Jumatatu, 10 Rabi' al-awwal 1445 | 2023/09/25
Saa hii ni: (M.M.T)
Menu
Main menu
Main menu

Afisi ya Habari
Kenya

H.  9 Jumada II 1443 Na: 1443/06 H
M.  Jumatano, 12 Januari 2022

 Taarifa kwa Vyombo vya Habari

Uchochezi na Uenezaji wa Sumu za Kikabila ni Ada ya Siasa ya Kidemokrasia Iliyofeli

Seneta wa Meru anakabiliwa na mashtaka ya madai ya matamshi ya uchochezi aliyoyatamka kwenye mkutano wa kisiasa wa naib rais William Ruto huko Eldoret. Kwengineko mkurugenzi mkuu wa mashtaka ya umma amemwagiza mkuu wa Polisi Hillary Mutyambai kumchunguza mbunge wa eneo la kitutu chache huko Kisii Richard Onyoka kwa matamshi aliyoyasema kwenye mkutano wa kisiasa. Kulingana na baadhi ya ripoti mbunge huyo alikamatwa kwa mashtaka ya kutamka semi za chuki za kuchochea ghasia. Tuhuma hizi za matamshi ya kiuchochezi ndizo za karibu zaidi kuripotiwa humu nchini hali ambayo sasa imekuwa ada ya siasa za Kenya.

Miezi saba kufikia kwenye uchaguzi mkuu, tayari hali ya kisiasa nchini inaanza kugubikwa na taharuki na uchochezi kwenye safu za wanasiasa. Viongozi wa kisiasa wakijitolea kwa udi na uvumba kujaribu kuyafikia maslahi yao ya kisiasa, kiuchumi na kijamii kwa kutumia mbinu ya kuwabagua raia kimaeneo sambamba na kueneza sumu za ukabila ambazo hutumiwa kama zana zao za kufikia malengo yao ya kisiasa. Kwa kutumia mbinu hizi chafu, wanasiasa wa mirengo yote husikika wakitamka semi za uchochezi na kupandikiza ukabila.

Kwa kuwa Demokrasia ni siasa ya ‘wengi wape’ hali inayopelekea wanasiasa wake kuweza kuunda na kubuni miungano ya kikabila na kimaeneo itakayowawezesha kupata kura nyingi.  Miungano ya kikabila ndio kiashirio kikubwa kwenye mashindano ya kuingia ikulu- nafasi kubwa ya kisiasa ya nchi. Kwa kuwa msingi wa itikadi ya kiilmaaniya (secularism) umefanya kipimo cha matendo ya wanadamu ikiwemo siasa ni kujitafutia mapato na maslahi hivyo si ajabu kusikia ule msemo maarufu wa kisiasa usemao: “Hakuna adui wa kudumu wala rafiki wa kudumu bali yaliyoko ni maslahi ya kudumu.” Itikadi hii ndio hupelekea kuibuka kwa ndoa na miungano mipya ya kisiasa kwenye kila muhula wa uchaguzi, ambayo wanasiasa hulenga kushinda tu uchaguzi wala sio kuhudumikia jamii.

Tungependa kueleza bayana kwamba mfumo huu wa Kidemokrasia unaotawala leo duniani umeshindwa kudhamini mabadiliko ya kiutawala ya amani na utulivu kutoka uongozi mmoja hadi kwa mwengine. Isitoshe, mfumo huu kimaumbile huzua hofu na taharuki miongoni mwa raia hasa katika vipindi vya uchaguzi na hili si tu kwa Kenya tu bali hata zile nchi zinazojipiga kifua kuwa zimeendelea Kidemokrasia kama vile Marekani. Ikumbukwe kwa mfano, Januari mwaka jana mashindano ya kisiasa kati ya Biden na Trump yaligeuka fujo pale wafuasi wa Trump walipovamia jengo kuu la Capitol Hill. Si hilo tu bali khiyana za Kisiasa nazo zimekuwa mojawapo ya sifa inayojitokeza katika siasa ya Demokrasia ambapo maslahi yakiwa ni yenye kuzunguka kadri ya mazingira ya kisiasa yanavyobadilika.

Uislamu una mfumo wa kiutawala wa aina yake uliokitia kwenye msingi wa kuchanganya hisia ya kiroho (Uchamungu) katika matendo yote yakiwemo ya kisiasa. Kwa mantiki hii, ndio michakato yote ya kisiasa ipo katika kutafuta radhi za Mwenyezi Mungu (swt). Sifa ya uchajimungu humfanya mtu yeyote akiwemo kiongozi wa kisiasa kufanya uongozi na siasa kuwa ni ubebaji wa majukumu na uwajibikaji asili ukilenga ufanisi sio tu maisha ya hapa duniani bali hata  kesho akhera. Kwa msingi wa falsafa hii, Uislamu ukazalisha wanasiasa wakomavu na mahiri walio na sera imara zilizopelekea kuweko na ufanisi wa kisiasa, kiuchumi na kijamii kama ilivyoshuhudiwa katika kipindi cha utawala wa Khilafah kwa karne kumi na tatu.

Shabani Mwalimu

Mwakilishi kwa Vyombo vya Habari

Hizb ut Tahrir Kenya

Hizb-ut Tahrir: Afisi ya Habari
Kenya
Address & Website
Tel:  +254 707458907
E-Mail: mediarep@hizb.or.ke

Andika maoni

Hakikisha umejaza (*) habari zinazohitajika palipoashiriwa. Kodi za HTML haziruhusiwi.

Vifungu vya Tovuti

Viunganishi

Magharibi

Ardhi za Waislamu

Ardhi za Waislamu