Jumamosi, 28 Shawwal 1443 | 2022/05/28
Saa hii ni: (M.M.T)
Menu
Main menu
Main menu

بسم الله الرحمن الرحيم

 Uhusiano wa Nyaraka za Pandora na Ufukara wa Dunia

(Imetafsiriwa)

Katika msimu wa kipupwe wa Oktoba 2021, Nyaraka za Pandora zilifichuliwa kwa walimwengu. Huu ulikuwa ni mvujo wa takriban makala milioni 12 ambazo zimefichua namna ya watu matajiri zaidi wa dunia wanavyofyonza utajiri (unaopatikana mara nyingi kwa njia zisizo halali) na kuuficha katika namna tafauti. Baadhi ya mbinu zenye utata zikiwemo ukwepaji kodi na ulanguzi wa fedha kwa ushirikiano kutoka kila hatua ya wenye ushawishi wakiwemo baadhi ya Wakurugenzi Wakuu wakubwa duniani na wanasiasa wenye nguvu.

Kufichuliwa kwa shughuli hizi za kilaghai za kiuchumi zinazofikia kiwango cha ufisadi wa kutisha katika baadhi ya hali ilikuwa ni matokeo ya mafaili ya uchunguzi wa wanahabari 600 katika nchi 117 kutoka vyanzo 14 uliochukua miezi mingi. Muungano wa Kimataifa wa Wanahabari za Kiuchunguzi (ICIJ) jijini Washington DC, ambao unafanyakazi na zaidi ya taasisi za habari 140 juu ya uchunguzi mkubwa zaidi wa kidunia. BBC Panorama na Guardian zimeongoza uchunguzi nchini Uingereza.

Mafaili yamefichua namna ya baadhi ya watu wenye nguvu zaidi duniani – wakiwemo zaidi ya wanasiasa 330 kutoka nchi 90 – walivyotumia makampuni ya siri yaliosajiliwa ng'ambo (offshore companies) kuficha mali zao.

Lakshmi Kumar kutoka jumuiya ya washauri mabingwa wa Global Financial Integrity ya Amerika alielezea kuwa watu hawa “wana uwezo wa kuchuja na kufyonza fedha na kuzificha,” mara nyingi kupitia utumiaji wa makampuni yenye utambulisho fiche.

Kwa nini hawa wenye utajiri mkubwa zaidi huchagua njia hizi kuficha utajiri wao kwa kutumia akaunti za makampuni haya na ni nani hao?

Nchi au maeneo ya kuwekeza makampuni kwa kificho yapo nje ya eneo la mtu anapoishi na hutoa faida zifuatazo:

.  Ni rahisi kuweka makampuni

. Kuna sheria zinafanya kuwa vigumu kuwatambua wamiliki wa makampuni        

.  Kuna kodi ndogo ya mashirika au huwa hakuna kabisa

Maeneo haya mara nyingi huitwa makimbilio ya maficho ya kodi au mamlaka za siri. Hakuna orodha ya wazi ya maeneo haya, lakini maeneo maarufu yanayojulikana yanajumuisha Mamlaka za British Overseas, kama visiwa vya Cayman na Visiwa vya British Virgin, pamoja na nchi kama Uswizi na Singapore.

Mfumo huu unawekwa kama ni “siri” lakini kwa hakika ni chombo kinachojulikana kinachotumiwa na matajiri wakubwa kuhodhi kiasi kikubwa cha rasilimali ambazo mara nyingi hazipaswi kuwa katika milki yao.

Katika kujihami kwao, baadhi hudai kuwa hakuna kosa kwa kutumia njia hizi katika kutumia “mwanya” kwenye sheria. Suala la kuwa kwake ni tendo lisilo la maadili kabisa ni habari za uwongo kwa kundi la watu waliofungamana kwenye janga hili la kifedha. Jambo la kuzingatia kwa Waislamu duniani ni suala la kuwa orodha ya mamia ya maafisa walionaswa katika mtandao huu wa udanganyifu unahusisha watawala wengi na viongozi wa ulimwengu wa Kiislamu.

Kukiwa na wengi wanaoteseka na umasikini ukiwakumba kote duniani kuanzia Afghanistan, Syria, Lebanon, Afrika na Asia kutaja kwa uchache, ni matusi kwa umma ambapo viongozi wetu wamekuwa wachoyo na makatili, ni hali isioweza kuachwa bila kuhojiwa.

Hakuna kiasi halisi cha fedha zilizofichwa katika akaunti hizi (offshore) kinachofahamika, lakini ICIJ imehitimisha kuwa inaweza kufikia dolari trilioni 32.

Kwa nini hili ni tatizo? Mfuko wa Fedha wa Kimataifa umesema matumizi ya maficho ya kodi yanazikosesha serikali hadi dolari bilioni 600 kama malipo ya kodi kila mwaka kote duniani. Ms. Kumar amesema hii ni kuleta hasara kwa jamii iliyosalia: “Uwezo wa kuficha fedha una athari ya moja kwa moja juu ya maisha yako… unaathiri uwezo wa kupata elimu kwa mtoto wako, uwezo wa kupata matibabu, uwezo wa kupata makaazi.”

Baadhi ya miamala michafu iliofichuliwa inajumuisha;

Familia ya watawala wa Qatar imekwepa kodi ya Pauni milioni 18.5 katika ununuzi wa kasri moja kuu la London.

Familia ya raisi Uhuru Kenyata wa Kenya inamiliki kwa siri mtandao wa makampuni ya ng'ambo kwa miongo kadhaa.

Tukio la manunuzi ya israfu ya Pauni milioni 70 ya Mfalme wa Jordan. Mkondo wa Nyaraka za Pandora umegundua kuwa Mfalme wa Jordan alifanya matumizi ya kifahari ya pauni milioni 70 kununulia rasilimali Uingereza na Amerika kupitia makampuni yake ya siri.

Familia inayoongoza Azerbaijan imehusika na miamala ya mali zilizofichwa nchini Uingereza zenye thamani ya zaidi ya Pauni milioni 400.

Kwa mifano ya wazi ya namna watawala wa ulimwengu wa Kiislamu wanavyonyonya kiasi kikubwa cha utajiri usiowekwa wazi kwa maslahi yao, tunaweza kuona kwa nini wanapendelea sana kuyaweka masuala yao ya kiuchumi kuwa siri.

Nyaraka za Pandora zinaonyesha tabia hii inaungwa mkono kimataifa na kipote cha mabwenyenye wachache duniani wanaosaidiana katika uovu wao.

Mahangaiko yanayoendelea na kutokuwepo usawa wa kijamii ambao ni hali ya kudumu kwa raia wengi wa dunia ni jambo lililoundwa kimkakati.

Maelezo kuhusu idadi kubwa wa watu na kutolingana kwa ikolojia (baina ya maeneo ya dunia) ni sababu duni zaidi za umasikini wa dunia na kunyimwa.

Mwenyezi Mungu (swt) ametueleza kuwa kwa kila kiumbe kuna riziki imetolewa na hivyo hatupaswi kuhofia uchache wake.

[وَاللّهُ فَضَّلَ بَعْضَكُمْ عَلَى بَعْضٍ فِي الْرِّزْقِ فَمَا الَّذِينَ فُضِّلُواْ بِرَآدِّي رِزْقِهِمْ عَلَى مَا مَلَكَتْ أَيْمَانُهُمْ فَهُمْ فِيهِ سَوَاء أَفَبِنِعْمَةِ اللّهِ يَجْحَدُونَ]

“Na Mwenyezi Mungu amewafadhilisha baadhi yenu kuliko wengine katika riziki. Na wale waliofadhilishwa hawarudishi riziki zao kwa wale iliowamiliki mikono yao ya kulia ili wawe sawa katika riziki hiyo. Basi je, wanazikataa neema za Mwenyezi Mungu?” [An Nahl: 71]

Ummah wa Kiislamu lazima ufichue sababu halisi ya ufisadi kote katika nchi zetu, yote hufanywa kwa msaada wa mataifa ya nje ya Kimagharibi kujinufaisha kutokana na watawala vibaraka.

Usimamizi mbaya na kizingiti chenye kudhibitiwa cha kurejea kwa Khilafah yote hutumiwa kuficha nyayo za uharibifu ambazo zimeachwa huru chini ya sera za kiliberali za demokrasia ya kibepari.

Fahamu ya mfumo wa uchumi wa Kiislamu na kanuni zake kali unaobainisha kwa uwazi mali ya ummah na ya binafsi kuwa ndio suluhisho halisi kwa maradhi ya ulafi yanayoambukiza wale wote walio madarakani.

Chini ya uongozi wa Umar Ibn Khattab, mali asili na uzalishaji wa ardhi ilikuwa ni maeneo muhimu ya usimamizi wa uchumi. Ardhi, kama mali asili nyengine hazikuruhusiwa kudhibitiwa au kulimbikizwa na watu wachache wenye nguvu, ilikuwa ni njia ya uzalishaji. Ardhi iliyopatikana kutoka maeneo yaliyokombolewa yaliachwa katika mikono ya wamiliki wake wa asili ambao wana uwezo mkubwa zaidi kuliko Waarabu katika kuyalima. Zaidi ya hivyo, katika kutoza kodi maalum ya ardhi (Kharaj) kuliwaongoza watu katika kuongeza na kueneza utajiri na kuongeza manufaa ya ardhi  kuwa ni njia ya uzalishaji. Hali ya sasa ya kukosekana usimamizi wa Zaka humaanisha mamilioni ya wastahiki hawapati haki yao ya kila mwaka ya usambazaji wa utajiri na tunafahamu utumiaji mbaya ulioenea wa chapa ya fadhila kutumika kwa Zaka.

Ni chini ya Khilafah tu ndipo uwajibikaji wa kweli utaweza kurejeshwa, na hii ndio sababu kwa nini kunakuwepo kampeni ya nguvu ya kuzuia kazi ya kisiasa na kueneza uongo wa kuwa Uislamu sio siasa na hauna mfumo maalum wa utawala.

Pindi Ummah unapoona mwangaza wa sera sahihi, hautofikiria kuchukua chaguo bandia au kubadilisha kwa kile ambacho Mwenyezi Mungu (swt) amekitengeneza katika mfumo adilifu ulio kamili.

Nyaraka za Pandora sio suala lisiloeleweka. Ufisadi na utumiaji mbaya wa madaraka utaendelea baada ya majina kusambazwa. Watu waliotumia sheria kutumikia maslahi yao binafsi haielekei kabisa kuadhibiwa kwa makosa yao. Khilafah itayafanya matendo kama haya kuwa ni suala la ummah linalobeba matokeo mazito ambayo viongozi katika kila ngazi watahofia kujiingiza au kuyaficha matendo hayo yenye kuleta hizaya.

Imeandikwa kwa Ajili ya Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir na

Imrana Mohammad

Mwanachama wa Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir

Andika maoni

Hakikisha umejaza (*) habari zinazohitajika palipoashiriwa. Kodi za HTML haziruhusiwi.

rudi juu

Vifungu vya Tovuti

Viunganishi

Magharibi

Ardhi za Waislamu

Ardhi za Waislamu