupitia kwao, kwa sababu nyadhifa zao ni nyeti. Watu hawa nchini Amerika ima ni mabepari wakuu au wawakilishi wao. Mabepari wakuu nchini Amerika wako makini kuhakikisha kuwa maafisa wakuu katika vyombo vya dola wanalinda maslahi yao, wanadumisha mawasiliano ya mara kwa mara na maafisa hawa ili kuendeleza maslahi yao. Kwa mfano, makampuni ya kifedha yako makini kuwa na wafuasi miongoni mwa wafanyikazi wa idara za kodi, huku makampuni ya silaha yako makini kuwa na wafuasi katika Pentagon na idara za kandarasi za kijeshi katika Wizara ya Mambo ya Nje. Makampuni ya madawa yana nia ya kuwa na wafuasi katika Wizara ya Afya na idara za bima za serikali. Kwa hivyo, kwa muda mrefu, mashirika makubwa yamefaulu kudhibiti imara serikali nchini Amerika kupitia wafanyikazi hawa katika nyadhifa nyeti na kupitia lobi za kushinikiza.

b- Huu ndio uhalisia wa mfumo wa kisiasa nchini Amerika. Kutokana na hayo, mabepari wakuu na mashirika makubwa ndio chimbuko na mzizi wa uhai wa dola ya kina (deep state) nchini Amerika. Ni nguvu iliyofichika, nyuma ya mielekeo ya kisiasa ya serikali, na ndiyo nguvu inayowapa motisha wafanyikazi katika nyadhifa nyeti kupinga mielekeo ya serikali ikiwa inakinzana na maslahi ya mashirika hayo. Katika maelezo haya, (deep state) iko nje na ndani ya vyombo vya dola na inafanya kazi katika sekta ya kifedha, biashara, na viwanda, lakini shughuli zake zinaonekana dhahiri ndani ya vyombo vya dola nchini Amerika.

c- Donald Trump alipoingia mamlakani mwaka wa 2016, alikabiliwa na hali ya kutoridhika miongoni mwa maafisa wakuu wa serikali na mashirika mbalimbali, hasa vyombo vya usalama. Alihisi kukataa kwao na upinzani kwa sera zake, ambazo baadaye zilikua na kuwa upinzani mkali kutoka ndani ya serikali ya Marekani, na kukaribia uasi. Kulikuwa na uvujaji mwingi wa habari za aibu kutoka kwa mashirika ya usalama na ujasusi ... Kisha, mashtaka mengi yalifunguliwa dhidi yake, ambayo maarufu zaidi ilikuwa msaada wa Urusi kwake katika uchaguzi. Uchunguzi na majaribio ya kumshtaki yalizuka katika Bunge la Congress, hadi Wizara ya Sheria ya Marekani ikawa mmoja wa maadui wake wakubwa. Shambulizi dhidi yake halikutoka tu ndani ya serikal hiyo, kwani kampuni za dawa ambazo zilikuwa zimegundua chanjo ya virusi vya korona ziligoma kutangaza uvumbuzi huu hadi baada ya ushindi wa Biden katika uchaguzi kutangazwa mwishoni mwa 2020, yaani, kumzuia Trump kufaidika na uvumbuzi huu. Kisha, kutokana na mateso yake kutokana na kikosi hiki kilichojificha, kilichopangwa kufanya kazi dhidi yake, rais alitilia shaka matokeo ya uchaguzi na hakuyatambua, akizingatia kuwa yalikuwa ya udanganyifu na kwamba ushindi umeibiwa kutoka kwake. Aliiongeza tume ya uchaguzi ya dola hiyo kwenye orodha yake ya maadui. "Ima dola ya kina (deep state) iiangamize Amerika, au tuiangamize dola ya kina," Trump aliuambia umati wa wafuasi huko Texas kwa mpiku wake kutoka kwa urais mnamo 2023. Tukichunguza uhalisia huu wa Amerika wakati wa utawala wa kwanza wa Trump na maelezo haya ya nguvu iliyofichika ndani ya Amerika inayomzuia rais mteule kubadili mwelekeo, tunapata kwamba maelezo haya yanaelezea uhalisia wa kweli wa mfumo wa serikali ya Amerika.

3 - Uingereza

Kuhusu Uingereza, inayo dola ya kina (deep state). Mfumo wake wa utawala unawakilishwa na Wahafidhina (Conservatives), familia za kifalme za Uingereza na vipote vya matajiri. Hao ndio watawala wa kweli wa Uingereza. Hata hivyo, sera zao walizotangaza wakati mwingine hupelekea nchi kuingia kwenye machafuko, kumaanisha wakati mwingine hudhuru maslahi ya nchi. Kwa hivyo, Chama cha Conservative huingia kwenye mapumziko, na Chama cha Leba kinatawala nchi. Dhamira ya Chama cha Leba ni kutatua migogoro na kuzuia madhara kwa maslahi ya nchi. Kisha kinashuka madarakani. Tulichoshuhudia hivi majuzi—kushindwa kwa kishindo kwa Chama cha Conservative na ushindi mkubwa wa Chama cha Leba—ni kazi ya Wahafidhina. Baada ya Brexit, Uingereza inakabiliwa na mgogoro mkali wa kiuchumi. Hakika, kuondoka kwake kutoka Muungano wa Ulaya kulitokana na makosa katika hesabu zake za kura ya maoni ya Uingereza kuhusu Ulaya. Kwa vile Conservatives ndio waliounda na kusababisha mgogoro huu, Chama cha Leba kinatakiwa leo kuutatua.

Dola ya kina (deep state) nchini Uingereza ni familia za zamani na kitajiri. Wamekuwa watawala wa Uingereza kila wakati. Endapo watajiweka kando na kuleta chama cha Leba, ni kwa sababu ya kutatua mgogoro unaosababishwa na Conservatives. "dola ya kina" nchini Uingereza hudhibiti serikali kwa urahisi na ulaini, ikimaanisha kuwa familia za zamani za kitajiri za Uingereza ndio chimbuko la serikali na walinzi wake, iwe wanaitekeleza au "wameajiri" chama chengine kutekeleza. Ili udhibiti huo uendelee kwa ulaini na urahisi huo, "chanzo cha serikali yenye ufanisi" nchini Uingereza na "mzizi wake hai" hueneza maadili yanayokataa mabadiliko na kunnyanyua hadhi ya ukale na fahari ya kale. Hili ndilo linalozingatiwa nchini Uingereza kutokana na shauku kubwa ya watu katika familia ya kifalme, habari na hadithi zake, siku za kuzaliwa za wakuu wake na mtindo wake wa maisha...!

Kwa kumalizia:

* Dola ya kina (deep state) ni nguvu yenye ushawishi ndani ya serikali iliyopo. Ni mtandao wa raia wa nchi, ndani na nje ya nchi, wanaofanya kazi kwa siri dhidi ya tabaka tawala nchini humo ili kuibadilisha au kuidhoofisha.

* Hata hivyo, ikiwa mtandao huu hautokani na watu wa nchi hiyo bali ni nguvu ya kigeni, kama vile dola ya kikoloni inayofanya kazi dhidi yake, au dola adui, basi nguvu hizo hazizingatiwi kuwa ni dola ya kina (deep state). Badala yake, ufafanuzi wake unaangukia chini ya kigawanyo cha ukoloni, vita, na uvamizi.

* Vile vile mtandao huu ukitayarishwa na tabaka tawala ili kujinasibisha na kazi dhidi ya dola na mipango yake, ili kuondosha lawama kutoka kwa mtawala na kupeleka lawama kwa mtandao hewa uliojiundia wenyewe, kwa lengo la kuwahadaa wananchi kuhusu ufisadi na uzembe wa mtawala, basi mtandao huo hauzingatiwi kuwa ni dola ya kina (deep state).

* Jambo la msingi ni kwamba ni mtandao wa wananchi ndani au nje ya nchi wanaofanya kazi kinyume na utawala uliopo katika nchi hiyo ili kuubadilisha au kuudhoofisha. Kwa maana hii, upo tu katika nchi ambazo zinatawaliwa na sheria zilizotungwa na binadamu, ambapo kuna uwezekano wa mitandao kuwepo ndani au nje ambayo inatofautiana katika aina ya utawala wanaoutaka, na migogoro hutokea baina yao kuhusiana na aina ya utawala uliotungwa na mwanadamu unaotakiwa.

* Iwapo hukmu imeegemezwa juu ya sheria kutoka kwa Mola Mlezi wa Walimwengu wote, basi Waislamu, wawe ndani au nje ya nchi, hawawezi kuwa na dola ya kina (deep state) inayofanya kazi ya kuubadilisha utawala wa Uislamu kwa hukmu tofauti. Hii ni isipokuwa ikiwa Waislamu wanaofanya kazi ndani au nje ya nchi wanasukumwa na mkoloni wa nje au kikosi cha uvamizi. Katika hali zote mbili, sio dola ya kina (deep state), kama tulivyosema hapo awali.

Kwa hiyo, mabadiliko au mapinduzi yaliyoonekana katika baadhi ya nchi za Kiislamu, kama yalivyotokea au yanayotokea Pakistan, Bangladesh, Misri, nk., hayawezi kuelezewa kuwa ni dola ya kina (deep state), kwa sababu ukoloni ndio unaoendesha matukio katika nchi vibaraka zinazoitumikia.

**Iwapo kuna vuguvugu katika nchi za Kiislamu ambalo linatawaliwa na sheria zilizotungwa na mwanadamu, na harakati hii inafanya kazi ya kubadilisha utawala wa mwanadamu katika nchi za Kiislamu kwa utawala wa Kiislamu, Khilafah Rashida, basi harakati hii haiitwi dola ya kina (deep state). Bali ni harakati ya Nusra kwa ajili ya Mwenyezi Mungu (swt) na Mtume wake (saw).

Tunamuomba Mwenyezi Mungu (swt) atunusuru na kufaulu katika kusimamisha tena Khilafah Rashida, ili Uislamu na Waislamu wapate ushindi na ukafiri na makafiri wadhalilike:

[وَعَدَ اللهُ الَّذِينَ آمَنُوا مِنْكُمْ وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ لَيَسْتَخْلِفَنَّهُمْ فِي الْأَرْضِ كَمَا اسْتَخْلَفَ الَّذِينَ مِنْ قَبْلِهِمْ]

“Mwenyezi Mungu amewaahidi wale walio amini miongoni mwenu na wakatenda mema, ya kwamba atawafanya makhalifa katika ardhi kama alivyo wafanya makhalifa wa kabla yao” [An-Nur: 55].

6 Dhul Qi’dah 1446 H

4/5/2025 M

Andika maoni

Hakikisha umejaza (*) habari zinazohitajika palipoashiriwa. Kodi za HTML haziruhusiwi.

rudi juu

Vifungu vya Tovuti

Viunganishi

Magharibi

Ardhi za Waislamu

Ardhi za Waislamu