- |
- Kuwa wa kwanza kutoa maoni!
- ukubwa wa font punguza ukubwa wa font zidisha ukubwa wa font
بسم الله الرحمن الرحيم
Uislamu Uliingiaje Sudan?
(Imetafsiriwa)
Kabla ya kuwasili kwa Uislamu, eneo linalojulikana leo kama Sudan halikuwa umbo lililounganishwa kisiasa, kitamaduni au kidini. Ilikuwa makao ya makabila, desturi, na imani mbalimbali. Upande wa kaskazini, Wanubi walifuata Ukristo wa Kiorthodoksi, na lugha ya Kinubi, pamoja na lahaja zake mbalimbali, ilikuwa njia ya siasa, utamaduni, na mawasiliano. Katika mashariki, makabila ya Beja, vizazi vya Hamu (mwana wa Nuhu), walikuwa na lugha yao wenyewe tofauti, utamaduni, na matendo ya kidini. Upande wa kusini, makabila ya Zanj, yenye sifa na lugha zao za kipekee, yalishikamana na imani za kipagani, na tofauti kama hizo zilikuwepo katika upande wa magharibi. (1)
Tofauti hii ya kikabila na kitamaduni ilikuwa alama mahususi ya watu wa Sudan kabla ya Uislamu, ikifinyangwa kwa eneo lake la kimkakati la kijiografia kaskazini mashariki mwa Afrika. Sudan ilitumika kama lango la kuingia kwenye Pembe ya Afrika na daraja kati ya ulimwengu wa Kiarabu, Afrika Kaskazini, na Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara. Bandari zake muhimu kwenye Bahari Nyekundu, njia kuu ya biashara ya kimataifa, iliboresha zaidi dori yake katika kihadhara, kitamaduni, kisiasa, na ubadilishanaji wa kiuchumi katika kipindi chote cha historia.
Uhusiano wa kwanza wa awali kati ya Uislamu na Sudan unaweza kufuatiliwa hadi kuhama kwa maswahaba wa Mtume kwenda Abyssinia “Alhabacha” (mwezi Rajab katika mwaka wa tano wa Utume/mwaka wa pili wa kutangazwa hadharani kwa Uislamu). Ingawa madhumuni msingi ya uhamiaji huu yalikuwa kutafuta kimbilio kutoka kwa mateso mjini Makka, iliashiria uwepo wa awali wa Uislamu katika muktadha wa Afrika na Sudan. Mnamo mwaka wa 6 Hijria, Mtume Muhammad (saw) alituma barua pamoja na mjumbe wake, Amr ibn Umayyah, kwenda Najash, wakimualika kwenye Uislamu. Najash alijibu vyema (2).
Kwa kufunguliwa kwa Misri na Amr ibn al-As wakati wa khilafah ya Umar ibn al-Khattab mwaka wa 20 H/641 M, Wanubi walihisi kutishiwa wakati dola ya Kiislamu ilipoanza kuimarisha udhibiti wake wa kiutawala na kisiasa juu ya Bonde la Nile la kaskazini, hasa Misri ya Juu, ambayo ilikuwa na mafungamano ya kimkakati na kijiografia na falme za Kinubi nchini Sudan. Kwa kujibu, falme za Kinubi zilianzisha mashambulizi ya mapema dhidi ya Misri ya Juu. Khalifa Umar ibn al-Khattab alimuamuru Amr ibn al-As, gavana wa Misri, kutuma misafara ya kijeshi katika ardhi ya Wanubi ili kulinda mipaka ya kusini mwa Misri, kulinda njia za kibiashara, kuondoa nguvu yoyote iliyo tiifu kwa Milki ya Byzantine na kufikisha ujumbe wa Uislamu. Mnamo mwaka wa 21 Hijria, Amr alituma jeshi likiongozwa na Uqba ibn Nafi al-Fihri, lakini Waislamu walilazimika kurudi nyuma kutokana na upinzani mkali kutoka kwa Wanubi, ambao walikuwa wapiga mishale mahiri wenye uwezo wa kufuma kwa usahihi, hata kulenga macho. Hii iliwapa jina la utani "Wafuma mishale wa Macho" (Rumat al-Hadaq).
Mnamo mwaka wa 26 H / 647 M, Abdullah ibn Sa'd ibn Abi Sarh aliteuliwa kuwa gavana wa Misri wakati wa khilafah ya Uthman ibn Affan. Alitayarisha kampeni yenye vifaa vya kutosha dhidi ya Wanubi, ikisonga mbele kuelekea kusini hadi Dongola, mji mkuu wa ufalme wa Kikristo wa Wanubi, mwaka wa 31 H/652 M.
Kabla ya Uislamu, Nubia iligawanyika katika falme 3, Nuba (Nobatia), Muqurra, na Alawa (kutoka Aswan kusini hadi Khartoum leo), kisha baada ya hapo, falme za Nuba na Muqurra ziliungana kati ya 570 M hadi 652 M na uliitwa Ufalme wa Nuba, na mji mkuu wake ulikuwa Dongola.
Baada ya kuzingirwa kwa vikali, Wanubi waliomba amani, na Abdullah akakubali (3). Mkataba unaojulikana kama “Baqt” ulihitimishwa na msikiti ukajengwa huko Dongola. Wanazuoni wamejadili maana ya “Baqt,” wengine wakipendekeza linatokana na neno la Kilatini “Pactum,” linalomaanisha makubaliano. Wanahistoria na waandishi hawaoni upatanisho huu kama mikataba mingine ya amani ambayo Waislamu waliweka jizya kwa wale waliopatana nao, bali kama makubaliano au mapatano kati ya Waislamu na Nuba.
Mkataba huo uliwapa usalama Wanubi, ukiweka masharti kwamba Waislamu hawatawashambulia, na Wanubi wanaweza kupita katika ardhi za Waislamu kama wasafiri lakini wasiishi humo. Wanubi walitakiwa kumlinda Muislamu au mshirika yeyote anayeingia katika eneo lao, kudumisha msikiti uliojengwa na Waislamu huko Dongola, na kutoa wakuu wa watumwa 360 kila mwaka. Kwa kujibu, Waislamu waliwapa nafaka na nguo (kwa kuwa mfalme wa Nubia alilalamika juu ya uhaba wa chakula) lakini hawakuwa na wajibu wa kuwalinda dhidi ya maadui. Mkataba huu ulihakikisha usalama wa mipaka ya Waislamu, kuwezesha biashara ya mipakani, na kuruhusu nguvu za Wanubi kutumikia dola ya Kiislamu. Baada ya muda, fikra zilienea kupitia biashara, na wafanyibiashara na wahubiri wa Kiislamu walicheza dori muhimu katika kueneza Uislamu kwa amani, hasa kupitia tabia nzuri. Hivyo, misafara ya biashara ilibeba fikra, lugha, hadhara, na mfumo wa maisha pamoja na bidhaa za biashara.
Lugha ya Kiarabu pia ilipata umaarufu katika maisha ya kila siku, haswa kaskazini mwa Sudan. Mkataba wa Baqt ulianzisha mawasiliano ya kudumu kati ya Waislamu na Wanubi Wakristo kwa karne sita. (5) Katika kipindi hiki, Uislamu ulienea polepole kaskazini na mashariki mwa Sudan kuanzia katikati ya karne ya 7 M kupitia wafanyibiashara Waislamu na wahamiaji Waarabu. Uhamiaji huu mkubwa wa Waarabu ulipenyezwa kupitia njia 3: Ya kwanza Kutoka Misri, ya pili kutoka Hijaz kupitia bandari kama Bada'a, Aydhab na Suakin, na ya tatu: Kutoka Morocco na Afrika Kaskazini kupitia Sudan ya kati. Hata hivyo, athari za uhamiaji huu wa awali ulikuwa mdogo ikilinganishwa na harakati kubwa za Waarabu kutoka Misri kuelekea kusini kuanzia karne ya 9 M. Hapo nyuma, mabadiliko yalikuja wakati wa utawala wa Khalifa wa Abbasiyya al-Mu'tasim (218-227 H / 833-842 M), alipotegemea askari wa Kituruki na kuwatenga askari wa Kiarabu, na kusababisha uhamiaji mkubwa wa Waarabu kuingia Sudan. Kufurika huku kulisababisha kutia Kiarabu maeneo ya Beja, Nubia, na Sudan ya kati. Kwa hiyo, karne ya 3 H / karne ya 9 M ilishuhudia uhamiaji mkubwa wa Waarabu kwenda Sudan na kisha wakapenya tambarare kubwa kusini na mashariki. (6) Kuishi katika maeneo haya kulisaidia katika kuwasiliana na kuwashawishi watu wa nchi hiyo na kuwashawishi kuukubali Uislamu na kusilimu.
Kufikia karne ya 12 M, baada ya Makruseda kuiteka Palestina, njia ya Sinai ikawa sio salama kwa mahujaji wa Misri na Maghrebi, ambao waligeukia bandari ya Aydhab (iliyojulikana kama “Bandari ya Dhahabu”). Mabadiliko haya yalikuza umuhimu wa kidini na kibiashara wa Aydhab, kwani ikawa kitovu cha mahujaji na biashara na Yemen na India. (7)
Mnamo 1272 M, Mfalme Daudi wa Nubi alipokiuka mkataba kwa kushambulia Aswan, Waislamu, chini ya Sultan al-Zahir Baybars, walilazimika kulipiza kisasi. Mkataba mpya ulitiwa saini mnamo 1276 M. Hatimaye, mwaka wa 1317 M, Sultan al-Nasir Muhammad ibn Qalawun aliifungua Dongola baada ya mpwa wa Mfalme Daudi, Abdullah, kusilimu mwaka wa 1316 M, na kuwezesha kuenea kwa Uislamu huko Nubia. (8)
Ama Ufalme wa Kikristo wa Alwa ulianguka mnamo 1504 M baada ya muungano kati ya makabila ya Waarabu Abdallab na Funj, na kusababisha kuanzishwa kwa Usultani wa Kiislamu wa Funj, unaojulikana pia kama “Usultani wa Samawati ” au “Usultani wa Sennar.” Hii ikawa dola ya kwanza ya Kiarabu na Kiislamu nchini Sudan baada ya kuenea kwa Uislamu na Kiarabu. (9)
Ushawishi wa Waarabu na Uislamu ulipokua, familia zinazotawala huko Nubia, Alwa, Sennar, Taqali, na Darfur zilikubali Uislamu baada ya kuwa Wakristo au wapagani. Kusilimu kwa tabaka tawala kulipelekea mapinduzi ya pande nyingi katika historia ya Sudan. Familia za watawala wa Kiislamu zilianzishwa, na pamoja nazo, vielelezo vya kwanza vya falme za Kiislamu za Sudan vilianzishwa, jambo ambalo lilikuwa na taathira kubwa katika kuipa nguvu dini hii na kuchangia ipasavyo katika kueneza Uislamu, kusimamisha nguzo zake na kuweka misingi ya hadhara ya Kiislamu katika ardhi ya Sudan. Baadhi ya watawala hao wa Kiislamu wakawa watetezi wa Uislamu, wakihimiza uadilifu, wakiamrisha mema, na kukataza maovu.
Kwa hilo, Uislamu ulienea kwa nguvu katikati ya mashinikizo ya wapagani na wamisionari wa Kikristo, huku misafara ya biashara na wasomi wakicheza dori muhimu. Uenezaji wa amani wa Uislamu kwa njia ya ushawishi, dalili, na muamala mzuri ukawa alama mahususi ya historia ya Kiislamu ya Sudan. Kama ilivyobainishwa na mwanachuoni Abu al-Abbas Ahmad Baba al-Timbukti: “Watu wa Sudan walisilimu kwa khiyari yao bila ya mtu yeyote kuwakamata, kama vile watu wa Kano na Borno, na hatujapata kusikia kwamba kuna mtu aliwateka kabla ya kusilimu.” (11)
#أزمة_السودان
#SudanCrisis
Imeandikwa kwa Ajili ya Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir
Mhandisi Dorra Baccouche
Maregeo
(1) The Entry of Islam into Sudan and Its Impact on Correcting Beliefs, Dr. Salah Ibrahim Issa
(2) Tanzir al-Ghubash fi Fadl Ahl al-Sudan wa-l-Habash, Ibn al-Jawzi
(3) Futuh al-Buldan, al-Baladhuri
(5) Islam in Sudan, J. Spencer Trimingham
(6) The Spread of Islam in Sub-Saharan Africa, Yusuf Fadl Hasan
(7) Sudan Through the Ages, Dr. Maki Shubayka
(8) Sudan, Mahmud Shakir
(9) A Study of the Funj Islamic Kingdom (910–1237 AH/1504–1821 CE), Dr. Tayyib Bujumah Na'ima
(10) Islam and Nubia in the Middle Ages, Dr. Mustafa Muhammad Sa'd
(11) Studies in the History of Islam and Ruling Dynasties in Sub-Saharan Africa, Dr. Nur al-Din al-Sha'bani