Jumapili, 27 Dhu al-Qi'dah 1443 | 2022/06/26
Saa hii ni: (M.M.T)
Menu
Main menu
Main menu

بسم الله الرحمن الرحيم

 Majibu kuhusu Mgogoro wa Mazingira yako ndani ya Qur'an na Sunnah

(Imetafsiriwa)

Mfumo wa Kirasilimali unaotawala dunia nzima leo ingawa unapiga domo tupu kuhusu kuyajali mazingira kiuhalisia unalenga kuongeza uzalishaji na kuwatajirisha kipote cha mabwenyenye wachache kwa gharama yoyote ile. Hii ni kwa sababu sifa ya asili ya Urasilimali inafafanuliwa na dhana kwamba wanadamu wana "mahitaji yasiyo kikomo katika ulimwengu wenye rasilimali haba za kuwatosheleza wote."

Suluhisho la urasilimali kwa tatizo hili, ni ukuaji wa kudumu ambao huongeza uzalishaji ili kutimiza mahitaji haya yasiyo na kikomo. Urasilimali huona Uzalishaji wa Taifa (Gross Domestic Production) kama kiashirio muhimu cha jinsi nchi inavyofanya vizuri. Kwa lugha nyengine, nchi inazalisha kiasi gani kwa wakati uliowekwa ili kutimiza mahitaji yote yasiyo na kikomo. Na hapa kuna mojawapo ya dosari nyingi za kanuni ya Urasilimali, kwani nchi inaweza kuwa na GPD kubwa huku nusu ya wakaazi wake wanaishi katika umaskini. Hii ni kwa sababu Urasilimali haujaundwa kumtunza kila mtu bali kipote cha mabwenyenye wachache tu, na kuchukua GDP kama kiashirio cha mafanikio hakutatuambia chochote kuhusu jinsi uzalishaji ulivyosambazwa. Madhara yake ni kwamba wachache tu; mabwenyenye, biashara kubwa kubwa na nchi tajiri zitafaidika na kanuni hii, wakati huo huo zikiamua sera. Mazingira ni mmoja tu wa waathiriwa wasioepukika wa muundo wa kasoro hiyo ya kimfumo, ambayo italeta mgongano na sera endelevu za mazingira. Imepelekea kuchomwa kwa rasilimali za thamani na chache za sayari hii ili kuwezesha ukuaji huku ukijaza kila aina ya uchafuzi wa mazingira kwenye mazingira. Kinachofanya mambo kuwa mabaya zaidi ni kwamba mahitaji msingi ya wengi hata hayakidhiwi.

Kinyume kabisa na mfumo wa Kiislamu ambao kimsingi ni tofauti kabisa na Urasilimali. Thamani kuu ya Uislamu ni ugawanyaji wa mali na sio uzalishaji tu. Wajibu wake ni kuhakikisha kwamba kila mtu anapata mahitaji msingi ya maisha, kama vile chakula cha kutosha, malazi na mavazi na si wachache tu.

Mwenyezi Mungu (swt) anasisitiza kuwa mali zisizunguke miongoni mwa wachache, Anasema (swt) akizungumzia mali:

 [كَيْ لَا يَكُونَ دُولَةً بَيْنَ الْأَغْنِيَاءِ مِنْكُمْ]

“Ili yasiwe yakizunguka baina ya matajiri tu miongoni mwenu.” [Al-Hashr: 7]

[وَأَطْعِمُوا الْبَائِسَ الْفَقِيرَ]

“Na mlisheni mwenye shida aliye fakiri.” [Al-Hajj: 28].

Hata tubadilishe sera kiasi gani ili "kulinda" mazingira maadamu mfumo wa kirasilimali bado ungalipo hakuna mabadiliko ya kweli yatakayofanyika. Kwani Urasilimali ndio chanzo cha matatizo mengi yanayowakabili wanadamu. Hili lisije kuwashangaza Waislamu kwani tumeonywa juu ya hili tena na tena katika Quran.

Maafa ambayo wanadamu watakabiliana nayo tunapofuata kitu chengine chochote kando na mwongozo wa Muumba wetu, Uislamu. Demokrasia na urasilimali vina uhusiano wa karibu, na zikiweka msingi wa jamii nyingi za Kirasilimali kuwa wa kisekula, hii ni kutenganisha dini na mambo ya maisha - Inaamini kwamba wanadamu wanapaswa kuamua mema na mabaya kwa msingi wa matamanio yao. Na ni hili haswa, kujiweka mbali na neno la Mwenyezi Mungu (swt), ndilo linalosababisha uharibifu katika kila nyanja ya maisha, yakiwemo mazingira.

Nini hutokea pindi tunapokengeuka kutokana na ujumbe auliotumwa nao Muhammad (saw) kwetu?

 [وَإِذَا تَوَلَّىٰ سَعَىٰ فِي ٱلۡأَرۡضِ لِيُفۡسِدَ فِيهَا وَيُهۡلِكَ ٱلۡحَرۡثَ وَٱلنَّسۡلَۚ وَٱللَّهُ لَا يُحِبُّ ٱلۡفَسَادَ]

“Na anapo tawala hufanya juhudi katika nchi kwa kufisidi humo na kuteketeza mimea na viumbe. Na Mwenyezi Mungu hapendi ufisadi.” [Surah Al-Baqara 2:205].

Ni Uislamu pamoja na wahyi wa Quran ambao ndio chimbuko la milele la mwongozo wa wanadamu unaopanga mambo yote ya maisha na mwongozo huu haswa ndio tulioupuuza kwa miaka mingi.

Mwongozo kutoka kwa Mjuzi wa kila kitu:

 [وَكُلُواْ وَٱشۡرَبُواْ وَلَا تُسۡرِفُوٓاْۚ إِنَّهُۥ لَا يُحِبُّ ٱلۡمُسۡرِفِينَ]

“na kuleni, na kunyweni na wala msifanye ubadhirifu. Kwa hakika Yeye hapendi wanao fanya israfu.” [Surat Al-A’raf 7: 31].

[وَٱلۡأَرۡضَ مَدَدۡنَٰهَا وَأَلۡقَيۡنَا فِيهَا رَوَٰسِيَ وَأَنۢبَتۡنَا فِيهَا مِن كُلِّ شَيۡءٖ مَّوۡزُونٖ * وَجَعَلۡنَا لَكُمۡ فِيهَا مَعَٰيِشَ وَمَن  لَّسۡتُمۡ لَهُۥ بِرَٰزِقِينَ * وَإِن مِّن شَيۡءٍ إِلَّا عِندَنَا خَزَآئِنُهُۥ وَمَا نُنَزِّلُهُۥٓ إِلَّا بِقَدَرٖ مَّعۡلُومٖ]

“Na ardhi tumeitandaza na humo tumeweka milima, na tumeotesha kila kitu kwa kiasi chake. Na tumekujaalieni humo vitu vya maisha yenu, na ya hao ambao nyinyi sio wenye kuwaruzuku. Na hakuna chochote ila asili yake inatokana na Sisi; wala hatukiteremshi ila kwa kipimo maalumu.” [Al-Hijr 15: 19-21].

[وَلاَ تُفْسِدُواْ فِي الأَرْضِ بَعْدَ إِصْلاَحِهَا وَادْعُوهُ خَوْفًا وَطَمَعًا إِنَّ رَحْمَتَ اللّهِ قَرِيبٌ مِّنَ الْمُحْسِنِينَ]

“Wala msifanye uharibifu katika nchi baada ya kuwa imekwisha tengenezwa. Na muombeni kwa kuogopa na kwa kutumai. Hakika rehema ya Mwenyzi Mungu iko karibu na wanao fanya mema!” [Al-A’raf 7: 56]. Na kutoka kwa Mtume wake: Mtume (saw) amesema,

«إِنَّ الدُّنْيَا حُلْوَةٌ خَضِرَةٌ وَإِنَّ اللَّهَ مُسْتَخْلِفُكُمْ فِيهَا فَيَنْظُرُ كَيْفَ تَعْمَلُونَ»

“Hakika duniani ni tamu na rangi ya kijani, na hakika Mwenyezi Mungu amewafanyeni wasimamizi (Makhalifa) ili aone mtakavyofanya”. (Sahih Muslim) Mtume (saw) amesema,

«مَا مِنْ مُسْلِمٍ يَغْرِسُ غَرْسًا، أَوْ يَزْرَعُ زَرْعًا، فَيَأْكُلُ مِنْهُ طَيْرٌ أَوْ إِنْسَانٌ أَوْ بَهِيمَةٌ، إِلاَّ كَانَ لَهُ بِهِ صَدَقَةٌ»

“Hakuna Muislamu yeyote atakayepanda mti, au kupanda mbegu, kisha ndege, au mtu au mnyama akala kutokana nayo, isipokuwa hilo itakuwa ni sadaka kwake”. (Sahih al-Bukhari)

Abu Hurayrah (ra) amesimulia kwamba watu walimuuliza Mtume (saw) kuhusu ujira wa kuwahudumia wanyama. Mtume (saw) akajibu,

«فِي كُلِّ كَبِدٍ رَطْبَةٍ أَجْرٌ»

“Kuna ujira kwa kila kiumbe hai anayehudumiwa”. (Sahih al-Bukhari)

Chukua muda wa kutafakari juu ya umuhimu wa jumbe hizi muhimu katika ulimwengu tunaoishi hivi leo na utambue jukumu zito lililo juu ya Waislamu la kurekebisha matatizo mengi ya wanadamu na kurudisha uadilifu mkubwa wa Uislamu.

#أزمة_البيئة    #EnvironmentalCrisis

Imeandikwa kwa Ajili ya Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir na
Yasmin Malik
Mwanachama wa Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir

Andika maoni

Hakikisha umejaza (*) habari zinazohitajika palipoashiriwa. Kodi za HTML haziruhusiwi.

rudi juu

Vifungu vya Tovuti

Viunganishi

Magharibi

Ardhi za Waislamu

Ardhi za Waislamu